Waziri Mwakyembe aiagiza BAKITA kudhibiti upotoshaji Kiswahili

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,007
9,873
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amelitaka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kuwasajili wafasiri, wakalimani na wataalamu wa lugha ya alama, ili kuboresha matumizi fasaha ya Kiswahili na kuzuia upotoshaji.

Pia, amewataka BAKITA kuwabana wachapishaji wa vitabu kabla ya kuingia sokoni mpaka vipate ithibati, wamiliki na walimu wa vituo vya kufundishia Kiswahili kwa wageni kupewa vyeti vya utambuzi.

Alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kanuni za sheria mpya za BAKITA.

“Vitabu vyote vipate ithibati, vitakavyobainika havina ithibati viondolewe na muhusika achukuliwe hatua,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema hatua ya kutoa vyeti kwa vituo vya kufundishia Kiswahili kwa wageni itasaidia kuwapo kwa vituo vyenye ubora na kuwaondoa watoa huduma wasio na uwezo.
Naye, Kaimu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi akizungumzia kuhusu kanuni hizo, alisema lengo ni kuliwezesha BAKITA kusimamia shughuli za maendeleo na matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha, kuhimiza, kuzuia upotoshaji wake.

“Licha ya kanuni hizi kuwalenga watumiaji wote wa lugha ya Kiswahili, hata hivyo kuna makundi na wadau mbalimbali ambao wataguswa moja kwa moja na masharti ya kanuni hizi,” alisema Mushi.

Mushi alisema wamiliki na walimu wa kufundisha Kiswahili kwa wageni watapaswa kupata vyeti vya utambuzi kutoka BAKITA, kupitisha mitaala na vitabu.
Alisema waandaaji wa matamasha ya Kiswahili kwa wageni watapaswa kuomba idhini ya kuandaa tamasha au shindano la Kiswahili kwa BAKITA.

Pia, vyombo vya habari vitapaswa kupata tafsiri rasmi kutoka BAKITA ya tangazo au habari iliyo katika lugha ya kigeni, kushiriki katika semina za mafunzo yanayohusiana na lugha ya Kiswahili.

Alisema kwa wafasiri, wahariri, wakalimani na wataalamu wa lugha ya alama, watapaswa kujisajili katika kanzidata ya BAKITA na kupata cheti cha utambuzi, kushiriki katika semina za mafunzo yanayohusiana na lugha ya Kiswahili yaliyoandaliwa na BAKITA.

“Waratibu na waandaaji wa mikutano watapaswa kupata wafasiri, wakalimani na wataalamu wa lugha ya alama kutoka BAKITA.

Vilevile watafiti katika lugha ya Kiswahili nao watalazimika kupata kibali, wachapishaji wa vitabu kupata ithibati ya vitabu kutoka BAKITA kabla ya kuchapisha na kusambaza vitabu vyao,” alisema Mushi.

Mushi alisema wazalishaji wa bidhaa viwandani watapaswa kupata tafsiri ya lugha ya Kiswahili ya maelekezo ya matumizi ya bidhaa zao, kuwasilisha maandiko ya lugha ya Kiswahili yanayohusu bidhaa au huduma kutoka BAKITA kwa ajili ya kuhaririwa.

Kwa mujibu wa Mushi, kanuni hizo zitawahusu watumiaji wa lugha ya Kiswahili pamoja na wazalishaji wa bidhaa viwandani, wachapishaji vitabu, vyombo vya habari, wasanii wakalimani na wataalamu wa lugha za alama.

Wengine ni wamiliki na walimu wa vituo vya kufundishia Kiswahili kwa wageni, waandaaji wa matamasha, mashindano ya Kiswahili, wahariri, wataalamu wa lugha ya alama, waratibu wa waandaaji wa mikutano, watafiti katika lugha ya Kiswahili pamoja na waandishi chipukizi.

NIPASHE
 
Back
Top Bottom