Waziri sonyo aja na mwisho wa siku ya siku

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MWIMBAJI mahiri nchini, Waziri Sonyo ameibuka na wimbo mpya uitwao Mwisho wa Siku ya Siku.

Akizungumza Dar es Salaam Desemba 16 Sonyo alisema wimbo huo utakuwa katika albamu yake binafsi anayoiandaa ambayo itakuwa moto wa kuotea mbali.

Mwimbaji huyo aliyesema ameibuka kwa kasi ya ajabu, alieleza kuwa anashukuru kwamba matatizo yaliyokuwa yakimkabili yamekwisha na sasa anajipanga upya kuwapa mashabiki wake vitu vya uhakika.

Sonyo alikuwa akikabiliwa na shitaka kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tanga akidaiwa kula njama na kuiba pikipiki tangu Septemba mwaka jana, lakini Oktoba mwaka huu alipewa adhabu ya kifungo cha nje kutokana na kukutwa na hatia ya kupatikana na pikipiki ya wizi.

Katika kesi hiyo Sonyo na washitakiwa wengine wawili ambao ni Ally Saidi na Mohamed Mabranto, walishitakiwa kwa tuhuma za kula njama na kuiba pikipiki aina ya Yamaha CC200, tukio lililohusisha matumizi ya silaha, ambapo washitakiwa wote walikana tuhuma hizo.

“Wote wanaoenda jela si kwamba wana hatia, lakini pia wote wanaokaa uraiani si kwamba ni wema, wengine ni wahalifu wa kutupwa, lakini tunao mtaani.

“Wengine ni waungwana, lakini wapo magerezani, wengine kwa kesi za kutungwa, wengine kwa kushindwa kujitetea na kujua haki zao, ndivyo dunia ilivyo.

“Lakini matatizo yameumbiwa binadamu, wala hayajaumbiwa nyani, tayari nimeyakabili, nilichomekewa pale kuna watu walikuwa na nia mbaya na mimi, ila yamekwisha. Sina kinyongo na yeyote, yaliyopita yameshapita sasa tugange yajayo.

“Nawaomba mashabiki wangu wanielewe kwamba najipanga upya kuhakikisha nawapa burudani ya kutosha.

Nahitaji kuingia studio kurekodi, lakini tatizo kubwa ni gharama zimekuwa kubwa, ndio napambana angalau nikamilishe jambo hilo,” alisema.

Aliwaomba wadau mbalimbali wakiwemo mashabiki wake kumuunga mkono kwa hali na mali ili aweze kutimiza ndoto yake ya kukamilisha albamu hiyo, ambayo bado hajaamua itaitwaje.

Alisema wimbo wa Mwisho wa Siku ya Siku utakuwa moto wa kuotea mbali na kutaja nyimbo nyingine kuwa ni Nani Ajuaye ambao tayari umesharekodiwa, Penzi la Sumu, Wazazi Wangu, Ndugu Zangu na Hatima Yangu.

Anasema kama akifanikiwa kuingia studio na kurekodi nyimbo hizo, atakuwa amekata kiu ya mashabiki wa burudani nchini alioeleza kuwa wamemmisi kutokana na kutoona kazi zake kwa muda mrefu.

Msanii huyo amepata kung’ara na bendi za Chuchu Sound, TOT Plus, African Revolution ‘Tamtam’ na Mviko Sound.
 
Back
Top Bottom