Wizara ya Elimu ya China yawapa nafuu wazazi wakati shule zinapofungwa kwenye likizo ndefu ya majira ya joto

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,008
1,032
VCG111340927995.jpg


Majira ya joto yamefika na tunapozungumzia majira ya joto, huwa mara nyingi kwa wanafunzi wa nchi mbalimbali pia wanazungumzia likizo yao ndefu hasa kwa nchi zile zenye misimu ya joto, baridi, mpukutiko na spring au mchipuko.

Katika kipindi hiki baadhi ya wanafunzi huwa wanajiunga na kambi za majira ya joto ambazo kwa lugha ya wenzetu wanaita “summer camp” na wengine huwa wanajiunga na madarasa ya kawaida ambayo yanatoa kozi mbalimbali. Lakini kwa nchi zetu za Afrika wanafunzi wengi, likizo hii ambayo kwao wao ni ya kumaliza muhula wa kwanza, huwa wanaitumia kutembea ama kupumzika hasa nyumbani. Pia baadhi ya wazazi huwa wanatumia muda huu kuwahamasisha watoto wao kusaidia kazi mbalimbali za nyumbani, kwani zinapofungwa shule ndio muda pekee ambao wanafunzi wanakuwa nafasi. Lakini wazazi wengine huwa wanapendelea kutumia muda huu kuwaendeleza kimasomo watoto wao kwa kuwatafutia madarasa ya ziada.

Sekta ya elimu nchini China mwaka huu imeshuhudiwa ikifanya marekebisho mengi yanayohusu elimu yakiwa na lengo la kuwapunguzia mzigo wazazi wanaofanya kazi, ambao hawana muda wa kuwaangalia na kuwashughulikia watoto wao nyumbani. Hivi sasa mamlaka za elimu katika miji kadhaa zimetangaza kutoa huduma ya kuwaangalia wanafunzi wa shule za msingi wakati wa mchana katika kipindi hiki cha likizo ya majira ya joto ambayo mwaka huu imeanzia katikati ya mwezi Julai.

Huduma hii inatolewa kwa mujibu wa mahitaji ya wanafunzi. Na cha kufurahisha zaidi ni kwamba huduma hii si ya lazima, kila mzazi wa mwanafunzi ana hiari ya kuamua kumpeleka mtoto wake ama la. Shule nazo zinatakiwa kufungua maktaba pamoja na viwanja vya michezo ili wanafunzi waweze kutumia katika kipindi cha likizo yao. Pia zinaruhusiwa kupanga shughuli za michezo kwa wanafunzi, lakini haziruhusiwi kutoa mafunzo ya kielimu au kuwafunza wanafunzi kwani huu si muda wa wanafunzi kusoma bali ni muda wa kufurahia utoto wao na kucheza pamoja.

Katika mji wa Beijing, kila wilaya ndogo inahitajika kufungua angalau shule moja ili kutoa huduma hiyo kwa wanafunzi wa shule ya msingi kutoka darasa la kwanza hadi la tano. Hata hivyo mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Elimu wa Karne ya 21 ya Beijing, Xiong Bingqi, anasema shule zisiwalazimishe walimu wote kushiriki kutoa huduma hii ya matunzo ya watoto shuleni, kwani na wao pia wanahitaji kupumzika katika kipindi cha likizo.

Mabadiliko yoyote yale katika jamii huwa yanapokelewa kwa mitazamo tofauti, kuna wale wanaounga mkono na wale wasiounga mkono. Lakini inaonekana safari hii hatua hii imewafurahisha wazazi wengi pamoja na jamii kwa ujumla, kwani sio tu inapunguza shinikizo la wanafunzi kwenye vituo vinavyotoa mafunzo, bali pia inawaondolea mzigo mzito wazazi wanaofanya kazi ambao wanalazimika kuwatunza watoto wao wakati wakiwa kwenye likizo yao.

Nakumbuka katika likizo za wanafunzi za miaka iliyopita tulikuwa tukishuhudia watoto wengi kwenye maeneo yetu ya kazi wakizunguka na kucheza, kutokana na wazazi wao kulazimika kuwabeba kazini kwa vile nyumbani hawana watu wa kuwaangalia. Lakini mwaka huu hali imekuwa tofauti kabisa, yote haya ni kutokana na hatua mpya iliyochukuliwa na wizara ya elimu ya China ambayo inaoneka kuridhisha wazazi wengi wanofanya kazi.

Wanafunzi wengi walioanza kujaribu huduma hiyo wanasema kwamba ni nzuri kwani shughuli wanazofanya zinawavutia zaidi kuliko walivyotarajia. Ingawa awali baadhi ya wanafunzi hao walidhani kwamba huduma hiyo inaweza kuwachosha na kulazimika kufanya kazi za darasani, lakini matokeo yake baada ya kujaribu wamejikuta wakituliza akili zao na kupata marafiki wa kila aina. Kuna kauli moja ya Kingereza inayotumika sana yaani “win win” na kweli hapa tunaona hatua hii inanunufaisha pande zote, yaani wazazi, wanafunzi na hata shule pia.

Lakini ushauri wangu kwa wazazi, ni kwamba wasisahau ule msemo usemao “Ng’ombe hashindwi na nundu yake” hivyo madarasa haya ya mchana ya kuwaangalia wanafunzi, yasichukuliwe kama mbadala au kuchukua nafasi ya wajibu wa wazazi kwa watoto wao katika kipindi cha likizo. Bali wazazi wanatakiwa kutenga muda wao na kukaa na watoto wao wakati shule zimefungwa, kwani kufanya hivi kutajenga mahusiano mazuri zaidi kati ya mzazi na mtoto wake.
 
Back
Top Bottom