Wizara ya Afya: Watu Milioni 2.4 Tanzania wana matatizo ya macho

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Zaidi ya watu milioni 2.4 nchini wana matatizo ya kuona huku ugonjwa wa kisukari ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu saba zinazochangia hali hiyo.

Kutokana na hali hiyo, serikali imeandaa mkakati mwingine wa kukabiliana na tatizo la macho unaotarajiwa kusogeza huduma za macho karibu na wananchi.

Mkurugenzi wa Tiba katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Magembe, alisema jana kuwa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha asilimia moja ya watu kwenye nchi zinazoendelea na za uchumi wa kati wana ulemavu wa kuona.

Dk. Magembe alikuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani huku akibainisha kuwa Tanzania kuna watu 600,000 wenye ulemavu wa kuona.

“Pia watu wenye matatizo ya kuona kwa kiwango cha kati na juu hapa nchini wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasioona ambao ni takribani watu milioni 1.8. kwa ujumla Tanzania ina watu milioni 2.4 wenye matatizo ya kuona,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema watu wanaokaa kwa muda mrefu kwenye runinga na kompyuta wako hatarini kupata upofu kutokana na mwanga wa vitu hivyo kuwa na athari.

Alitaja visabababishi ambavyo vinaweza kuzuilika ni pamoja na upeo mdogo wa macho kuona au uoni hafifu unaorekebishika kwa miwani, mtoto wa jicho, shinikizo la jicho, makovu kwenye kioo cha mbele cha jicho, vikope, tatizo la retina linalotokana na ugonjwa wa kisukari.

Pia alisema upofu wa utotoni utokanao na upungufu wa Vitamin A, mtoto wa jicho, maambukizi ya surua, kisonono kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na saratani ya macho kwa watoto.

“Iwapo una tatizo la kisukari, hakikisha umefanyiwa uchunguzi maalum wa macho hata kama huna dalili yoyote na kufuata maelekezo ya daktari kwa kuwa ugonjwa huu una sababisha tatizo kwenye retina,” alisema.

Mkurugenzi huyo alitaja hatua mbalimbali ambazo serikali imechukua kupambana na upovu unaozuilika kuwa ni kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya ya macho kutoka asilimia 75 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 93.9 hivi sasa.

“Pia miundombinu imeboreshwa ya huduma za upasuaji wa macho kwenye hospitali za mikoa 26 nchini,” alisema.

Alisema pia huduma za uchunguzi wa macho kwenye kliniki za kisukari zimeongezeka kutoka wagonjwa 14,000 mwaka 2017 hadi kufikia 22,000 mwaka 2019.

Akizungumzia mkakati mpya, Dk. Magembe alisema unalenga kuimarisha huduma za macho za msingi sambamba na kutoa huduma za afya ya msingi ngazi zote.
 
Back
Top Bottom