Waziri Mkuu Mh. Pinda apigwa kombora

Combative

Member
Apr 19, 2014
58
103
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi, Moses Machali, amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwaomba radhi Watanzania kutokana na hatua yake ya kuyaruhusu malori makubwa kubeba mizigo mizito na kusababisha barabara zinazojengwa kwa mamilioni ya fedha za kodi za wananchi kuharibika.

Aidha, Mbunge huyo pia amesema kitendo hicho kililenga kumdhalilisha Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliyeyazua malori hayo kwa mujibu wa sheria.

Alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma juzi na Waziri Dk. Magufuli.

Mbunge huyo alisema haikuwa sahihi kwa Waziri Mkuu kutofautiana na Waziri wake kwani Dk. Magufuli alikuwa anasimamia Sheria namba 30 ya mwaka 1973 inayoanisha uzito unaopaswa kubebwa na malori na kupitisha katika barabara kuu za Tanzania.

"Uamuzi wa Waziri Mkuu wa kuyaruhusu tena malori ulikuwa ni wa kifisadi...halikuwa jambo la afya kwa Taifa na ni jambo lisilokubalika," alisisitiza Machali.

Hata hivyo, Mbunge Machali alimtaka Waziri Magufuli kutokufa moyo aendelee kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na amwambie Waziri Mkuu pia asimamie misingi ya sheria.

Alisema uamuzi huo wa Waziri Mkuu ulimfedhehesha Dk. Magufuli na kwamba hakusema kwa kuwa Pinda ni bosi wake.
Mbunge huyo alimtaka Pinda, ajisahihishe kwa hilo kwa kuwaomba radhi Watanzania ambao fedha zao ndizo zinazotengeneza barabara kutokana na kodi wanazolipa serikalini.

KAMBI YA UPINZANI
Kabla ya kuchangia jana, Felix Mkosamali juzi usiku wakati akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia alilalamikia hatua ya ya Pinda kuingilia kati mgogoro kati ya wenye malori na Waziri Magufuli.

Mkosamali ambaye ni Waziri kivuli wa Ujenzi, alisema Waziri Mkuu anapaswa kueleza kama yeye na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanamiliki malori au wanahisa kwenye kampuni mbalimbali.

"Ndiyo maana imekuwa rahisi kwake kuruhusu uzidishaji wa mizigo katika malori na kuunga mkono uharibifu wa barabara zetu zilizojengwa kwa jasho la walalahoi ili yeye na marafiki zake wazidi kuneemeka na kukubali uharibifu wa barabara kwa maslahi yao na malori yao," alisema Mkosamali.

Alisema uamuzi wa Waziri Mkuu, kuruhusu malori kuendelea kuzidisha uzito umeisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha.

Mkosamali alisema Waziri Magufuli aliwahi kunukuliwa akieleza kuwa ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya mwaka 1973 hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo yanazidisha uzito na kuharibu barabara.

Aidha, alimtaka Dk. Magufuli kusimamia kauli yake, vinginevyo ajiuzulu kwa kushindwa kusimamia kauli zake.

Oktoba mwaka jana Waziri Dk. Magufuli aliwaagiza wamiliki wa malori kulipa asilimia tano ya uzito unaozidi kwa mujibu wa kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2001, vinginevyo wasiingize magari yao barabarani.

Hata hivyo, agizo hilo lililoonekana kuzua mtafaruku mkubwa kati ya serikali na wasafirishaji hao ambapo walisimamisha shughuli zao kwa siku kadhaa na kuzua hofu ya kuanguka kwa uchumi nchini kutokana na shehena nyingi kukwama kusafirishwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na hofu hiyo, siku chache baadaye, Waziri Mkuu Pinda, alitengua agizo hilo la Waziri Magufuli kwa kutayataka malori hayo kuendelea na utaratibu wake wa zamani.

Wakati Pinda akitengua agizo la Waziri Magufuli, alisema mwaka 2006, Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba (wakati huo), aliandika waraka wenye kumbukumbu namba CKA/16/419/01Julai 19/2006 uliotoa msamaha wa tozo ya magari kwa uzito uliozidi asilimia tano ya uzito unaokubalika kisheria.

Pinda alisisitiza kwa kuwataka watendaji serikalini kuhakikisha kwamba wanawashirikisha wadau kila wanapotaka kufanya mabadiliko ya jambo fulani kwa lengo la kuepusha ghasia na migogoro isiyo ya lazima.

Wakichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, wabunge wengi waliiomba serikali kuhakikisha kwamba inatengeneza barabara za majimbo yao kwa kiwango cha lami ama kuweza kupitika msimu mzima.

Karibu kila mbunge aliyesimama kuchangia hotuba ya Waziri Magufuli, alitoa ombi hilo ikiwa ni pamoja na kumsifia (Magufuli) na watendaji wake katika wizara hiyo, kwa kile walichoeleza kuwa ni utendaji mzuri wa kazi, jambo lililoonekana kama ni kuanza kuandaa mazingira ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

KIGOLA ATAKA LAMI
Mendrad Kigola (CCM-Mufindi Kaskazini), alimuomba Waziri Magufuli kuangali kwa jicho tofauti barabara zilizoko katika jimbo lake kwa maelezo kwamba ni kitovu kikubwa cha uchumi wa nchi.

Kigola alisema licha ya barabara za Mafinga - Mtiri -Sawala na Mgogolo kutengewa Sh. milioni 800 katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, lakini pia kuna umuhimu wa barabara za Nyololo -Igowole - Mgololo zikatengewa fedha za barabara ya lami kwa kuwa ni maeneo yenye viwanda na hivyo kutowakatisha tamaa wawekezaji.

JAFO ATAKA BANDARI KAVU
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema aliitaka serikali kujenga barabara za lami kati ya Kisarawe -Maneromango na Mlandizi - Mzenga - Maneromango.

Aidha, Jafo aliishauri serikali kujenga bandari kavu Kisarawe ambayo alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Hali kadhalika, alishauri serikali kujenga barabara ya lami kutoka Kibaha Maili Moja - Kisarawe kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari jijini humo.

"Kwa kweli Mheshimiwa Magufuli anafanya kazi...ni jembe, jembe kweli," Jafo alimsifia huku akiungwa mkono na Spika wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda, aliyesema Magufuli anafanya kazi sana mpaka anakonda.

PAMBA ATAKA KIVUKO
Mbunge wa Pangani (CCM), Salehe Pamba, aliiomba serikali kununua kivuko kingine cha pili kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakazi wa jimbo lake.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, takribani nusu ya wakazi wa jimbo lake hushindwa kufikia makao makuu ya wilaya kutokana na kutokuwapo kwa kivuko cha uhakika.

FILIKUNJOMBE: MAGUFULI SI MZIGO
Deo Filikunjombe (CCM-Ludewa), aliishukuru serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kati ya Njombe na Ludewa.

Aidha, alisema Waziri Magufuli ni mtendaji mzuri na ndiyo maana hayumo katika orodha ya mawaziri mizigo na kuongeza kuwa kama wangekuwapo mawaziri watano tu wachapa kazi kama yeye, basi Tanzania ingefika mbali kimaendeleo.

"Mheshimiwa Magufuli karibu sana Ludewa ukija wananchi wa huko watakubadilisha jina na kukuita Kayombo ama Mtweve na siyo Magufuli tena kwa kuwa ni waziri wa wote," alisisitiza Filikunjombe.


SOURCE: NIPASHE
 
Hakika magufuli ni kiongozi nataman awe waziri mkuu na Sio pinda maana sioni anachofanya hapo katika position ya uwaziri mkuu zaidi ya kuwa na maamuzi legelege.
 
Unapokuwa na kiongozi kama Mh.Pinda ni hasara kwa Taifa utaona tu hata kauli mbiu zake sizizotekelezeka I.e Kilimo kwanza etc upuuzi mtupu!
 
Unapokuwa na kiongozi kama Mh.Pinda ni hasara kwa Taifa utaona tu hata kauli mbiu zake sizizotekelezeka I.e Kilimo kwanza etc upuuzi mtupu!

Hawa majasusi kuwapa uongozi wa juu ni hasara wamezoea uongo mno!!Pinda hakupaswa kuwa mwanasiasa kabisa huyu anahitaji kuongozwa na sio kuongoza.
 
Hawa majasusi kuwapa uongozi wa juu ni hasara wamezoea uongo mno!!Pinda hakupaswa kuwa mwanasiasa kabisa huyu anahitaji kuongozwa na sio kuongoza.


Sidhani kama unajua unachokisema!!!!!!!!!!
Hebu leta failure zao hapa!!!!
 
Sidhani kama unajua unachokisema!!!!!!!!!!
Hebu leta failure zao hapa!!!!

Unauliza failure kweli, hebu jiulize :-

1. 2025 Vision inatekelezeka?
2. 5 year nation plan inatekelezeka ?

3. Millenium goals zimetekelezeka?

4. Etc

Nchi haina viongozi kama wapo wachache sana!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom