..Mateo Qares namkubali kama mtu asiyekuwa na uoga kutetea lile analoliamini.
..alikuwepo hata kwenye lile kundi maarufu la G-55.
..wananchi wa Mbeya wanakumbuka kama mtu asiyependa majungu ktk kazi.
kikwete ongoza nchi na hatumwoni so far wa kusema wewe haufai
Pamoja na habari nzuri ila simuamini kabisa huyu mwandishi.nafahamu kuwa sio muadilifu na najua ameandika stori hii kwa sababu zake nyingine wal si za kiuandishi.Waziri wa Mkapa amshukia Kikwete ataka CCM imtose 2010
ATAKA CCM IMTOSE 2010 KAMA HAWEZI KUFANYA MAAMUZI MAZITO
Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa zamani katika serikali ya awamu ya tatu, Matheo Qares ameshauri kuwa CCM isimsimamishe tena Rais Jakaya Kikwete kutetea wadhifa huo iwapo atashindwa kufanya maamuzi magumu ya kusafisha watu wachafu ndani ya chama hicho.
Wakati Qares akisema hayo, waziri mwingine katika serikali ya awamu ya pili, Mussa Nkangaa amesema CCM imepoteza hadhi yake ya kuwa chama cha wafanyakazi na wakulima na ndio maana inashindwa kuwashughulikia watuhumiwa katika kashfa za Richmond na Kagoda.
Wawili hao walikuwa wakichangia mada katika siku ya mwishoni ya kongamano la siku tatu la kumuenzi muasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kufanyika jijini Dar es salaam.
"Ninayemzungumzia sasa kwamba achukue maamuzi magumu si mwingine, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano," alisema Qares ambaye aliwahi kuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya wakati akizungumzia kushuka kwa maadili ya uongozi nchini katika miaka ya kifo cha Nyerere.
"Anaweza kuchukua maamuzi magumu kwa kufumba macho na kuwashughulikia hao wanaosema hakujuana nao barabarani, kwa kupitisha wino mwekundu akawa rais mzuri tu. Lakini kama atashindwa, basi ashauriwe miaka yake mitano inamtosha.
"Chama kitafute mwanachama mwingine atakayekuwa na uwezo wa kufanya maamuzi magumu; kwanza huu utaratibu wa miaka kumi ni hisani yetu tu ndani ya CCM, naomba hili lizingatiwe."
Makombora hayo mazito ya Qares yalimfanya mwenyekiti wa kongamano hilo, Dk Salim Ahemd Salim kulazimika kutoa ufafanuzi mwishoni kuwa kazi ya kongamano hilo ni kukusanya maoni na kwamba mtu yeyote anaweza kutoa mawazo mbadala.
Qares, ambaye alionekana kujiandaa vema kurusha makombora hayo, alisema CCM sasa imechafuka kutokana na kushikwa na matajiri wachache wakubwa ambao ni wachafu na ambao hawajui historia ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Qares, ambaye aliwahi kushika wizara nyeti ya Menejimenti na Utumishi wa Umma iliyokuwa chini ya Ofisi ya Rais, chama hicho kinavurugwa na watu hao ambao pia alisema wanavuruga nchi.
Alisema hoja ya msingi ni mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni rais kujiandaa kufanya maamuzi magumu kwani hiyo itamuweka katika nafasi nzuri, lakini vinginevyo ashauriwe mwakani apumzike kwa kuwa miaka mitano aliyoongoza inamtosha.
"Siku moja niliwahi kumuuliza (katibu mkuu wa CCM, Yusuf) Makamba kwanini matajiri wachafu ndani ya chama wasing'oke, akanijibu sasa wewe unataka matajiri waende chama gani?" alimnukuu Makamba.
"Nilikaa kimya, baadaye nikafikiri sana, lakini sasa ni wakati wa maamuzi magumu."
Qares alisema kibaya zaidi ni kwamba baadhi ya matajiri hao waliovamia CCM ni wageni.
"Matajiri hao hawana wala hawajui hata historia ya CCM, wengine kwanza uraia wao una utata ni wageni."
Baada ya kumaliza kutoa mchango wake ulioufanya ukumbi kuzizima, Dk Salim, ambaye alionekana kumudu vema mkutano huo, alisema: "Ndiyo maana ya mkutano huu. Hapa tunapokea maoni ya watu mbalimbali, lakini si lazima yakubalike na wote, wengine wanaweza kupinga au kukubali."
Dk Salim alisema kongamano hilo lilikuwa la maana kwa ajili ya kujaribu kuzuia mianya ya kuivuruga nchi na kusisitiza umuhimu wa maadili ya uongozi.
Awali, waziri mwingine wa awamu ya pili, Musa Nkangaa aliituhumu CCM kuwa imepoteza hadhi yake na kujikuta ikikumbatia matajiri wachafu.
Kwa mujibu wa Nkangaa, CCM imekuwa si chama cha wakulima na wafanyakazi tena, bali kimebaki kuwa chama cha matajiri.
"Ndiyo maana imekuwa ikiweweseka kuwashughulikia watuhumiwa wa Richmond na Kagoda," alisema akimaanisha kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa Richmond Development Company LLC na tuhuma za wizi wa mabilioni ya fedha kutoka BoT.
Nkangaa, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maji na pia Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), alisema ni lazima wananchi watambue nafasi yao katika kufanya maamuzi katika nchi.
Kwa mujibu wa Nkangaa, Watanzania wanapaswa kujitambua kwa kuwa bila ya kufanya hivyo mambo yatazidi kuwa ya ovyo na kujikuta wakiendelea kuwa maskini katika nchi yao yenye utajiri.
Aliitaka Taasisi ya Mwalimu Nyerere, ambayo iliandaa kongamano hilo la siku tatu, iandae sifa za mtu kuwa kiongozi na kuweka bayana kwamba wala rushwa hawafai kuongoza nchi.
Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kikristo (CCT), Peter Kikula alitoa tahadhari kwa vyama vya siasa kuacha kuingiza mambo ya Mahakama ya Kadhi na mpango wa Tanzania kujiunga katika Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC), kwa kuwa masuala hayo yatavunja katiba ya nchi.
Kiongozi huyo alisema tayari halmashauri kuu ya jumuiya hiyo ilitoa mapendekezo yake na kuyawasilisha serikalini ili kuepusha vyama kutumia dini kujipatia kura hapo mwakani.
Naye Nape Nnauye alieleza wasiwasi wake kama mfumo uliopo wa mamlaka za uwajibishaji unaweza kutoa ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya msingi ya kimaadili katika uongozi, hasa wa umma.
Nape alihoji kuwa kama mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alipaswa kuwajibishwa na mamlaka ya juu, lakini hakuwajibishwa, nini kitafuata baada ya mamlaka hiyo kushindwa kumwajibisha.
"Ninachosisitiza ni kujaribu kuangalia mfumo wetu ukoje, kwa mfano mkurugenzi wa Takukuru alipaswa kuwajibishwa, lakini anapita mitaani na kutamba hajiuzulu... lakini anayepaswa kumwajibisha naye hamwajibishi, sasa hapo tunafanye?"
Naye Profesa Issa Shivji alionya kwamba maadili ya uongozi ni kitu muhimu ambacho kinapaswa kupewa kipaumbele na kusimamiwa vema.