Wema hauozi jamani

Aggrey86

JF-Expert Member
Jun 26, 2011
853
155
Habari ya mapuziko wakuu ni baada ya mchaka mchaka wa wiki nzima katika ujenzi wa Taifa letu basi si mbaya wakati huu wa mapumziko ya wiki tukakumbushana baadhi ya mambo na kuwekana katika dira nzuri, hi ni story kuna rafiki yangu alishawahi kunisimulia si mbaya na wengine tukaisoma na kutukumbusha baadhi ya mambo katika maisha yetu ya kila siku.

Wapendwataarifa hii naileta kwenu kama nilivyoipokea toka kwa ndugu yangu. Mimi binafsi fundisho nililopata ni usemi wa ile methali isemayo "WEMA HAUOZI"

"Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi.

Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kama siku hizi.

Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili.

Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.

Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni
bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli alisema kwa kudhamiria hasa.

Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha polisi ili nishughulikiwe..

Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana.

Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama huko polisi ningeaminika.

Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake
ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko. Nilimshukuru na
kuondoka kukimbilia basi. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu.

Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe.
Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.

Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili.

Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa
sio sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. alikuwa ameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi
yalinitoka.

Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale tulipanda basi kuendelea na safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili.

Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.

Nillishindwa kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu na pengine maswali ya kijinga pia. Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati
ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa. Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule aliniamini nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu.

Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na namna ujuavyo wewe.

Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo hiyo. Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule kuwa mbaya kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda nchini Uingereza. Mwaka 1991 nilianza shughuli zangu.

Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco ambalo liliungua mwaka 1996, ambapo lilijengwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa Water Front. Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa na sekratari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya yake ikiwa
hairidhishi sana.

Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye huruma sana na nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza,
"nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao baada ya muda mfupi". Nilisema na sikuwa na kikao chochote, lakini nilitaka tu aondoke haraka.

"Samahani mzee, nilikuwa na shida...nimefukuzwa shule na sina tena mtu wakunisaidia kwa sababu ...nime..niko ..kidato cha pili na hivyo tu natafuta tu kama atatokea mtu...Nilimkatisha. "Sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie..Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe ...Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezo, wanataka sifa?"

"Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa hata kazi hafanyi..," Alianza kulia. Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi, kwa nini nisiwe mwema, angalau kwa mara moja tu. "Baba na mama walifariki lini?" Niliuliza nikijua kwamba, watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo kila anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi.

"Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndio shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa." Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji
unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.

Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana. "Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?" Yule kijana alisema, "Nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, na ndio nimejikuta nikiingia hapa, sijui....sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa."
Alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso.

Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona kama vile nimebanwa na kushindwa kupumua. "Baba yako alikuwa anaitwa nani?" "Alikuwa anaitwa Siame..Cosmas Siame.." Niliinuka ghaflahadi
yule kijana alishtuka . Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti ndani ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi.

"Ndio alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika." Nilinong'ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali. "Mungu, wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba
kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani." Halafu nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.

Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilihisi kuwa mtu mwingine kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. "Mimi ni baba yako mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu
yangu sasa kukulea hadi mwisho" Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita.

Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo dada yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki hata hivyo mwaka mmoja baadae, lakini akiwa ameridhika sana.

Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi sasa yuko nchini Australia anakofanya kazi. Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile
walichokipanda miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado. Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine
zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu. NGUVU HIZO NI UPENDO WA MU

Asanteni nawatakieni mapumziko mema huku tukitafakari jinsi ya kutendeana mema sisi kama watanzania kwa manufaa ya maisha yetu sote.
 
Dah! nimesoma hii stori inasisimua sana. Kweli wema ni akiba kubwa sana ktk maisha ya binadam.
 
Wapendwa, hiyo yaitwa " Power of Kindness " Duniani kuna mengi nahiyo ni moja tu !!

Shukraani zangu nyingi mh. Aggrey86
 
Ongera sn but naona umeingilia kaz za watu.Hiyo story ungemsimulia shigongo kingekuja kitab chenye kurasa zaid ya 800.mngekuwa mnapiga pesa tu
 
Kweli una roho mbaya sana wewe!

Yaani humsaidii mtu hadi akusimulie historia yake yoooote!kwani hata maelezo yako yanadhihirisha ukatili wako,eti zungumza haraka,nina kikao! Huna ubinadamu kabisa wee mzee
 
kweli una roho mbaya sana wewe.!
yaani humsaidii mtu hadi akusimulie historia yake yoooote!kwani hata maelezo yako yanadhihirisha ukatili wako,eti zungumza haraka,nina kikao!Huna ubinadamu kabisa wee mzee
Hakika!
 
Nimemkumbuka marehemu Munga Tehenan..ndio vilikua visa vyake hivi hata hiki aliwahi kutoa kwenye gazeti la jitambue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom