Waziri: Viongozi wengi mafisadi

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
Chikawe%289%29.jpg

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, amesema viongozi wa umma wanaojaza fomu za matamko wakati wa kuorodhesha mali zao, hawesemi ukweli kutokana na wengine kupata mali hizo kwa njia za ufisadi.
Kadhalika, Waziri Chikawe alisema theluthi moja ya fedha za serikali zinapotea katika rushwa na ufisadi, hivyo wizara yake kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itahakikisha zinarejeshwa serikalini.
Akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jana jijini Dar es Salaam, Waziri Chikawe alisema ukiwepo utendaji wa ushirikiano katika kazi, watatimiza misingi ya utawala bora na maadili. "Kwa sasa viongozi wengi hawasemi ukweli, wanadanganya kwa sababu hawawezi kueleza jinsi gani wamepata mali zao… wengine wamezipata kwa njia ya ufisadi hivyo ni vigumu kupata ukweli halisi," alisema Chikawe ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Utawala Bora katika Baraza la Mawaziri jipya lililoundwa na Rais Jakaya Kikwete baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba.
Waziri Chikawe aliongeza kuwa: "Wale viongozi 7,888 kwa sasa wanaotakiwa kujaza fomu mhakikishe wanajaza zote na mnazihakiki, ofisi yangu iko wazi njooni tuzungumze pale panapohitaji msaada wangu msilete majungu." Waziri huyo alisema Sekretarieti hiyo inakabiliwa na changamoto kwa sababu bado haijajijenga kwa jamii.
Alisema utawala bora unakuwa chini ya sekta zote za nchi ambayo msingi wake mkubwa ni maadili.
Viongozi wengi wa umma wamekuwa wakilalamikiwa kwa kutotoa matamko ya mali zao na wengine wanalalamikiwa kwa kutoa matamko ya uongo. Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa ni makosa kisheria kwa viongozi wa umma kutotoa matamko ya mali zao. Hata hivyo, hakuna kiongozi hata mmoja aliyechukuliwa hatua kwa kuvunja sheria hiyo.
Mbali na Sekretarieti ya Maadili, taasisi nyingine ambayo iko chini ya Waziri wa Utawala Bora ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Nayo imekuwa ikilaumiwa kwa kutokuendesha mambo yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kufumbia macho tuhuma kubwa za rushwa zinazowahusu vigogo. CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom