Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.44 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo pamoja na taasisi zake kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.
Matumizi ya Kawaida: Shilingi trilioni 1.95 sawa na asilimia 80% zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Katika kiasi hiki, Shilingi trilioni 1.18 zitaenda kwenye mishahara ya watumishi, huku Shilingi bilioni 769.5 zikiwa ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Miradi ya Maendeleo: Jumla ya Shilingi bilioni 489.8 sawa na asilimia 20% zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wizara.
Akifafanua kuhusu fedha za miradi ya maendeleo, Waziri Katambi amebainisha kuwa serikali itajitegemea kwa kiasi kikubwa ambapo Shilingi bilioni 453.9 (92.7%) ni fedha za ndani, huku Shilingi bilioni 35.8 (7.3%) pekee zikiwa ni fedha kutoka nje (kwa wahisani).