Waziri Kombani adai wanaodai Katiba mpya ni watu 'wa barabarani'
Kauli ya Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, kwamba wale wanaodai katiba mpya ni watu wa barabarani wasiokuwa na uelewa juu ya masuala hayo, hakika imetusikitisha sana. Kwamba sauti zinazoendelea kupazwa kuhusu umuhimu wa kuandika katiba mpya zinatoka katika vinywa vya watu wa kawaida wanaotembea kwa miguu, kwa kweli ni kauli tete inayofaa kulaaniwa na wananchi kwa nguvu zote.
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen mwanzoni mwa wiki, waziri huyo pia alisema hakuna umuhimu wa kuwapo katiba mpya na kwamba Serikali inaridhika na utaratibu uliopo wa kuifanyia katiba hiyo marekebisho ya mara kwa mara pindi umuhimu wa kufanya hivyo unapokuwapo. Alisema kuwa Serikali haiko tayari kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya kwa sababu wanaodai kuwapo kwa katiba hiyo hawajapeleka maombi yao serikalini kwa maandishi.
Waziri Kombani alisema maombi hayo lazima yaainishe vifungu vya katiba ambavyo wanaona vina utata na wapendekeze vifungu mbadala, lakini alionya kwamba suala hilo lina gharama na sio kipaumbele cha Serikali wala wananchi. Alisema hayo mara baada ya kuhudhuria kikao cha baraza jipya la mawaziri kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Tumelazimika kuelezea kauli ya waziri huyo kwa kirefu ili kuwatoa mashaka watu wanaoweza kudhani kuwa labda kauli yake ilikuwa mawazo yake binafsi, hivyo ilitolewa kwa nia njema tu, au kwamba kauli hiyo aliitoa kwa niaba ya Serikali, kwa maana ya kufikisha ujumbe kwa watu na asasi zinazodai katiba mpya kwamba Serikali ya Rais Kikwete haitafanya kitu kama hicho, wala hailazimiki kufanya hivyo kwa sababu suala hilo halimo katika Ilani ya chama tawala kinachounda serikali hiyo.
Ni kauli inayofifisha matumaini ya Watanzania waliodhani kwamba huu ulikuwa wakati muafaka wa kusimika katiba mpya ambayo ingebeba matakwa ya wananchi wengi badala ya katiba ya sasa ambayo ni matokeo ya mawazo na matamanio ya kundi dogo la wakereketwa wa chama tawala. Ni kauli inayolenga kuihalalisha katiba iliyopo ambayo imewekwa viraka vingi kiasi cha kutokuwa tena na nafasi ya kupachika viraka vingine. Ni kauli isiyo na ujasiri wa kutenda, bali woga wa kufanya mabadiliko kukidhi matakwa ya wananchi walio wengi na kwa wakati uliopo.
Ni kauli yenye kubeba ujumbe mzito wenye shari na jeuri. Waziri anaposema kuwa kuandika katiba mpya hakuna maslahi kwa Serikali wala taifa, hana lengo lolote zaidi ya kuwadhihaki na kuwadhalilisha wananchi wenyewe ambao kwa muda mrefu sasa, wameonyesha kiu ya kupata katiba mpya yenye kukubalika kwa wengi na kuondoa uwezekano wa kufarakana katika masuala ya msingi, ikiwamo kupata viongozi waliotokana na ridhaa ya wananchi kutokana na kuwapo tume huru ya uchaguzi itakayosimamia chaguzi zilizo huru na haki.
Tumesema tena na tena kwamba suala la katiba mpya ni la Watanzania wote na kuwa nchi yetu haina njia mbadala ya kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinakuwa vitu vya kudumu isipokuwa kusimika katiba mpya itakayokubalika kwa wengi. Ndio maana tumekuwa tukisisitiza kuwa ni vizuri Serikali ya Rais Kikwete ikajipanga sasa na kuanza mchakato wa kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata katiba mpya ndani ya miaka mitano ijayo.
Hoja yetu daima imekuwa kwamba tusisubiri machafuko ndipo tutende, kwamba tutende wakati tukiwa bado wamoja, kwani kutenda baada ya kufarakana na kutengana au kutenda wakati nyoyo na mitima yetu ikiwa tayari imegubikwa na chuki, visirani na dhamira ya kuangamizana wenyewe kwa wenyewe, tutakuwa hatuwezi kutenda tena kwani hatutakuwa tena watu timamu bali wendawazimu.
Source: MWANANCHI 1st December 2010