Wizara ya Afya kutumia uvumbuzi wa Chuo Kikuu cha SUA kwa kutumia panya wenye uwezo wa kugundua vimelea vya kifua kikuu

Wizara ya Afya Tanzania

Official Account
Oct 1, 2020
58
124
Na Emmanuel Malegi-Morogoro

Wizara ya Afya imeshaanza kutumia teknolojia ya Panyabuku katika kubaini ugonjwa wa Kifua Kikuu (Tuberculosis ) kwa sampuli za wagonjwa wenye dalili hizo ili kuongeza uwezo wa kutambua vimelea hivyo hasa pale ambapo njia zingine zimekuwa zimeshindwa kubaini.

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi ambaye alitembelea kitengo hicho cha APOPO katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro amepongeza mapinduzi kutoka kwa Wanasayansi Wazalendo ya kuwawezesha Panya buku wa Chuo Kikuu hicho kunusa na kubaini vimelea vya Kifua Kikuu katika sampuli za makohozi yanayoletwa hapo kwa ajili ya vipimo vya Kifua Kikuu, na ameelekeza kufikia mwaka huu huduma hii iweze kuzifikia zaidi ya Hospitali 100 nchini.

“Nawapongeza sana watafiti wa SUA kwa hatua ambayo mmefikia, kituo hiki baada ya kukitembelea tumeona kuwa kimekua kikifanya ugunduzi wa vimelea vya kifua kikuu kwa kutumia hawa Panya. Lakini pia wameweza kuwafundisha na kusambaza hiyo Teknolojia katika nchi mbalimbali kama vile Msumbiji na Ethiopia ambako wanafanya kazi ya kupima ugonjwa wa Kifua kikuu, na kwenye nchi za Cambodia na Angola ambako wanafanyakazi ya kutambua mabomu ya ardhini”. Amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema Panya hao wana uwezo mkubwa wa kugundua vimelea vya Kifua Kikuu hata kwa mtu ambaye alifanya vipimo Hospitalini kama vile vya hadubuni (microscope) na mashine za kupima vinasaba mfano GeneXpert na vipimo vingine na vikatoa majibu kuwa hana TB, lakini panya hao wana uwezo wa kubaini vimelea ambavyo mashine za Hospitalini zinaweza zisibaini. Hii inaonyesha utumiaji wa panya hawa unaweza kusaidia kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wengi zaidi. Panya mmoja anauwezo wa kugundua kama sampuli ina vimelea vya kifua kikuu kwa muda wa sekunde moja, na hupima sampuli za makohozi 100 kwa dakika 20 hivyo teknolojia hii inaweza kutumika hata kwenye upimaji wa sampuli nyingi kutoka kwenye kundi kubwa la watu (mass Screening) kwa muda mfupi.

Mganga Mkuu wa Serikali aliweza kushuhudia Panya ajulikanae kwa jina la Justine aliyeweza kupima sampuli 60 za makohozi ndani ya dakika tano na kugundua sampuli sita zenye vimelea vya Kifua Kikuu.

Mpaka sasa huduma hiyo inatolewa katika Hospitali 74 na kuweza kubaini wagonjwa 14,680 ambao hawakuweza kugundulika kwa njia za kawaida. Hii imesaidia wagonjwa 8,119 kuanza matibabu ambayo yamezuia maambukizi ya kifua kikuu kwa wanachi 81,190 hadi 121,785 ambao wangeweza kuambukizwa kutokana na mgonjwa mmoja ambaye hajatibiwa anaweza kuambukiza ugonjwa huu kwa watu wa karibu naye 10 hadi 15 kwa mwaka.

“Hatua hii inanipa faraja sana kama Sekta ya Afya kwa sababu dhumuni la Sekta hii ni kulinda afya za watu wake. Tunapopata kipimo kama hiki kitasaidia wananchi wengi kuweza kujua afya zao na matokeo yake tutaokoa wananchi wengi kwa kupata tiba na kufanya maisha yao yaweze kuwa marefu zaidi lakini pia tunapunguza uwezekano wa kusambaza ugonjwa huo kwa watu wengine”. Ameongeza Prof. Makubi.

Aidha, Mganga Mkuu huyo aliahidi kulifanyia kazi ombi la Mkuu wa Mradi wa kutambua Kifua Kikuu kupitia Panya Buku Dr. Georgies Mgode la kuitambua Teknolojia hiyo ya Panya katika Mwongozo wa Kutibu Kifua Kikuu hapa nchini.

Pamoja na hayo, Mganga Mkuu huyo wa Serikali ameelekeza Chuo cha SUA kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na NIMR katika kuboresha huduma za Sekta ya Afya katika maeneo ya kubaini magonjwa, kuanza kutengeneza chanjo, kuimarisha tiba asili, kupanua tafiti za magonjwa, kutoa mchango katika kuboresha lishe za wananchi na kushirikisha sekta mbalimbali katika kuboresha huduma za afya nchini (One Health Approach).

Kwa upande wake Mkuu wa Mradi wa kutambua Kifua Kikuu kutumia Panya Buku Dr. Georgies Mgode amesema kuanzia mwaka 2007 mpaka Desemba 2020 mradi huo umeshapokea na kupima sampuli za makohozi 559,428 kutoka kwa wahisiwa wa kifua kikuu 315,476 huku wakiongeza utambuzi wa wagonjwa wa kifua kikuu kwa asilimia 40 katika maeneo ya mradi. Huduma hii ikisambaa maeneo mengi nchini basi Tanzania inaweza kuondokana na janga la ugonjwa huu kwani tayari Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma unatambulika duniani kuwa mfano katika mapambano dhidi ya kifua kikuu.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi kwa kuonesha nia ya Wizara ya Afya pamoja na SUA kuweza kushirikiana kuzalisha wataalamu na kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitaweza kusaidia sekta ya afya. Aidha Prof. Chibunda, ameahidi kuwa SUA itaendelea kutoa mchango wake katika tafiti mbalimbali za kuboresha huduma za afya nchini. Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha chuo hicho katika uboreshaji wa miundo mbinu, vifaa na mafunzo kwa watalaamu.

MWISHO

IMG-20210225-WA0038.jpg
IMG-20210225-WA0041.jpg
IMG-20210225-WA0043.jpg
IMG-20210225-WA0039.jpg
IMG-20210225-WA0036.jpg
IMG-20210225-WA0040.jpg
 
Kwani jamiiforum ndiyo imefika hapa.

Hii habari kwani ni mpya Jambo hilo Ni lamiaka mingi mikajua kwa Sasa panya wamefikia kupima Corona labda
 
Kwani jamiiforum ndiyo imefika hapa.

Hii habari kwani ni mpya Jambo hilo Ni lamiaka mingi mikajua kwa Sasa panya wamefikia kupima Corona labda
Sasa ndugu yangu, hapa ni kwa vipi hili ni kosa la JamiiForums wakati walioanzisha huu uzi "kwa kuchelewa" ni Wizara ya Afya wenyewe? Huoni hiyo ni verified account?
 
Napata faraja sana kuona wataalam wetu wa ndani wakifanya mambo makubwa kama haya,,Twaweza✊✊
 
Mwambieni waziri wenu aache drama.apige kazi kimyakimya tutamuona tu
 
tunawapongeza kwa uvumbuzi huu.Ila bado Kuna Mambo bado hamjafika hata 60% kwenye uvumbuzi mfano,A.I , artificial insemination,naona mmejikita Sana kwa ng'ombe tu ,tungependa kama mnge wekeza tafiti za A.I hata kwa mifugo mingine Kama nguruwe,mbuzi,kondoo,punda n.k.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom