Wazo la Biashara yenye mtaji mdogo kwa Wamama wa nyumbani

DustBin

JF-Expert Member
Jun 3, 2021
544
558
Katika vitu vinawatatiza wa mama wengi mtaani ni kupata shuguli itakayowaingizia kipato cha kutosha. Na kila wanapofikiria wazo la kuanzisha biashara basi wanakwazwa na ughali wa mtaji unaohitajika kuanzisha biashara hiyo au kama ni biashara yenye mtaji mdogo basi huwa haina faida kutokana na wingi wa wenye kufanya biashara hiyo.

Leo nimekuja na wazo la biashara kwa wakina mama hao, biashara ambayo haina kuhangaika kwa kujichosha. Ni biashara ambayo mama anaweza kuifanya na huku shuguli zake za nyumbani akizitekeleza kama kawaida. Ni ujuzi tu ndio ambao unahitajika, na ujuzi wake mama anaweza kuupata kwa kujifunza kwa rafiki au mtu yeyote anaejishugulisha na biashara hiyo. Nayo ni ususi wa makapu.

Makapu ni bidhaa inahitajika sana katika maisha ya sasa. Makapu haya hutumiwa na watu wa aina zote, kuanzia wanawake na hata wanaume. Sehemu kama sokoni, dukani, gulioni, hospitali nk. Utakuta watu wengi wakiwa wamebeba makapu hayo. Hapa nazungumzia makapu ya kufumwa kwa kutumia mikanda ya plastki (plastic strips) ile inayotumiwa kufungia marobota (mabalo) ya mtumba. Biashara ya makapu ina faida sana hasa katika maeneo ya mjini. Nasema hivi kwa sababu gharama za kununua bunda moja la zile kamba za kufumia ni nafuu sana ukilinganisha na idadi ya makapu utakayoyafuma kwa bunda moja hilo.

Gharama ya bunda moja la kamba huwa ni kati ya elfu thelathini hadi arobaini inategemea na maeneo. Na bunda moja hutoa makapu zaidi ya kumi ambapo kapu dogo la chini linauzwa shilingi elfu nne na kubwa kabisa mpaka elfu kumi na tano kutegemea na eneo ulilopo na mahitaji yake. Ili uweze kutengeneza kapu lenye mvuto unahitaji upate bunda tatu za kamba za rangi tofauti hivyo kukugharimu elfu tisini hadi laki moja na ishirini elfu. Utanunua mkasi kwa ajili ya kukatia kamba au unaweza ukatumia mkasi wanyumbani, pia utanunua kamba kwa ajili ya mikono ya kushikia ingawa wengine hutumia kamba hizo hizo za kufumia kutengeneza mikono ya kapu.

Kwa kuzingatia mama anafanya kazi za nyumbani, kwa siku anaweza kutengeneza makapu mawili au matatu. Hivyo kwa wiki anaweza akamaliza bando moja kama ataifanya kazi hiyo kila siku.

Soko la kuuzia makapu ni hata hapohapo nyumbani anaweza akayapanga akapata wateja. Au anaweza akaongea na mtu yeyote katika ndugu zake au rafiki zake wenye maduka mjini au sokoni akayapanga huko, au akamtafuta kijana akawa anayapitisha mitaani. Huyo kijana anaweza akawa anampa ujira wake au wakakubaliana katika kila kapu atakalouza kijana atapata kiasi kadhaa.

Kuna wana mama nimeona wamefanikiwa kwa biashara hii, ewe mama wa nyumbani hujachelewa unaweza ukapanga mipango yako sasa ukaanza kujishugulisha kwa biashara hii ambayo haina shuruba wala idhilali na huku ukiendelea kutekeleza majukumu yako ya nyumbani kama kawaida.


DustBin
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom