We Ludenga! Mrembo wa Kidigo Kwa sifa za Kizungu? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

We Ludenga! Mrembo wa Kidigo Kwa sifa za Kizungu?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mgoyangi, Aug 20, 2009.

 1. Mgoyangi

  Mgoyangi Senior Member

  #1
  Aug 20, 2009
  Joined: Feb 6, 2008
  Messages: 184
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Inabidi Ludenga japo asome hii na kisha ajue kuwa kuwaparade Mabinti zetu na watu kuingia kwa pesa kuwatazama wakiwa nusu uchi ni udhalilishaji kwa upande wetu, ingawa kwake ni kuganga njaa. lakini wakulu wengine wanaona raha kweli kushuhudia mapaja. :rolleyes:

  Joseph Mihangwa
  Agosti 19, 2009

  "Mke mwema, ni nani awezaye kumwona?
  Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake,
  Anaucheka wakati ujao.

  Hufumba kinywa chake kwa hekima,
  Na sheria ya wema i katika ulimi wake.

  Huangalia sana njia [utamaduni] za watu wa nyumbani mwake
  Wala hali chakula cha uvivu.

  … mumewe humsifu, na kusema
  Binti za watu wengi wamefanya mema,
  Lakini wewe umewapita wote
  Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili" [Mithali 10 – 30]

  Nao wakapita jukwaani mbele ya kadamnasi, kwa vitimbwi, madaha na maringo ya ulimbwende, wakijitangaza kulisaka taji la urembo, apatikane mmoja kuwapita wengine wote. Kumi idadi yao, waliochujwa kutoka idadi ya makumi, na wengine kupigwa buti, na kuachwa majeruhi. Hawa ndio kumi bora, katika kinyang’anyiro cha kumsaka mrembo, mlimbwende.

  Nguo zao fupi na nyepesi, kutoa maungo nje, kutukumbusha laghai ya Hawa, kwa Adamu kula tunda la kifo; Ngozi yao “suriama”, iliyopikwa kwa vipodozi vya kemikali; kucha zao ndefu, na mizigo ya nywele kichwani isiyowakilisha wajihi wa mbebaji, kutukumbusha sura ya Jini katika hadithi za “Alfu Lela Ulela” niliyoisoma utotoni.

  Kope na nyusi za macho yao zilipambwa kwa wanja uliokolea; midomo yao myekundu kwa rangi mithili ya “Subiani” mlamba damu; kwa maumbile, wote walikuwa wembamba mfano wa ajuza mchawi, Gagula, katika hadithi ya Machimbo ya Mfalme Sulemani.

  Wakatokomea upande wa pili wa jukwaa, nao ukumbi mzima ukashangilia, kwa vifijo na hoi hoi, kukiri “urembo” wa vidosho hao. Nao waamuzi wa shindano wakanoa kalamu zao, wakainama kurekodi alama kwa kila mshiriki wa hatua hiyo. Ni weusi tii, lakini nahau na hulka yao iliwakilisha radha ya kigeni, kwa lugha na vitendo.

  Kisha mabinti hao wakarejea tena jukwaani, safari hii mmoja mmoja, kwa zamu; kila tokeo, vazi tofauti, na kwa mwendo bandia wa maringo, hatua za hesabu, ili kukamata macho ya watazamaji kukonga roho zao.

  Yakafuatia mahojiano, kupima uwezo wa washiriki wa kufikiri, yaani IQ. Na ingawa wote walikuwa Waswahili, lakini yaliendeshwa kwa lugha ya Kiingereza kuonyesha “Ukuu” wa lugha za kigeni dhidi ya Kiswahili, na dhidi ya utamaduni wa wahojiwa.

  Hayo yalikuwa mashindano ya kumtafuta Mrembo kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Mrembo wa Dunia.

  Tanzania imeingia kwa nguvu zote katika ulimwengu wa mashindano haya kiasi kwamba sasa ni tukio la kila mwaka. Mwanzoni, tulifikiri mashindano hayo yanalenga kukuza utamaduni wa Mtanzania na wa Mwafrika, lakini katika utekelezaji wake, kinyume chake ndio ukweli wenyewe kiasi kwamba kwa Mtanzania urembo sasa ni bidhaa ya inayoweza kuuzwa katika soko la kimataifa.

  Kama hivyo ndivyo, basi, urembo kama bidhaa nyingine yoyote inayowania soko la nje, itapimwa tu kwa vigezo vya kimataifa ili iweze kukubalika. Inapokuwa hivyo, urembo unakoma kuwa suala la utamaduni. Pengine ni kwa sababu hii kwamba Wizara ya Biashara ndiyo lilikuwa lengo la Waasisi wa mashindano haya yaliyoanza mwaka 1951, nao ni Bwana Eric Morley [alifariki 2001] na mkewe Julia, ambao huchukua asilimia 52 ya mapato kutokana na mashindano hayo; Eric hupata asilimia 26.68 na Julia asilimia 25 ya mapato yote.

  Kumekuwapo mitazamo na tafsiri tofauti katika jamii za Kiafrika, ikiwamo Tanzania, kuhusu mashindano haya. Wapo wanaoyaona kwamba yanalenga kumdhalilisha mwanamke. Wanayafananisha na biashara ya mwili inayomwanika mwanamke pa wazi kama ng’ombe mnadani.

  Kambi hii inadiriki kuhoji: “ kuna tofauti gani kati ya mashindano haya na biashara ya utalii, ambapo wanyama wa mbuga kama Serengeti hujianika kwa kila mtalii kushibisha jicho lake na kuondoka?”.

  Wapo pia wanaoona kwamba, licha ya mashindano haya kumdhalilisha mwanamke, yanatumika pia kukuza soko la bidhaa za mataifa yenye viwanda – bidhaa kama vile vipodozi na aina ya mavazi inayobuniwa na wanamitindo wa nje. Yanakuza pia utamaduni wa kigeni kwa kuwa washindani hupimwa kwa vigezo vya nchi za Magharibi.

  Kwa maana nyingine ni kwamba, mwanamke sasa anatumika kama kikorombwezo katika kukuza na kuimarisha utamaduni wa kibepari wa nchi za Magharibi. Kuna ukweli gani katika tuhuma hizi?

  Inadaiwa kwamba kwa karne nyingi, mwanamke amenyanyasika katika mfumo dume wa jamii kiasi kwamba sasa anataka kujikomboa. Kwa hiyo hizi ni enzi za ukombozi wa mwanamke, ni enzi za kupigania haki zake alizopokonywa.

  Katika kutekeleza azma hii, hapa kwetu, licha ya kuanzisha taasisi mbali mbali za kuwainua akina mama, tumeunda pia Wizara inayoshughulikia haki za Wanawake na Watoto. Mwanzoni, Wizara hii iliitwa “Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto”, ikiongozwa na Waziri na Katibu Mkuu mwanamke kuonyesha jinsi mwanamke alivyopania “kujikomboa”.

  Ghafla na bila ya kutarajiwa Wizara hii ilibadili jina na kuitwa “Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto”, pengine kwa lengo la kufuta ile dhana kwamba mwanamke ni mnyonge kiasi cha kuwekwa kundi moja na watoto. Tunapoondoa neno “Wanawake”, na kuweka neno “Jinsia” badala yake, tunazungumzia jinsia gani? Je, inamaanisha matatizo kwa jinsia zote? Kuna nini zaidi kwa jinsia hizi kwa pamoja hata kuundiwa Wizara maalumu?

  Wanafalsafa wa kale na wa nyakati za ubepari wanasema nini kuhusu hadhi ya mwanamke katika jamii?.

  Plato, mwanafalsafa aliyeishi kati ya mwaka 428 – 348 kabla ya Kristo [KK], aliwahi kuandika hivi: “Watu waoga, na wale wenye maisha mabaya na hohe hahe, bila shaka watakapokufa na kuzaliwa kwa mara ya pili, watageuzwa wanawake. Kwa mtu kuzaliwa mwanamke ni balaa kubwa inayopitwa na kifo pekee”.

  Mwanafalsafa mwingine, Homer, akimfananisha mwanamke na shetani aliandika: “Hakuna roho iliyo mbaya na ya kishetani kama ya mwanamke, [daima] moyo wake hukimbilia kutamani maovu”.

  Naye Mtakatifu Thomas wa Akwino [384 – 324 KK] aliandika: “Mwanamke hakustahili kuumbwa na kuishi, yeye ni ajali iliyotokea kutokana na Mungu kumuumba Adam”.

  Mwanatheolojia mmoja mahiri, Arthur Schoppenhaner, aliyeishi kati ya mwaka 1788 – 1860 baada ya Kristo [BK], anamwelezea mwanamke kwa ukakamavu bila aibu kwa kusema, “Ukitazama tumbo la mwanamke, utaelewa sawia kwamba hafai kwa kazi yoyote ya maana, iwe ya kiroho [uinjilisti], kwa maumbile na mwili, mwanamke anafaa kwa kazi pekee ya kusafisha nyumba na kulea watoto, kwani yeye daima ni mpungukiwa mwenye fikra sawa na mtoto; kwa kifupi, mwanamke ni mtoto mkubwa maisha yake yote; ni kiumbe mwenye akili iliyo kati ya akili ya mtoto na akili ya mwanaume ambaye ndiye binadamu wa kweli”.

  Huko Uchina, kati ya karne ya 16 na 17, wasichana walilazimishwa kukariri kimoyomoyo mwongozo uliosema hivi: “Kasoro tano kubwa za mwanamke ni ujinga, kutoridhika, kashfa, uvivu na upumbavu; kati ya wanawake kumi, saba au wanane kati yao wana kasoro hizo tano, na hii ndiyo sababu wako chini ya mwanaume”.

  Kashfa kubwa kuliko zote hizi dhidi ya mwanamke enzi hizo ni ile ya Fredrick Nietzche [Mjerumani], aliyewahi kuandika: “Mwanaume alelewe kwa ajili ya vita [kazi ngumu], na mwanamke kwa ajili ya kumburudisha askari [na maonyesho ya urembo kwenye kumbi za starehe?], mengine yote ni upuuzi tu”.

  Mawazo ya kina Nietzche na wengineo dhidi ya hadhi ya mwanamke yanaendelea kudumu hadi leo katika jamii zetu zenye mfumo dume.

  Tukichukua taswira ya “Mwanamke mwema”, tunayoisoma katika kitabu cha Mithali, na ile ya Mashindano ya Urembo ya leo, ni nani mke mwema kati ya hao? Yu wapi mrembo wa dunia? Je, mashindano ya urembo, kama yalivyo, ni sehemu ya vita ya ukombozi wa mwanamke? Je, si kweli kwamba mashindano haya yamevuka mipaka ya “utu bora” na kugeuka tusi na dhihaka kwa hadhi na heshima ya mwanamke?.

  Ni kweli kwamba mashindano ya urembo yanaendeshwa kwa kuzingatia vigezo vya utamaduni wa Magharibi; kwa hiyo tunaweza kusema yanawakilisha ukoloni mamboleo kiutamaduni.

  Tanzania sasa inaongoza barani Afrika kwa mmomonyoko wa utamaduni na maadili ya Taifa kwa nyanja zote. Je, ni kweli kwamba kuna kitu kiitwacho “urembo” wa kimataifa? Yu wapi Mrembo wa Dunia? Anafananaje?.

  Tunadhani hakuna kitu kama hicho kwani urembo ni mtazamo na ridhio la mtu binafsi, jamii na taifa, kwa vigezo vya utamaduni wake. Kwa mfano, wakati kwa Mchina au Mjapani macho madogo yaliyobonyea yanaweza kuwa ndio urembo wenyewe; kwa Mswahili meno yenye mwanya au macho ya “gololi” vyaweza kuwa urembo usio kifani.

  Katika makabila mengine pambo la chale usoni au kutoga mdomo na masikio, ni urembo tosha kwa binti kupiganiwa na wachumba, ambapo kwa wengine mambo hayo ni ishara ya “ushamba”.

  Vivyo hivyo kwa mavazi, maremba na kujikwatua, mwendo wa maringo, ili mradi kila jamii na kila taifa lina vigezo vyake vya kufurahia, kupima na kujivunia “urembo” wake.

  Katika baadhi ya makabila hapo kale, msichana aliyechumbiwa alipelekwa kwenye nyumba maalumu ambako alilishwa chakula cha mafuta ili anenepe kabla ya kujitokeza hadharani siku ya harusi. Unene ulihesabiwa kama sehemu ya urembo na dalili ya afya njema. Leo, ni kinyume chake; wasichana wanatafuta uembamba kama sehemu ya urembo kwa misingi ya utamaduni wa Magharibi.

  Urembo au uzuri wa mwanamke haupimwi jukwaani kwa mbwembwe na maringo ya ulimbwende. Twendeni vijijini, huko tutamwona mwanamke mwema, mrembo mwenye kustahili kuwakilisha jamii ya Kitanzania na Afrika kimataifa bila ya upendeleo.

  Huyu ndiye mwanamke bora, mwenye nguvu, auchekaye wakati ujao. Hayumbishwi wala kupaparuka na anasa za utandawazi; hufumba kinywa chake kwa hekima, ni mlinzi wa utamaduni wetu; hali vya kudakia, anaishi kwa jasho lake.

  Uzuri wake ni wa asilia, hautafutwi kwa vipodozi vya kemikali. Njoo mvua njoo jua, upepo na baridi, uzuri wake upo pale pale, hauathiriki. Huyo ndiye mrembo wa mazingira yetu, ni mrembo wa kujivunia.

  Mrembo wetu si “Skitter Davis”, “Doreen Thatcher” au “Kutchi Hiroshima”; wala hatupashwi kufanana au kushindanishwa na hawa kwa sababu kila jamii ina vigezo vyake vya urembo. Kuiga “urembo” wa kigeni ni kupapalika na utamaduni wa kigeni usio na mwelekeo. Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mti usio na mizizi.

  Mfano wa mwanamke mwema na mrembo wa Afrika si Mama Maria wa Uyahudi au Fatimah Binti Muhamad wa Uarabuni, bali ni Isis, mama wa Kiafrika aliyezaa mtoto wa kiume, Horus, bila ya kukutana na mwanaume, kama ilivyokuwa imetabiriwa na Manabii wa Kiafrika miaka ya 300 KK. [Pia kuna Osiris aliyeuawa, akafufuka na kupaa mbinguni kusubiri siku ya kiyama].

  Mfano wa Mrembo wa Afrika si “Joan Johnson”, bali ni Gati Chacha, Kabula Mabula au “Malkia wa Sheba” aliyeitwa Makeda, kutoka Afrika, aliyeisumbua roho ya Mfalme Suleman [Solomon] wa Uyahudi kwa “urembo” wake, miaka ya 500 KK.

  Ni lini msichana wa Kimasai, kwa urembo wake na kwa vazi lake la asilia, atafikia kilele cha mashindano ya mrembo wa dunia? Ni wakati sasa tujichunguze; tukifahamu kwamba “Mrembo” wa dunia siyo kwamba ndiye mwanamke mrembo kuliko wanawake wote duniani.  Simu:
  0713-526972


  Barua-pepe:
  jmihangwa@yahoo.com
   
 2. longi mapexa

  longi mapexa JF-Expert Member

  #2
  May 5, 2016
  Joined: Jul 18, 2015
  Messages: 2,007
  Likes Received: 1,317
  Trophy Points: 280
  dah ukweli mtupu!...
   
 3. mitindo huru

  mitindo huru JF-Expert Member

  #3
  May 6, 2016
  Joined: Apr 26, 2016
  Messages: 983
  Likes Received: 734
  Trophy Points: 180
  Inabidi uitungie mashairi sasa, maana ilivyokaa..!
   
 4. r

  rubii JF-Expert Member

  #4
  May 6, 2016
  Joined: Feb 22, 2015
  Messages: 11,320
  Likes Received: 9,931
  Trophy Points: 280
  Kila jambo lina pande mbili.
  Ukitazama kila jambo kwa upande wa mabaya tu hutaendelea!
   
Loading...