Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,808
- 11,973
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) ameongoza maadhimisho ya miaka ya 95 ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (Chinese People’s Liberation Army) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1927, maadhimisho haya yamefanyika kwenye Ubalozi wa China hapa Nchini.
Akiongea wakati wa hafla ya kuadhimisha kuanziswa kwa Jeshi hilo, Waziri kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Maafisa pamoja na Askari wote wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu yenye kumbukumbu tele na nzuri zinazoakisi mafanikio mbalimbali tangu kuanzishwa kwake.
Aidha, katika hotuba yake, Waziri aliwasilisha pia, Salaam za Pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Dkt. Stergomena amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa Jeshi hili, limekuwa ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha watu wa Taifa la China na kuwafanya kuwa wamoja hadi hapo mwaka 1949, ambapo mwasisi wa Taifa hilo la China, Hayati Mao Tse Tung alipotangaza kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Waziri ameongeza kwa kusema kuwa kwa miaka 95 iliyopita, Jeshi hili limeweza kutoa mchango mkubwa katika kulinda utaifa, usalama, masilahi ya Taifa, kulinda na kudumisha amani na usalama duniani. Kupitia Jeshi la Ukombozi la watu wa China tumeweza kushuhudia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, siasa za kidunia pamoja na kiuchumi.
Jeshi la Ukombozi la Watu wa China linapodhimisha Miaka 95 ya kuanzishwa kwake ifikapo tarehe 01 Agosti, 2022 tunapongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa mafanikio yake kitaifa, kikanda na kimataifa Serikali ya Tanzania inathamini mchango na ushirikiano baina ya Tanzania na China katika ngazi ya kimataifa katika kulinda maslahi baina yetu.
Chini ya Uongozi imara wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha mahusiano ya kihistoria na Serikali Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa Tax amesema pia, kuwa Tanzania itaendelea kukumbuka misaada iliyotolewa na China kupitia Ujenzi wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Ujenzi w Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC), Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi- Monduli (TMA) pamoja na taasisi nyingine za kitaaluma.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia, na Balozi wa China hapa nchini Bi. Chen Mingjian, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Jacob John Mkunda, Viongozi wa Chama na Serikali, Wakuu wa Kamandi na Waambata Jeshi wanaowakilisha majeshi yao hapa nchini.