Wizara: 'Dk' Mwaka jeuri

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
2,000
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa ufafanuzi kuhusu vituo vilivyofungiwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kusisitiza kwamba vimekiuka masharti ya utoaji huduma.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Nsachris Mwamwaja aliyasema hayo Dar es Salaam baada ya maswali mengi ambayo Wizara imekuwa ikiulizwa kutokana na uamuzi huo.

“Tunatoa shukrani kwa mchango wa Tiba Asili katika kuhudumia wananchi wenye matatizo ya kiafya. Wizara inapenda kufafanua kwamba Kamati ya Maadili ilikutatana na baadhi ya Matabibu mnamo Juni 17 na 22, 2016 kuhusu ukiukwaji unaofanywa katika utoaji wa huduma,” alisema.

Alisema kamati ilikaa na kujadili kwa kina ripoti ya matabibu waliotuhumiwa na kutoa maazimio mbalimbali ambapo Tabibu Juma Mwaka alionekana ni mkosefu wa mara kwa mara kwani Aprili 2, 2016 aliitwa na Baraza lakini yeye hakufika na badala yake alimtuma mwakilishi wake.

Alisema mwakilishi huyo hakuwa na taaluma ya Tiba Mbadala na hakuwa na utambulisho wowote, hivyo kuonesha alipuuzia wito wa baraza na kukiuka Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala sura 244 Kifungu cha 48(b).

Mwamwaja alisema Aprili 9, 2014 Tabibu Mwaka aliitwa na baraza kwa mahojiano na alipewa onyo kwa mdomo kutokana na matangazo yaliyokuwa yanaendelea kutangazwa kwenye vyombo vya habari bila idhini ya Baraza.

Alisema Mei 28, 2014 alipewa kibali cha kurusha matangazo mawili na Baraza yaliyohusu magonjwa ya ‘Fibroid’ na ‘kidney’ lakini alirusha vipindi vingine zaidi kinyume na utaratibu wa kifungu cha 10 cha Tangazo la Serikali Namba 409 ya mwaka 2008.

Alisema kifungu hicho kinaeleza kwamba tangazo lolote ambalo litatolewa kwa umma lazima liwe limeidhinishwa na Baraza na Baraza linatoa idhini baada ya kuipitia matangazo kwa kina ili umma upate ujumbe sahihi.

Alisema Septemba 19, 2014 Tabibu Mwaka alipewa barua yenye onyo kali iliyomtaka kusitisha matangazo kwenye vyombo vya habari, lakini aliendelea kutoa matangazo hata baada ya Tamko la Serikali lililotolewa na Mwenyekiti wa Baraza kuonyesha kwamba Tabibu Mwaka amezoea kufanya makosa.

“Ripoti inaeleza Tabibu Mwaka alitamka mbele ya Kamati kwamba hakuna madaraka ya kumzuia kwa kuwa yeye ni maarufu, hivyo amekuwa jeuri kuendelea kujitangaza,” alisema.

Alisema kwa upande wa tabibu John Lupimo, ripoti yake inaonesha kuwa ana tabia ya kurudia kufanya makosa anayoonywa na Baraza na kukaidi.

“Matangazo yaliyorushwa na Redio Ebon saa 3.15 usiku pia alitoa matangazo katika kipindi cha Chereko Chereko TBC akielezea uzazi, shinikizo la damu pamoja na tatizo la choo kigumu kinyume na matakwa ya Sheria lakini yeye ameendelea kutoa hayo matangazo bila kupata idhini ya Baraza,” alisema.

Kwa upande wa Tabibu, Abdala Mandai yeye amekuwa akirusha matangazo katika vyombo vya habari, na anapokuwa anajitangaza kuwa yeye ni Tabibu wa Tiba Asili na anakuwa anakiuka Tangazo la Serikali Namba 410 la mwaka 2008 kifungu cha 15 ambacho kinamkataza mtu kufanya matangazo, hali inayoonyesha yeye pia ni mzoefu wa kutofuata sheria.

Aidha alisema Septemba 23, 2014 Tabibu Mandai alipewa barua na baraza kusitisha matangazo mara moja lakini aliendelea kutangaza.

Alisema kwa upande wa Castor Ndulu na Esbon Baroshigwa wote wana makosa ya utoaji elimu ya Tiba Mbadala na Tiba Asili kinyume na Tamko la Waziri la Januari 16, 2016.

“Hawa walisikika Redio Abood, Planet FM na TBC FM kinyume na sheria. Hawa walionywa na kukiri makosa yao hivyo kuonekana sio wavunjivu wa sheria hivyo walipewa adhabu ndogo” alisema.

Alisema “ikumbukwe kwamba Wizara ndiyo yenye dhamana ya afya za Watanzania hivyo kwa kupitia vyombo vyake haiwezi kukaa kimya na kuona wananchi wanaumia”.

Hata hivyo alivitaka vyombo vya habari vinavyohusika kurusha matangazo hayo yaliyokatazwa kuacha mara moja kwani ni uvunjaji wa sheria na hatua kali zitachukuliwa. “Tunaomba wamiliki wa vyombo vya habari husika wafuate maagizo ya serikali kwa sababu wateja wao wamekatazwa lakini bado wanazidi kuvunja sheria. Tunajua watu hawa ni wenzetu lakini wafuate taratibu na sheria,” alisema.

Chanzo: Habari Leo
 

Mwana

JF-Expert Member
Aug 6, 2010
5,392
2,000
Sheria zipo na zifuatwe. Mtu maarufu hayuko juu ya sharia hata kidogo!
 

kajima

JF-Expert Member
Dec 5, 2009
1,289
2,000
I hope kafungiwa kwa misingi ya ukweli na sio personal vendetta.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom