RUCCI
JF-Expert Member
- Oct 6, 2011
- 1,701
- 1,714
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kufutwa mara moja umiliki wa mashamba makubwa 11 yenye ukubwa wa ekari 7,700 kwenye vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera wilayani Ngara Kagera, ambayo hayana hati na yametelekezwa.
Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumatano, Machi 16, 2016) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera katika kata ya Kasulo wilayani Ngara akiwa njiani kuelekea mkoa wa Geita.
Waziri Mkuu alilazimika kufanya mkutano huo mapema asubuhi baada ya kuamua kuitisha uongozi wa wilaya ya Ngara ufike kwenye mkutano huo ili kujibu kero za wananchi waliosimamisha msafara wake jana wakati akielekea Ngara mjini.
Uamuzi huo unafuatia hatua ya Waziri Mkuu kumwita kwenye mkutano huo Afisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Bi. Betty Munuo ili aeleze chanzo cha mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.
Bi. Munuo ambaye amehamishiwa wilaya hiyo Agosti, mwaka jana, alisema aliyakuta malalamiko hayo na amefanya uchambuzi wa majina ya wamiliki wote wa mashamba na walikuwa wanapanga kuwapatia notisi ili wajieleze.
Katika orodha yake, Bi. Munuo alitaja wamiliki 18 wa mashamba makubwa lakini kati yao ni wamiliki saba tu ambao mashamba yao yana hati lakini matatu ndiyo yameendelezwa na manne hayajaendelezwa.
Mashamba yaliyoendelezwa yanatumika kwa kilimo, ufugaji na shule. Nayo yanamilikiwa na Dayosisi ya Rulenge (shamba na. 606 lenye ekari 161 liko Mbuba); Dario Zakaria (shamba na. 639 lenye ekari 282 liko Nyakariba) na Masista wa Mt. Fransisco (shamba na. 234 lenye ekari 759 liko Kasulo).
Mashamba manne yenye hati lakini yametelekezwa ambayo yote yako kijiji cha Rwakalemera ni ya Abdallah Sadala na. 235 lenye ekari 521; Mahsen Saidi shamba na. 333 lenye ekari 458; Mshengezi Nyambele shamba na. 746 lenye ekari 388 na Mushengezi Nyambele shamba na. 745 lenye ekari 497.
Akitangaza uamuzi wake, Waziri Mkuu aliwataja wamiliki wa mashamba yasiyo na hati kuwa ni Bw. Joseph Rugumyamheto mwenye shamba na. 527 (ekari 505 liko Rwakalemera); Bw. Nicolaus Kidenke shamba halina namba na ukubwa wake haujulikani; Bw. Gwasa Angas Sababili shamba na. 714 (ekari 236 liko Kasharazi); na Bw. Makumi Adili Rufyega (ekari 500 liko Rwakalemera).
Wamiliki wengine ambao mashamba yao yapo kijiji cha Rwakalemera ni Paulo Shikiri ekari 250; Frank Mukama Derila ekari 750; Godfrey Kitanga ekari 800; Philemon Mpanju ekari 200; Issa Sama ekari 500; Hekizayo Mtalitinya ekari 225 na Joel Nkinga ekari 1,250.
Waziri Mkuu aliagiza ifanyike sensa ili kubaini kama wamiliki wa mashamba hayo yote ni Watanzania au la. "Haya yenye hati nataka yafanyike mapitio ya hati zao na kubainisha ni namna gani walipatiwa hati hizo. Nataka taarifa inifikie ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 Machi, 2016," alisema.
Ili kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu ameagiza kurejeshwa mara moja kwa aliyekuwa Afisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Mponzi ambaye amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ili aje asaidie uchunguzi wa ugawaji wa maeneo hayo.
Alimtaka Mwenyekiti wa kijiji cha Rwakalemera, Bw. Brighton Kemikimba aitishe mkutano wa kijiji kabla ya tarehe 31 Machi 2016 na abainishe mashamba yote makubwa ambayo yanazidi ekari 50. Pia afuatilie kama yana kibali cha Baraza la Madiwani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameagiza kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Bw. Colnel Ngudungi na kutaka arejeshwe wilayani humo kujibu tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha za mauzo ya mbao kutoka kwenye msitu wa Rumasi, wilayani humo.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Adam Swai ameagizwa kumwandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ili atekeleze maagizo hayo na Bw. Ngudungi arejeshwe Ngara kujibu tuhuma hizo. Bw. Ngudungi alihamishwa kwenda Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, Agosti 2015.
Akiwa njiani kuelekea Ngara jana mchana (Machi 15, 2016), waziri Mkuu alisimamishwa katika kijiji cha Rwakalemera na wananchi wenye mabango wakiomba kurejeshewa ardhi ya kijiji huku baadhi yao wakidai wanatishiwa na bunduki pindi wakisogelea mashamba hayo makubwa.
Pia walidai kuuzwa kwa msitu wa Rumasi na mapato kutojulikana yalipokwenda huku wakidai kuwa kijiji chao hakipati mapato yoyote kutokana na minada ya ng’ombe inayofayika kijijini hapo wakati sharia inataka asilimia 20 ya mapato ibakizwe kijijini.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, MACHI 16, 2016.