Wenye kinga ni Rais, Makamu, Waziri Mkuu, mawaziri

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,047
Nagu, Mwanyika wasema hakuna aliye juu ya sheria
*Wenye kinga ni Rais, Makamu, Waziri Mkuu, mawaziri

Na John Daniel, Dodoma
Majira

SERIKALI imesema hakuna aliye juu ya Sheria na kwamba hata Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Bw. Edward Hosea, anaweza kuchunguzwa na Polisi kuhusu tuhuma za rushwa.

Hata hivyo imesisitiza kuwa suala hilo linapaswa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu na uangalifu mkubwa, kwa kuwa watu wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa wanaweza kumpaka matope kiongozi huyo wa TAKUKURU kwa kuwa ameonekana kuwa mwiba kwao.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Sheria na Katiba Dkt. Mary Nagu, wakati akizungumza na Majira nje ya ukumbi wa Bunge kuhusu tuhuma zilitolewa kupitia mtandao wa intaneti kuwa Bw. Hosea anakabiliwa na tuhuma za rushwa.

"Mimi ninachojua ni kwamba hakuna aliye juu ya sheria, mtu yeyote akifanya kosa anaweza kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua kisheria, mimi sijui kama kuna tuhuma zozote kuhusu Mkurugenzi wa TAKUKURU, lakini hata kama yapo, suala hilo linapaswa kuchukuliwa kwa umakini na kwa uangalifu sana.

"Mtu anaweza kuona huyu anafanya kazi vizuri, akaamua kuweka uwongo wake ili kutuharibia tusishinde vita ya rushwa, kwanza kama ni kweli kwa nini wasipeleke barua au malalamiko panapohusika? Intaneti imekuwa ofisi ya kupeka barua? Hili suala ni zito na linapaswa hata ninyi waandishi kuwa makini sana," alionya Dkt. Nagu.

Alipoulizwa kama Mkurugenzi huyo ana kinga kikatiba alisema "Kikatiba hajatajwa, waliopo ni Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na mawaziri, ila mahitaji ya yeye kutajwa moja kwa moja yalijitokeza ili kuweka ulinzi fulani, lakini bado halijawekwa," alisema Dkt. Nagu

Alisema kwa kuwa Katiba ni sheria mama na imeandikwa kijumlajumla, ataendelea kuangalia kama kuna kifungu kinachomzungumza moja kwa moja.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika, alisema yeye kama anavyojua, sheria hakuna mtu ambaye hawezi kuchunguzwa kwa kosa lolote na kusisitiza kuwa polisi wanaweza kumchunguza Bw. Hosea, iwapo kuna ulazima wa kufanya hivyo.

"Kwanza mimi sijui kama kuna tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU lakini ninachojua, hakuna aliye juu ya sheria, wote sisi ni raia wa Tanzania, polisi wana uwezo wa kumchunguza Mkurugenzi wa TAKUKURU," alisema Bw. Mwanyika.

Alipoulizwa sheria inasema nini kwa kiongozi kama huyo anapochunguzwa kama anaweza kuendelea kufanya kazi au kupumzika mpaka uchunguzi ukamilike, alisema suala hilo ni la Waziri katika Ofisi ya Rais Utawala Bora, Bw. Philip Marmo.

"Kama nilivyokwambia, sijui kama unayemzungumza ana tuhuma zozote, pia swali hilo muulize Bw. Marmo ndiye anaweza kukujibu vizuri," alisema Bw. Mwanyika.

Alipoulizwa kuhusu kanuni za maadili ya uongozi kwa ujumla kwa mujibu wa sheria, alisema Bw. Marmo anaweza kujibu hilo vizuri zaidi kwa kuwa yeye anawajibika kwa masuala yote ya Utawala Bora.

Naye Grace Michael alisema wanasheria mbalimbali Dar es Salaam nao walisema Mkurugenzi wa TAKUKURU anaweza akachunguzwa tuhuma zozote zinazohusiana na rushwa na vyombo mbalimbali vya Dola kama Idara ya Usalama wa Taifa au kuundiwa Tume.

Wakizungumza jana na Majira kwa njia ya simu kwa masharti ya kutotajwa majina, wanasheria hao walisema hakuna mtu aliye juu ya sheria, hivyo kama ana tuhuma anaweza akachunguzwa na vyombo vingine na tuhuma zake zikabainika.

Aidha, walisema hata watendaji wake wanaweza wakamchunguza endapo atakuwa amejiuzulu ili waweze kutoa taarifa yenye ukweli, kwani kuchunguzwa akiwa bado kazini ni lazima kutakuwa na mgongano wa maslahi na hawataweza kutoa taarifa sahihi.

"Kuna vyombo kama Usalama wa Taifa ambao wanaweza wakamchunguza, lakini pia maofisa wengine wa taasisi hiyo nao wanaweza wakamchunguza endapo atakuwa amejiuzlu ili kufanikisha uchunguzi huo na kuepuka mgongano wa maslahi," alisema mmoja wa wanasheria hao

Aidha, walisema kutokana na yeye kuwa ni wa kuteuliwa inatakiwa aliyemteua kushika nafasi hiyo aunde Tume ichunguze madai yake na Tume hiyo inaweza ikaundwa kwa kuwekwa watu mbalimbali wakiwamo majaji, wapelelezi, Usalama wa Taifa ili waweze kukusanya taarifa na kisha kutoa ripoti ya tuhuma anazokabiliwa nazo.

Kauli za wanasheria hao zimekuja kama ufafanuzi kuhusiana na kauli nyingine aliyoitoa hivi karibuni Waziri Marmo kuhusiana na tuhuma ambazo zimekuwa zikisambazwa kwenye mtandao wa kompyuta dhidi ya Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bw. Hosea.

Akizungumza na gazeti moja kwa simu akiwa nje ya nchi, Bw. Marmo alisema Serikali inachunguza tuhuma hizo ili kuona ukweli na uhalali wake, huku aliyetuhumiwa akikanusha madai yaliyotolewa katika mtandao.
 
sasa hii sentensi ya kwanza tuu siielewi....hakuna aliye juu ya sheria ila wenye kinga ni raisi,makamu na waziri mkuu wat daz that sent.mean
 
Back
Top Bottom