Waziri wa JK ashinikiza dhamana kwa watuhumiwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waziri wa JK ashinikiza dhamana kwa watuhumiwa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Zak Malang, May 22, 2010.

 1. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #1
  May 22, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Waziri wa JK ashinikiza dhamana kwa watuhumiwa

  Ni waliokutwa na viungo vya binadamu, DC, Polisi wakiri kupata maagizo

  MMOJA wa mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete anatuhumiwa kushinikiza kuachiwa kwa dhamana ndugu wawili waliokamatwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na viungo vinavyosadikiwa kuwa vya binadamu.


  Taarifa hizo za waziri huyo, ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa, kuhusishwa katika kashfa hiyo, ni mwendelezo wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne kuingia kwenye kashfa ambazo baadhi zimetinga mahakamani na nyingine kutolewa maamuzi.

  Taariofa hizo pia zimeibuka siku chache baada ya mtu anayedaiwa kuwa mtoto wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Celina Kombani kuhusishwa na tukio la utekaji kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Minja, tukio ambalo polisi imesema inaendelea kulichunguza wakati watuhumiwa wakiwa mahabusu.

  Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka wilayani Urambo mkoani Tabora zinasema waziri huyo alishinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa hao kwa kumtumia mkuu wa wilaya hiyo, Anna Magoha.

  Habari zinasema kuwa watuhumiwa hao waliokamatwa walikuwa wakiuza mifupa hiyo ya binadamu kwa kukata vipande vidogovidogo ambavyo waliviuza kila kimoja kwa Sh2,000.

  Ilielezwa kuwa viongozi wa Kata ya Kaliua, akiwemo diwani, waliandaa watu kwa maelekezo ya waziri huyo ambaye alikodi magari mawili ambayo Jumatano wiki hii yaliwapeleka watu ambao walienda kufurika kwenye ofisi ya Magoha kulalamikia kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

  Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Magoha alikiri kupokea malalamiko ya watu hao na kwamba kutokana na maelezo ya mashahidi walioshuhudia watuhumiwa hao wakikamatwa, waziri huyo aliwaita polisi, akiwemo mkuu wa upelelezi wa wilaya hiyo, na kuagiza watuhumiwa hao wadhaminiwe.

  “Nafahamu kwamba suala hilo ni la kisheria zaidi, lakini, kwa kweli watu walikuwa wengi na malalamiko yao nilihisi yalikuwa ya msingi, nikawaita polisi akiwemo OC-CID, nikazungumza nao na kuwaagiza wataalamu wa sheria wapitie sheria kuona zinasemaje, nikaagiza wadhaminiwe wakati uchunguzi ukiendelea,” alieleza Magoha.

  Kwa mujibu wa habari za kimahakama, waliokamatwa na viungo hivyo vinavyodhaniwa kuwa ni vya binadamu ni Risasi Jumanne, 27, na Mashaka Juma, 26, wakazi Kaliuwa kitongoji cha Mwangaza.

  Kamanda wa polisi mkoani humo, David Mwakiruma, alithibitisha taarifa hizo na kueleza kwamba watuhumiwa hao walitiwa mbaroni Jumapili iliyopita wakiwa na viungo hivyo.

  Alisema polisi ilipata taarifa za kuwepo kwa watu wanaouza vipande vya mifupa ya viungo vya binadamu, ambavyo walikuwa wakiuza kila kipande kidogo Sh2000 na baada ya kufuatilia polisi ilibaini kuwepo dalili za ukweli na baada ya kufanya upekuzi ndani ya nyumba ya watuhumiwa wakiongozwa na kamanda wa upelelezi wa wilaya hiyo, ASP Kaijanente, walibaini viungo hivyo.

  Alisema upekuzi huo ulifanyika saa 12:50 jioni, Jumapili mbele ya mwenyekiti wa kitongoji hicho na jirani wa watuhumiwa na kwamba ndani ya chumba kimoja kati ya viwili vinavyotumiwa na watuhumiwa hao, darini kulikutwa viroba viwili kimoja kikiwa na madaftari.

  Kifurushi kingine kinaelezwa na Mwakiruma kuwa kilikutwa na fuvu la kichwa kilichopasuliwa katikati, lakini kikiunganishwa kinaonyesha kuwa ni cha binadamu, taya la gego la chini lenye meno matatu na mfupa mmoja wa mguu kuanzia gotini kuteremka chini.
  Vipande vyote vinasadikiwa ni viungo vya binadamu na polisi imesema vitapelekwa kwa mkemia mkuu wa sarikali ili vichunguzwe.

  Taarifa kutoka Mirambo zilisema watuhumiwa walifikishwa mahakamani Juma nne wiki hii na kusomewa shitaka la kukutwa na viungo vya binadamu.

  Wafuatiliaji wa sakata hilo walilieleza Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao kuwa dhamana hiyo ilitolewa juzi jioni baada ya Magoha kuwaita viongozi wa polisi na hakimu wa wilaya hiyo ofisini kwake na kuwashinikiza watekeleze agizo hilo linalosadikiwa kutolewa na waziri huyo.

  Source: Mwananchi
   
 2. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #2
  May 22, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Ingawa gazeti linahifadhi jina lake, huyu waziri atakuwa ni Kapuya tu. Ni yeye pekee anayeweza kufanya madudu makubwa yoyote serikalini na akaachwa. Kumbuka: Kashfa ya wizi wa mitihani (mwaka 1998), kashfa ya matumizi ya ndege za JWTZ (2006) ni mifano miwili mizuri. mimi nina wasiwasi sana kwamba yeye ni mshirikina mkubwa katika matumizi ya viungo hivyo vya binadamu na ndiyo maana (anaamini) haguswi. Kwa hivyo si ajabu akawatetea watuhumiwa hao.

  Aidha Kapuya kafanikiwa kumfanya JK aamini kuwa yeye ndiye alifanikisha ushindi wake Mkoani Tabora mwaka 2005.
   
 3. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #3
  May 22, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Inafanya kampeni nzima ya serikali ya JK ya vita dhidi ya mauaji ya Albino kuonekana ni kichekesho kikubwa! Mungu ibariki Tanzania!
   
 4. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #4
  May 23, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Huu ni uingiliaji wa mahakama unaofanywa na wanasiasa. Hii nchi polepole inaanza kwenda arijojo na hakuna nayejali! Utawala wa kambare -- ambapo kila mtu anajiona ana sharubu -- umeanza kujisimika.
   
 5. Ruge Opinion

  Ruge Opinion JF-Expert Member

  #5
  May 24, 2010
  Joined: Mar 22, 2006
  Messages: 1,696
  Likes Received: 306
  Trophy Points: 180
  Kidogo kidogo tunaanza kupata mwanga ni akina nani ni wateja wa viungo vya binaadamu viwe vya albino au ngozi za watu wanaochunwa. Lakini ipo siku yatawapata yaliyompata Ditopile wa Mzuzuri. Yeye na aliyemuua sasa wako pamoja. Nani mkubwa wa mwenzie huko?
   
Loading...