Why Magufuli administration misses the point on Government splurge

Status
Not open for further replies.
*MIAKA 40 YA KIFO CHA MH. HUSSEIN SHEKILANGO-: MTANZANIA SHUPAVU _ALIYEPEWA_ BARABARA SINZA!!!*


By _MZEE WA ATIKALI_


1. *Usuli*

Wiki hii, nchi yetu imetimiza miaka 40 toka marehemu Mh. HUSSEIN RAMADHANI SHEKILANGO afariki dunia kwenye ajali mbaya ya ndege mkoani Arusha ambako, yeye na wenzake, walikuwawakienda kukutana na Mwalimu JK NYERERE kikazi. Kwavile kuna _Bongolanders_ wengi hasa _Dot.com generation_ ambao hawamfahamu, na kwavile wengi hawajui kuwa barabara ya _Sinza kwa Wajanja_ ilipewa jina SHEKILANGO kutokana na Mtanzania huyu shupavu, nikiwa kama _MZEE_ wa _ATIKALI_ leo nimewiwa kuandika _ATIKALI_ hii mahsusi kabisa kwaajili ya Mtanzania huyu aliyeaminiwa sana na Baba wa Taifa na kupewa jukumu zito nchini Uganda baada ya vita ya Kagera.

2. *Mh. SHEKILANGO Alikuwa ni nani?*

Mh. HUSSEIN RAMADHANI SHEKILANGO alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na mbunge wa Korogwe (1975-1980). Kabla ya hapo, Mh. SHEKILANGO alikuwa Meneja Mkuu wa "The National Milling Cooperation".

3. *Mh. SHEKILANGO Apewa Kazi Maalum na Mwalimu*

Wahenga watakumbuka kwamba mwishoni mwa miaka ya 1970, TZ iliingia vitali na Uganda maarufu _Vita ya Kagera_. Vita hiyo ilirindima toka Jumatatu ya tarehe 9.10.1978 hadi Jumapili ya tarehe 3.6.1979, siku ambayo wanajeshi wazalendo wa TZ walipofanikiwa kumsambaratisha Nduli IDD AMIN DADA aliyelazimika kubwaga manyanga na kutoroka akikubali kuwa TZ ni moto wa kuotea mbali!.

Baada ya kumalizika kwa vita hiyo, kilipita kipindi cha mpito cha utawala wa Mh. YUSUPH KIRONDWA LULE na Mh. GODFREY LUKONGWA BINAISA kilichokuwa na sintofahamu na machafuko mengi.

Hivyo, Baba wa Taifa alimpa Mh. SHEKILANGO jukumu Maalum la kuwa Mratibu kati ya serikali ya TZ na Uganda. Hili lilikuwa ni jukumu kubwa sana na pia ilikuwa ni heshma kubwa sana kwake Mh. SHEKILANGO binafsi. Mh. SHEKILANGO alilitekeleza jukumu hili kuanzia Juni 1979, kwa usaidizi wa Mh. FARAJI A. KILUMANGA aliyekuwa Balozi wetu nchini Uganda. Lengo Kuu lilikuwa kuisaidia serikali ya Uganda isimame. Mh. SHEKILANGO alilitekeleza jukumu hili kwa weledi wa hali ya juu, usiku na mchana bila kuchoka.

4. *Mh. SHEKILANGO NA MWALIMU WAPANGA KUKUTANA ARUSHA*

Mh. SHEKILANGO alipanga miadi ya kukutana na Mwalimu NYERERE jijini Arusha aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi jijini humo. Lengo Kuu la Mh. SHEKILANGO kupanga miadi hiyo lilikuwa ni kumuhabarisha MWALIMU juu ya hali ya Usalama ya Uganda baada ya mfarakano mkubwa kati ya Rais BINAISA na Jenerali DAVID OYITE OJOK aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi. Mfarakano huu ulikuwa imeonesha dalili zote za kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hivyo, viongozi hao, MWALIMU na Mh. SHEKILANGO, walikubaliana kukutana asubuhi ya siku ya Jumapili, tarehe 11.5.1980.

5. *Mh. SHEKILANGO AKWEA _PIPA_ KWENDA _GENEVA YA AFRIKA_*

Asubuhi na mapema siku hiyo ya Jumapili ya tarehe 11.5.1980, Mh. SHEKILANGO aliongoza msafara wa maofisa wa serikali ya TZ uliokuwa ukitoka Uganda kuelekea Arusha _"Geneva ya Afrika"_ kwa ndege ndogo aina ya _Casena_ 402 yenye uwezo wa kuchukua abiria 8 tu.

5.1 *Ndege ilibeba Abiria 7*

Ndege hiyo ilibeba abiria 7 ambao walikuwa ni:

1. Mh. Waziri HUSSEIN SHEKILANGO
2. Mh. Balozi FARAJ KILUMANGA
3. Mwanadiplomasia IDD MSECHU
4. Luteni LUOGA
5. Luteni MALLYA
6. Cpl PETRO MAGUNDA
7. Pte STEVE MTAWA

6. *MWALIMU Amsubiri Mh. SHEKILANGO Kwa Hamu*

Siku hiyo ya Jumapili, Mwalimu alikwenda kanisani asubuhi na mapema. Baada ya kurudi na kupata staftahi, Mwalimu akawa anamsubiri Mh. SHEKILANGO kwa hamu ili amuhabarishe kuhusu hali tete iliyokuwa imejiri huko Uganda. Muda wa miadi ulipita sana, hali iliyomshangaza MWALIMU lakini hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuvuta subira.

Hata hivyo, Mwalimu alipoona amesubiri hadi saa 9 alasiri bila kumuona wala kupata taarifa zozote za Mh. SHEKILANGO, ikabidi aende kupata maakuli na kisha akapumzika.

7. *ASKARI WA MONDULI WAANZA MSAKO WA NDEGE*

Baada ya kuona ndege hiyo iliyokuwa ikitarajiwa kuwasili majira ya saa 5 na kwa vile mawasiliano ya anga yalikuwa yameonesha ndege hiyo tayari ilikuwa ndani ya anga za Arusha maeneo ya Monduli, askari wa Chuo cha kijeshi Monduli walianza msako mkali wa kuitafuta ndege hiyo milimani ambako kulikuwa na ukungu mwingi na hivyo kupelekea kazi hiyo kuwa ngumu sana.

Askari hao, hatimaye jioni, walifanikuwa kukutana na vijana Wawili wa kimasai, Bw. MUNDEREI ANGERUKAI na Bw. NUSERIEKI NJONJOLOI, ambao walikuwa wameshuhudia _live_ jinsi ajali ya ndege hiyo ilivyotokea asubuhi ya siku hiyo. Vijana hao waliwapeleka askari hao eneo la tukio ambapo waliona mabaki ya ndege na miili iliyokuwa imeharibika vibaya na kuichukua miili hiyo.

8. *MWALIMU AHUZUNIKA BAADA YA KUJULISHWA NDEGE IMEPATA AJALI, ABIRIA WOTE WAMEFARIKI!*

MWALIMU hakuamini maskio yake pale alipoamshwa na kuhabarishwa na wasaidizi wake kwamba ndege iliyokuwa imembeba Mh. SHEKILANGO ilikuwa imepata ajali ikiwa tayari imeingia anga za Arusha na kwamba abiria wote, akiwemo Mh. SHEKILANGO, wamefariki. MWALIMU alihuzunika mno!.

8. *JINSI AJALI YA NDEGE HIYO ILIVYOTOKEA*

8.1 *Ajali ilitokea Kijiji cha Engwik*

Ndege hiyo ndogo ya JWTZ iliyokuwa ikiruka usawa wa mita kati ya 5,000 na 7,000 toka usawa wa bahari, ilipata ajali kijiji cha Engwik kilichopo wilaya ya Monduli muda wa saa 5 asubuhi.

8.2 *Ndege hiyo Ililipuka baada ya kugonga Kilima*

Ndege hiyo ililipuka baada ya kugonga kilima cha Kolomoniki kutokana na ukungu mwingi uliokuwepo eneo hilo asubuhi hiyo. Ukungu huo uliokuwa umetamalaki ndio uliosababisha Rubani wa ndege hiyo ashindwe kabisa kukiona kilima hicho.

9. *Mh. SHEKILANGO AZIKWA NA MAELFU KOROGWE*

MWALIMU alilitaarifu Taifa kuhusu msiba huo mkubwa. Kwa hakika, ilikuwa ni huzuni kubwa. Mh. SHEKILANGO akazikwa kwao Jitengeni, Mombo, Korogwe ambapo maelfu ya wananchi toka maeneo yote ya mkoa wa Tanga walishiriki mazishi hayo yaliyoweka rekodi ya kipekee mkoani humo.

Kwa kumuenzi Mh. SHEKILANGO, shule moja wilayani Korogwe ikapewa jina lake.

10. *FAMILIA YA Mh. SHEKILANGO NA MCHANGO MKUBWA KIELIMU WA MKEWE*

Mh. SHEKILANGO alikuwa na wajihi wa urefu na wanawe walikuwawakijitofautisha kirahisi kutokana na urefu wao usio wa kawaida. Wakati wa uhai wake, Mh. SHEKILANGO alikuwa akiishi _Sea View_ . Familia hiyo baadaye ilihamia kwenye nyumba yao iliyopo Kinondoni Bwawani, kiwanja Na. 401 Kitalu 42.

Mama ZAPPORA SHEKILANGO, mke wa Mh. SHEKILANGO alikuwa ni mwanamke wa shoka kwani alikuwa ni mmoja wa wanawake waliotoa mchango mkubwa sana katika Taifa hili akiwaamefundisha wanafunzi lukuki. Mama huyu ni mmoja wa wanawake wa mwanzo kuwa ma-"headmistress" kwenye shule nyingi nchini. Alikuwa "Headmistress" Zanaki, Kisutu, Jangwani, Forodhani, Msalato na Iringa Girls. Mama huyu alifariki tarehe 1.9.2018.


11. *BARABARA YA _"SINZA KWA WAJANJA"_ YAPEWA JINA LA MH. SHEKILANGO*

Wahenga watakumbuka kuwa miaka ya 1980s, Sinza ilikuwa ni mashamba ya mpunga yaliyokuwa yamenawiri sana kwani kina cha maji kiko karibu na kulikuwa na nyumba na ofisi chache tu. Wakati huo, barabara ya lami toka Bamaga hadi Morogoro road ndio ilikuwaikijengwa. Uongozi wa Jiji la Dsm ukaamua kumuenzi Mh. SHEKILANGO kwa kuipa jina lake barabara hiyo maarufu ambayo kwasasa inafanyiwa ukarabati mkubwa.

12. *TAMATI:*

_ATIKALI_ hii, ni imani yangu, imeweza kukujuza kuhusu Mtanzania huyu shupavu marehemu HUSSEIN RAMADHANI SHEKILANGO. Viongozi wengi hapa nchini hufanya mambo makubwa na kwa Uzalendo wa hali ya juu na wakati mwingine katika mazingira hatarishi lakini historia zao zinakuwa hazijulikani kwa Taifa.

Nikiwa kama _MZEE WA ATIKALI_ nimekuwa nikipigiwa simu nyingi na ndugu wa familia hizi zikielezea kururahishwa na _ATIKALI_ zielezeazo historia za wapendwa wao ambazo mara nyingi _Bongolanders_ wengi hawazifahamu. Aidha, nafurahishwa sana, sana nipatapo _feedback/constructive criticism_ kuhusu _ATIKALI_ hizi kwa lengo la kuzifanya kuwa bora zaidi.


By _MZEE WA ATIKALI_


Mei 2020.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom