Wazo la Leo: IGP Sirro Msipofanya Hili sasa kwa Tabasamu, Mtafanya Lile Baadaye kwa Machozi...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
M. M. Mwanakijiji
Kumeanza na kuwa na kawaida ya aina Fulani ambapo mtu anakuja kukamatwa na maafisa wa usalama halafu watu wanadai kuwa watu hao ni wale wa kundi la “wasiojulikana”. Baada ya muda kidogo vyombo rasmi vya usalama vinatoa taarifa kuwa mtu huyo kakamatwa na polisi. Wakati mwingine inatokea katika mazingira ambayo yanawafanya watu wadhanie kuwa mtu huyo “ametekwa na watu wasiojulikana” lakini baadaye inakuja kugundulika kuwa yuko mikononi mwa polisi.
Vyombo vya usalama pote duniani vinakamata watu na wakati mwingine kwa mtindo wa kushtukiza (raid). Uvamizi huo wa polisi (raid) ni jambo la kawaida lakini mara nyingi unafanywa kwa ajili ya mambo makubwa mawili – ambayo yako wazi. Kwanza, kuwashtukiza walengwa ili wasijiandae au kupata taarifa na hivyo wakakimbia au kutoroka eneo na pili kuhakikisha kuwa ukamataji huo unapofanyika basi maisha na usalama wa wahusika wote unakuwa umelindwa. Hili la pili lina umuhimu hasa mahali ambapo mlengwa anaweza kuhisiwa kuwa ana silaha au uwezo wa kujihami na hivyo kumshtukiza na kumfanya asijiandae.
Mfano wa Jeffrey Epstein
1564546205526.png
Marekani hivi karibuni bilionea maarufu ambaye sasa hivi yuko rumande Bw. Jeffrey Epstein (kushoto) alikamatwa na maafisa wa upelelezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu na tuhuma za zinaa na watoto wadogo. Hakutarajia kukamatwa lakini maafisa wa upelelezi walikuwa na waranti za mahakama na waliitegea ndege yake binafsi ikitua na wakaiwahi hapo hapo uwanjani. Wakati huku uwanjani anakamatwa maafisa wengine walikuwa wanavamia wakiwa na hati za upekuzi (search warrant) kwenye nyumba yake huko New York ambapo waliweza kukusanya ushahidi mbalimbali. Polisi walivunja mlango kuingia nyumba hiyo. Yote haya yalifanyika kwa nguvu kubwa ya polisi wa FBI.

Hivyo, kufanikisha uvamizi kama huo hasa dhidi ya mtu mwenye hela nyingi na ulinzi kama Epstein polisi ilibidi wajipange kweli kweli lakini pia wahakikishe kuna usiri mkubwa. Hata hivyo, kitu ambacho polisi hawakukifanya ni kuficha ni nani walikuwa wanamkamata. Hili lilikuwa ni muhimu kwani bila kujitambulisha kuwa ni maafisa wa polisi – kwa mavazi na vitambulisho au alama mbalimbali – ni rahisi kwa walinzi wa mtu kama Epstein kutumia nguvu kumlinda bosi wao.

Ipo na mifano mingine mingi ya uvamizi wa watu mbalimbali unaofanywa na polisi sehemu mbalimbali duniani wakiwa na malengo ya ama kumkamata mtuhumiwa au kukusanya ushahidi, kufanya uokozi n.k Lakini mahali pote yanapofanyika haya suala kubwa ni kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anakamatwa lakini vile vile kuhakikisha kuwa polisi hawaingii katika hatari isiyo ya lazima ambayo inaweza kusababisha umwagikaji damu.

Uvamizi wa Polisi Una hatari kwa Polisi na Watuhumiwa
Pale ambapo inatokea uvamizi unafanyika pasipo kubisha hodi (no-knock raids) basi
1564546387432.png
kwa washukiwa/watuhumiwa na polisi ni kubwa sana. Mapema mwaka huu huko huko Milwaukee Marekani mwezi Februari maafisa wa polisi walivamia nyumba ya mshukiwa na walivamia kuvunja mlango huku wakipiga kelele “Polisi Waranti” lakini aliyekuweko ndani Bw. Jordan Fricke alichukua bastola yake na kulenga mlango na kufyatua wakati mlango unafunguka tu; risasi ilimpiga afisa wa polisi Rittner ambaye alifariki.

Tukio jingine kama hilo ambapo uvamizi bila hodi ulifanyika lilitokea mapema Marekani huko Jiji la Houston ambapo maafisa wa upelelezi (undercover) walijaribu kuvamia nyumba ya washukiwa wakitumia hati ya upekuzi. Kulikuwa na madai ya watu kuuza madawa ya kulevya. Hata hivyo, uvamizi ulipofanyika bila kubisha hodi watuhumiwa 2 (wenye nyumba) waliuawa na polisi watano kupigwa risasi na kujeruhiwa. Baadaye imekuja kugundulika hati yenyewe ya upekuzi haikuwa sahihi na uamuzi wa kuvamia ulifanywa vibaya na afisa kiongozi (ambaye anatarajiwa kushtakiwa). Jiji la Houston likaamua kuacha kutumia uvamizi wa bila kupiga hodi.

Vyombo Vyetu vya Usalama Visionekane kama Wahalifu

Mojawapo ya malalamiko makubwa yanayotokea mara kwa mara wakati baadhi ya watu wanakamatwa ni kuwa wale watu wanaokamata kwanza wanakuja na magari yasiyo na alama za polisi, wanakataa kujitambulisha, na kitu pekee ambacho wanadhania ni utambulisho ni silaha walizonazo. Hili ni muhimu libadilike na libadilike haraka sana.

Ni hatari sana kuwafanya polisi au maafisa wa usalama wadhaniwe kuwa ni wahalifu. Mfano ambao bado hatujajua mwisho wake ni suala la Peter Zakaria wa kule Musoma ambaye aliachiliwa hivi karibuni kwa dhamana baada ya kukaa rumande kwa tuhuma za kutaka kuwapiga risasi wanaotajwa kuwa ni maafisa wa usalama wa taifa (na tuhuma za uhujumu uchumi). Kulikuwa na madai kuwa maafisa hao walikuwa wanaweka mafuta kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Peter Zakaria na kuwa Peter Zakaria aliona wakiwa na silaha na akataka kuwawahi (akidhania ni majambazi) n.k Hatujui yote kwa hakika lakini hatari hapa iko wazi kabisa. Kama watu hao walikuwa kweli ni maafisa ilikuwaje Peter Zakaria aone silaha zao; nini kilitokea kabla ya hapo, na je walijaribu kwa namna yoyote kumtishia nay eye akataka kujihami. Natabiri – kesi hii itafutwa – kwa maslahi makubwa ya usalama.

Uongozi wa Jeshi la Polisi na Vyombo Vingine vya Usalama Vijipange
Nimeandika hili kwa sababu hali ya kisiasa nchini ambapo watu wanapotea, wanatoweka, wengine kukutwa wamekufa katika mazingira ya kutatanisha inalazimisha kufikiria Zaidi. Matukio ya “watu wasiojulikana” kuvamia na kukamata watu yanahatarisha maisha ya wanaokamatwa n ahata wale wanaokamata hasa kama ni watu wa vyombo vya usalama.
Bila kuweka utaratibu unaojulikana wa kujitambulisha ni haki kwa wananchi kuanza kujilinda na kujihami dhidi ya utekaji wa makundi ya kihalifu. Wananchi wana haki ya kujihami na kuhami maisha yao na hata ya watu wengine kama wanahisi kuna vitendo vya kihalifu. Majambazi ndio hayawezi kujitambulisha. Wananchi wana haki ya kudhania (presume) kuwa mtu asiyejitambulisha na ana silaha ni mhalifu na ni jukumu la mwananchi au wananchi kujilinda. SI JUKUMU LA RAIA KUJUA NANI NI POLISI, NI JUKUMU LA POLISI KUJITAMBULISHA KWA RAIA NANI NI POLISI. Lilitokea kwa Peter Zakaria ni mfano wa nini kinaweza kutokea. Tusitegemee bahati.

Mapendekezo Yangu:
  • 1564546830807.png
    Maafisa wa Usalama wanaofanya Uvamizi ni lazima wawe katika mavazi yanayoweza kuwatambulisha kuwa ni maafisa polisi (hata tshirt/vesti) au vyombo vya usalama. Wote tumeona mara nyingi wenzetu katika nchi nyingi ambapo maafisa wanaofanya hivi wamevaa mavazi yenye maneno mbele na mgongoni “POLISI” AU “USALAMA” au “FBI” n.k Yote hii ni kuondoa utata. Rais atakayempiga au kumjeruhi mtu ambaye wazi amevaa mavazi hayo ni wazi amekusudia kumjeruhia au kumdhuru afisa wa usalama.
  • Hili si kwa polisi tu bali hata kwa maafisa wa uhamiaji ambao wanaenda kufanya kazi ya kumkamata mtu au watu ambao wanashukiwa kuwa wamevunja sheria ya uhamiaji. Wakati umefika kwa maafisa wa uhamiaji kuvaa mavazi yanayowatambulisha hivyo - UHAMIAJI na kama wanafanya kazi ya kipolisi basi wavae mavazi au alama zinazosomeka "POLISI UHAMIAJI". Wenzetu Marekani kwa mfano maafisa wa uhamiaji wanapofanya uvamizi au ukamataji huwa wamevaa fulana au nguo zenye maandishi ya ICE POLICE au "POLICE US Immigration" kama inavyoonekana hapa chini.
    1564609942371.png
  • Maafisa wa Polisi na usalama hata kama hawahitaji kuvaa mavazi hayo juu ni
    1564546942070.png
    wawe na beji za mkononi na hata zile za shingoni ambazo zitawaonesha kuwa ni maafisa wa polisi. Hili ni muhimu kwa maafisa wa upelelezi au wale undercover. Inapofika wakati wa kujitambulisha wanatoa beji zao (zining’ingie shingoni, kwenye shati au suruali) na hivyo wananchi wanajua nani ni afisa wa usalama na nani siyo.
  • Muhimu sana kabla ya kuanza uvamizi au ukamataji wa mtu yeyote ni muhimu polisi kujitambulisha wazi kwa sauti ili kusiwe na utata. Kwa mfano, mtu akibisha hodi na kusema “Polisi Fungua Mlango” raia anatakiwa kujua ni polisi na mlango unapofunguliwa anaoneshwa kitambulisho au hati ya upekuzi na hivyo kuondoa mikinzano yoyote isiyo ya lazima.
  • Ni muhimu taratibu zilizowekwa kisheria zinazoongoza ukamataji wa polisi (au watu wengine wanaoruhusiwa kisheria kukamata) ziwekwe wazi na watu wajue. Mahakama zianze kufuta kesi hasa kama itagundulika kuwa watuhumiwa hawakupewa haki zao za msingi wa kukamatwa. Tunapotaka watu wengine watii sheria bila shurti, na vyombo vya polisi vitii sheria hizo hizo bila shurti.
Tusipofanya Hivi
Natumaini ujumbe huu utawafikia wahusika. Sasa hivi vyombo vyetu vinacheza na moto; vinacheza na moto huku vimejimwagia petrol. Hatari iliyo mbeleni ni kubwa na mwisho wa siku mtawalaumu Watanzania kwa kujihami na kuwafungulia kesi watu ambao walikuwa watetea na kulinda familia zao. Tusisubiri majanga ndio tuanze kufikiria nini cha kufanya. Kwa sababu hata kama haijatokea bado nawahakikishia kwa asilimia 100 itakuja kutokea; tutapoteza maafisa wa polisi kwa mtindo huu. Watu wataenda kumkamata mtu au kuvamia nyumba ya mtu na watu wataamua kujitetea na tutaamka taifa zima likiwa na majonzi. Tusipofanya hili siku ya leo kwa tabasamu, tutajikuta tunalazimika kufanya jingine siku nyingine kwa machozi.
Tusiisubiri siku hiyo.
 

Attachments

  • 1564546945241.png
    1564546945241.png
    1.4 MB · Views: 58
Ushauri murua kwa wana usalama wetu, nguvu na mazingira ya ukamataji hayana uiano na kosa na mkosaji. Fanyeni hayo kwa opereshen maalumu za majambazi, unamkamata msanii Roma kwa nguvu kubwaa! Ama mwanafunzi Nondo! Usemalo limetokea tayari mwanaume mmoja huko kanda maalumu Tarime aliwafanyizia maafisa wa usalama ktk ambush kazini kwake.
 
Kinachoendelea ni kile ulichokiandika katika uzi fulani humu kuhusu mfumo nje ya mfumo na mfumo ndani ya mfumo.
Kiuhalisia hao wakamataji huwa siyo Polisi bali huigiza kuwa ni Polisi na inapptokea upepo ukawa mbaya sana ndipo Polisi huusishwa ili kutuliza hali. Kumbuka kuwa hali inakuwa mbaya kwao sababu hata katika mfumo nje ya mfumo kuna watu wana maslahi na wale wanao shughulikiwa hivyo hutokea mfumo wenyewe kupatwa na hofu ya kuja kufunuliwa mask in Public.
Kwa kifupi Polisi hawapangi haya bali huelekezwa kwenda ku cover tracks tu, kitu ambacho kinazidi kuwaweka wao katika wakati mgumu kabisa kitendaji na kiusalama.
 
Hupo sahihi sana kwa hili, Huko tuendako hili LAZIMA LITOKEE. Kwani kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa sana wa taratibu wakati wanafanya ukamataji wa watu ama watuumiwa. Katika nchi inayofuata sheria taratibu zinatakiwa kufuatwa ili kuepuka kadhia kama hizi.
Kama wanakijiji huko katikati ya nchi waliweza kuwaua wafanyakazi wa serikali wakifiki kwamba ni wanyonya damu, je huko tuendako hakutakuwa na uwezekano wa watu kuwaua wanausalama ama hata watumishi wa idara ya serikali wakifikiri kwamba ni ni WASIOJULIKANA?
Kwa maoni yangu, Kwa kipindi hiki cha teknolojia, habari inatembea haraka sana iwe ya kweli ama ya uongo na jamii yetu ya KiTZ ni kubwa, hivyo ni jukumu la Serikali kuwa makini sana kwa jambo hili, wawe wanajitambulisha kwanza la sivyo tunaweza kushuhudia mambo ya SA na US yakiwa yanatokea kila siku hapa kwetu. Vilevile wale wanatoa taharifa mapema na isiyokuwa na ukakasi Siyo kuwachia watu ambao si wahusika kutoa taarifa za idara za serikani kwa niaba yao. Inawezekana vipi mtu furani hana mamlaka yoyote ile anasema kufa ama kuuwawa kwa watu ni jambo la kawaida sana na bado akiachwa pia anachochea kuni na vijarida vyake?
Ni vizuri kumkamata kuku mweusi wakati wa mchana kuliko kusubiri giza liingine ndiyo unaanza mtafuta gizani.
 
..nakubaliana na hoja yako kwa asilimia 100.

..pia nimewahi kushuhudia viongozi wa upinzani wakisindikizwa chini ya ulinzi wa askari waliovaa kiraia na wamebeba silaha na muonekano wao ni kama majambazi.

..yaani viongozi wa upinzani walionekana kama wako chini ya ulinzi wa majambazi.
 
Kwamba suala la kutekwa na issues za "wasiojulikana" lipo Chini ya Siro. ...
Kuna usilolijua au usilotaka kulisema. ..
Wahalifu wote nchi hii hukamatwa angalao kwa utaratibu isipokuwa, narudia isipokuwa wakosoaji wa Serikali pekeee au wadhamini wa upinzani... hao ni mwendo wa "kutekwa" tu
Huitaji degree au kwenda Marekani kujua who is behind the movie. .....
Mateso ya wapinzani nchi hii ni magum kuliko hata ya magaidi. ....
Siasa za upande mmoja na ki dola
Bora tu tanga ze sisi ni nchi ya chama kimoja bas.... end of story.
 
Back
Top Bottom