Waziri Sitta: viongozi wanawaza kwanza matumbo yao

dosama

JF-Expert Member
Dec 25, 2010
912
957
NA GODFREY MUSHI
18th May 2012 IPP MEDIA


Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amerusha kombora jipya dhidi ya mwenendo wa viongozi wa Tanzania, safari hii akisema kuwa, taifa lina sura na muundo wa viongozi wa aina mbili, ambao ni viongozi wanaofikiri kwa kutumia matumbo yao pamoja na waliojaliwa uwezo wa kufikiri na kutumia akili zaidi ya kuwatumikia wananchi.

Sitta alisema kuwa viongozi wachache wamepewa uwezo wa kufikiri na kutumia akili zaidi ya kuwatumikia Watanzania, lakini wapo baadhi ya viongozi wanaotumia matumbo yao kufikiri badala ya kutumia uwezo waliopewa na mwenyenzi Mungu.

Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, alisema viongozi wa aina hiyo wanajipambanua kwa ubinafsi, rushwa na ulafi wa madaraka.

Waziri Sitta aliyasema hayo jana wakati akitoa mada yake kuhusu mbinu za kisheria na utoaji wa huduma za kisheria nchini Tanzania, wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa (Iuco) katika kongamano la siku ya sheria iliyoandaliwa na Kitivo cha Sheria cha chuo hicho.
*
“Msishangae, sasa hivi tunao viongozi wa aina mbili hapa Tanzania, kwanza tunao viongozi wanaofikiri kwa kutumia matumbo yao kwa maana ya ubinafsi, rushwa na ulafi wa madaraka,” alisema Sitta na kuongeza:

*“Lakini pia tunao viongozi wachache ambao wanatumia ubongo waliopewa na mwenyenzi Mungu kuwatumikia wananchi kwa dhati kutoka moyoni...Hao ndio viongozi tulio nao.”

*Alisema kwa hali ilivyo hivi sasa, taifa halina budi kufikiria na kumpata kwa umakini Rais ajaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuwa atakuwa na kazi ya kuliokoa taifa lilipofikia kwa kuhakikisha kwamba anafuta aina ya makundi ya viongozi waliopo.

*“Hawa wanaofikiri kwa matumbo wanawaza namna ya kujilimbikizia mali na wana sura ya ubinafsi, hiyo ni lazima ifike mahali serikali ihakikishe wanaweka bayana mali zao na wananchi wanafahamu,” alisema Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.

“Mimi ni miongoni mwa hao viongozi wanaotumia ubongo wao kuwatumikia wananchi, lakini ninajivunia pia kwamba ni Spika wa Bunge la Tisa ambaye nimelisuka Bunge ambalo mnaliona hivi sasa linavyofanya kazi na viongozi wanahaha...Mimi ni muumini mzuri wa falsafa za Mwalimu Nyerere kuhusu ‘Utu na Usawa’ ndiyo maana nalaani *kufutwa kwa Azimio la Arusha kwamba ni pigo kwa sababu dhana ya uwajibikaji imekufa,” alisisitiza Sitta.

Kuhusu ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sitta, alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo hivi sasa wanafikiri njia bora na namna ya kuwa na sarafu moja, soko la pamoja na Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano huo.

“Mahali tulipofikia siyo pabaya, maana hivi sasa tunatafuta njia bora za namna ya kuwa na sarafu moja itakayotumika kwa nchi zote, lakini pia kuwa na soko la pamoja la bidhaa pamoja na kuwa na shirikisho la kisiasa la Afrika ya Mashariki," alisema.
*
Akielezea kuhusu changamoto za ajira katika jumuiya hiyo, Waziri Sitta, aliwataka wanachuo hao na Watanzania kwa ujumla kutoogopa kuomba ajira ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwa kigezo cha lugha ya Kiingereza kutumiwa kikamilifu na baadhi ya nchi kwa kuwa ukweli ni kwamba hata mwanafunzi bora wa insha katika nchi za jumuiya hiyo mwaka jana alitokea Sekondari ya Mazinde mkoani Tanga.
*
Akichangia katika kongamano hilo, mmoja wa wakufunzi wa Chuo hicho, Edward Ndunguru, alisema pamoja na serikali ya Tanzania kuwa na sheria bora zilizoigwa kutoka Uingereza na India, kuna haja katika Katiba mpya ijayo Rais wa nchi akapunguziwa madaraka na Katiba hiyo itamke wazi kwamba kiongozi huyo mkuu wa nchi atawajibishwa kikatiba pale atakapobainika kutenda makosa.

*“Tunashauri katika katiba mpya ijayo Rais wa nchi apunguziwe madaraka yake na tunataka Katiba itamke wazi kwamba akikosea atashitakiwa mahakamani kuliko katiba tunayoitumia sasa inavyompa kinga ya kisheria,” alisema Ndunguru.
*
Naye Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Tumaini, Profesa Seth Nyagava, alisema njia pekee ya kuwakomboa Watanzania katika lindi la umasikini ni kuwanoa ili waweze kuingia kwa uhakika katika soko la pamoja pasipo kuwa na shaka.
*
Katika kongamano hilo, Waziri Sitta aliwatunuku vyeti wanafunzi wa mwaka wa tatu wanaohitimu masomo yao wakiwa wanachama wa Jumuiya ya Wanasheria wa Tumaini (TULS) kwa kipindi chote cha masomo yao chuoni hapo.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom