Waziri Mkenda: Kaya zenye Wazazi Waliosoma zina Usitawi kuliko Kaya ambazo Wazazi hawajasoma

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,802
11,961
Salaam Wakuu,

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda, amesema Takwimu zinaonyeshwa kwamba Kaya zenye Wazazi Waliosoma, zina Usitawi kuliko familia za Wazazi ambao hawajasoma. Hata Nchi zilizowekeza kwenye Elimu zina maendeleo zaidi ya Nchi ambazo hazijawekeza kwenye Elimu. Ameyasema hayo kuonesha umuhimu wa Elimu na kuwekeza kwenye elimu.

Ameyama hayo leo 09/03/2022 Mkoani Dar, wakati akielezea mafanikio ya Rais Samia ndani ya Mwaka Mmoja.

Kasema Rais Samia kawekeza sana kwenye elimu. Kwani rais Samia Kuna msukumo kauchukua yeye mwenyewe.

Baadhi ya aliyofanya ni;

i). Kaongeza bajeti na uwekezaji katika elimu. Kasema Mkupo wa UVIKO, Sekta ya elimu ilipata robo ya fedha zote zilizotolewa Tril 1.3

ii). Madarasa 15 elfu yamejengwa kwa fedha za uviko kwa muda mfupi ambapo yamewezesha Wanafunzi kwenda Shule ambapo Kila mtoto sasa anaenda Shule

ii). Hata Walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, wametafutiwa Mkakati wa kurudi shule.

iii). Elimu kwa watu wenye Matatizo Maalum, Fedha zimeongezwa wamenunua vitabu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na vitendea kazi hata Viti mwendo.

iv). Vituo Shikizi 3000 vimejengwa. Kuna watoto wanatakiwa waende shule, shule ipo mbali kwahiyo Serikali imejenga vituo karibu. watoto walipo hasa wa darasa la kwanza na la pili. Hivyo wamejengewa Vituo Shikizi.

v).Bilioni 180 zimetengwa kwaajili ya kujenga Shule 215 katika kata ambazo hazina Shule za Sekondari na Madarasa 41 kwenye vyo vya Ufundi.

vi). Rais Samia kafanikisha kujengwa kwa Vyuo vipya vya VETA 25.

vi). Mikoa ya Geita, Simiyu Njombe na Rukwa ambazo ambayo ilikuwa haina vyup vya VETA, sasa vinajengwa.

Msikilize kupitia hii link



=====

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
TAARIFA YA BAADHI YA MAFANIKIO YA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KWA KIPINDI CHA KUANZIA MACHI HADI FEBRUARI, 2022

1. KUIMARISHA UTOAJI WA ELIMUMSINGI NA SEKONDARI

a) Elimu Maalum

Katika kuboresha utoaji wa elimu maalum na kuongeza nafasi za mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, Serikali inakamilisha ujenzi wa shule jumuishi ya mfano ya Lukuledi iliyopo Masasi Mkoani Mtwara itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 620. Aidha, Serikali imewezesha uchapaji wa vitabu vya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika ngazi ya Sekondari ambapo jumla ya vitabu 9,178 kwa wanafunzi 353 wasioona na vitabu 93,366 kwa ajili ya wanafunzi 3,591 wenye uoni hafifu wa elimu ya sekondari kwa thamani ya Shilingi 707,000,000. Vilevile, Serikali imewezesha ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi 486 wenye mahitaji maalum wa Elimu ya Juu katika taasisi 11 za umma vyenye thamani ya Shilingi 770,000,000.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imenunua vishikwambi (Tablets) 330 vyenye gharama ya shilingi milioni 134 kwa ajili ya shule 15 za msingi zinazopokea wanafunzi viziwI. Pia imenunua vitimwendo 1,334 vyenye thamani ya Shilingi milioni 191 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo waliobainika kuwa na uhitaji katika shule za msingi na sekondari.

b) Kuimarisha Uthibiti Ubora wa Elimumsingi


Ubora wa elimu unaendana na uwepo wa mifumo sahihi, nguvu kazi na vitendea kazi kwa ajili ya usimamizi na uthibiti ubora wa Elimu. Katika pindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imetumia Shilingi bilioni 5.94 kununua na kusambaza magari 38 kwa ajili ya ofisi za uthibiti ubora wa shule kwa lengo la kuimarisha uthibiti wa elimu nchini. Samabamba na hilo, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 2.6 kwa kuimarisha ufuatiliaji wa ufundishaji shuleni na kuwawezesha Maafisa Uthibiti Ubora wa Shule kutoa ushauri kwa lengo la kuboresha elimu.

c) Kuongeza fursa na Ubora wa Elimu ya Sekondari

Katika kuongeza fursa na ubora wa elimu ya Sekondari, Serikali imewezesha kazi zifuatazo kufanyika hususan katika kuhakikisha Watoto wa kike wanaendelea na elimu:

i. Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule ya Mfano Dodoma yenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 1,000 wa bweni. Ujenzi utagharimu Shilingi bilioni 17 ambapo hadi sasa jumla ya Shilingi bilioni 6.8 zimetumika ambapo hadi mwezi Februari ujenzi umefikia asilimia 65;

ii. Serikali imeendelea na ujenzi wa Shule mpya 245 za Sekondari kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Sekondari hususan kwa watoto wa kike. Ujenzi huu unafanyika katika kata ambazo hazina shule za sekondari kwa lengo la kuwapunguzia umbali wa kutembea watoto wa sekondari na hivyo kuimarisha ulinzi wao waendapo na watokapo shuleni. Jumla ya Shilingi bilioni 180 zimetolewa kutekeleza azma hii ya Serikali.

d) Uimarishaji wa Elimu ya Ualimu

Katika kuimarishaji Elimu ya Ualimu Shilingi bilioni 11.20 zimetumwa mwezi Juni, 2021 katika Vyuo vya Ualimu kwa ajili ya kujenga upya Vyuo vitatu vya Sumbawanga, Dakawa na Mhonda. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita, imewezesha ujenzi wa miundombinu katika vyuo 17 vya ualimu kwa itakayogharimu Shilingi 5,440,000,000.00 kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 (TCRP). Ujenzi katika vyuo 17 unahusisha: ujenzi wa madarasa 41; Kumbi za Mihadhara 3 na mabweni 15, katika Vvyuo vya Ualimu. Vilevile, katika kuimarisha uweze wa wakufunzi katika kufundisha, Serikali imetoa mafunzo kwa Wakufunzi 572 wa Vyuo vya Ualimu wa masomo ya Michezo, Muziki Sanaa za Maonesho, Sanaa za Ufundi na Biashara kuhusu stadi mbalimbali za ufundishaji.

2. KUONGEZA FURSA NA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA ELIMU YA UFUNDI

a) Chuo cha Ufundi Dodoma

Katika kuongeza fursa za elimu ya ufundi kwa lengo la kuongeza nguvu kazi ya watu wenye ujuzi (skills) katika taifa, Serikali imeanza ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma tarehe 28 Mei, 2021. Awamu ya kwanza ikikamilika, Chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 3,000 kwa mwaka ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 18 kwa gharama ya Shilingi bilioni 17.9 ambapo hadi Mwezi Januari 2021, Serikali imekwisha kutoa Shilingi bilioni 3.92 za awali. Kazi ya ujenzi ilianza rasmi tarehe 17 Julai, 2021 na hadi kufikia mwezi Februari, 2022 ujenzi umefikia asilimia 45 na ujenzi unatarajia kukamilika tarehe 30 Desemba, 2022.

b) Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA)
Tarehe Januari 2022, Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 30.84 kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya Wilaya 25 na hivyo kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Ufundi. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 28.7 zimetolewa kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 (TCRP).

Katika kuhakikisha fursa za upatikanaji wa elimu ya ufundi inaongezeka, maeneo mengine ya mafanikio katika uimarishaji wa Eimu hiyo ni pamoja na:

i. Kuendeleza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Mikoa ambayo ilikuwa haina vyuo katika ngazi hivyo ambayo ni: Njombe, Rukwa, Geita na Simiyu ambapo Serikali imetoa Shilingi bilioni 16,830,582,822.31 mwezi Desemba 2021 na ujenzi wa vyuo hivyo tayari umeanza mwezi Januari 2022.

ii. Uwezeshaji wa utoaji wa mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Makundi Maalumu ya Vijana takribani 8,000 wa kitanzania ambapo Serikali imetoa Shilingi bilioni 1.81 kwa lengo la kuwawezesha kujengewa ujuzi na hivyo kuweza kujiajiri na kuajiriwa;

iii. Ununuzi wa vifaa vya kutolea mafunzo katika Vyuo vya VETA vya Karagwe na Chato ambapo Serikali imetoa Shilingi milioni 340. 66;

iv. Ununuzi wa magari nane (8) kwa ajili ya usimamizi wa utoaji wa mafunzo ya Ufundi Stadi nchini ambapo Serikali imetoa Shilingi bilioni 1. 26; na

v. Kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa walimu wa Elimu ya Ufundi Stadi kwa kujenga Hosteli katika chuo cha Ualimu wa Ufundi stadi Morogoro, Serikali imetoa Shilingi milioni 446,921,958.7 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli. Lengo ni kuongeza wigo wa kuandaa walimu wa ufundi stadi na kuongeza upatikanaji wao katika soko la ajira.

c) Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDC)

Pamoja na uimarishaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali ilitoa jumla ya Shilingi bilioni 3.45 kwa ajili ya ukarabati wa Vyuo 12 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ambapo ukarabati huo umekalimika na kuwezesha kila kuchukua wastani wa wanafunzi 250 na hivyo kuongeza idadi ya vijana wanaopatiwa ujuzi nchini. Aidha, Serikali mwezi Desemba imeeidhinisha matumizi ya Shilingi bilioni 6.8 kwa ajili ya ununuzi wa samani katika vyuo 34 vya maendeleo ya wanachi kwa lengo la kuimarisha ujifunzaji kwa vitendo. Fedha hizi zimetolewa kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 (TCRP).

3. KUONGEZA FURSA NA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA ELIMU YA JUU

a) Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu

Katika kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu, Serikali Mwezi Juni, 2021 imeongeza Bajeti ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka Shilingi bilioni 464 mwaka 2020/21 hadi Shilingi bilioni 570 mwaka 2021/22. Ongezeko hili la Bajeti litawezesha kuongeza wanufaika wa mkopo wa mwaka wa kwanza kutoka wanafunzi 55,287 mwaka 2020/21 hadi takribani 76,300 mwaka 2021/22 ambapo ongezeko hilo la linajumuisha wanufaika wa mwaka wa kwanza na wanaondelea na masomo ambao walikosa mikopo hapo awali. Hivyo, kuongeza jumla ya wanufaika kwa mwaka kutoka wanafunzi 142,170 mwaka 2020/21 hadi wanufunzi 176,617 kwa mwaka 2021/22.

Kuanzia tarehe 1 Julai 2021, Serikali imeondoa TOZO ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo iliyokuwa inatozwa kwa wanufaika wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Aidha, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeondoa tozo ya adhabu ya asilimia 10 ya mkopo ambayo inatozwa kwa wanufaika waliochelewa kulipa mikopo hiyo.

b) Kuboresha na Kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu
Katika kuboresha na kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu, tarehe 27 Mei 2021, Serikali imewezesha upatikanaji wa mkopo nafuu wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 425 sawa na Shilingi bilioni 972.0 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Juu na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya nchi (Higher Education for Economic Transformation). Jumla ya vyuo vikuu 14 vya umma na Taasisi zinazosimamia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia zitanufaika ambapo kazi zinazoenda kutekelezwa zinalenga kuongeza ubora na fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari watakao takiwa kijiunga na Elimu ya Juu:

Maeneo mengine ya utekelezaji wa Mradi huo wenye lengo la kuimarisha Elimu ya Juu nchini ni kuwezesha mapitio ya Mitaala ya Programu mbalimbali katika Taasisi za Elimu ya Juu na kuimarisha uratibu na usimamizi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo taasisi zifuatazo zitajengewa uwezo:

1. Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),

2. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na

3. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Vilevile, Mradi utajielekeza katika kutekeleza afua za kuongeza wigo wa ushiriki wa wanafunzi wa kike katika Elimu ya Juu hususan katika Programu za Sayansi, Teknolojia na Hesabu. Utekelezaji wa afua hizi ni maandalizi ya kupokea wanafunzi watakao kuwa ni matunda ya utekelezaji wa mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Sekondari SEQUIP.

c) Kuimarisha Mazingira Ya Kujifunzia Ya Elimu Ya Juu
Katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali ilitoa Shilingi bilioni 8.94 kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya. Fedha hizi ni utekelezaji wa ahadi ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa katika ziara yake Mkoani Mbeya tarehe 03 Mei, 2019.

Maeneo mengine ya uongezaji wa fursa na Ubora wa elimu ya Juu ni pamoja na hatua ya Serikali kuwezesha Ujenzi wa Vituo 5 vya Mikoa kwa ajili ya Chuo Kikuu Huria kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu. Vituo hivyo ni Geita, Simiyu na Manyara ambapo ujenzi umekamilika na katika vituo vya mikoa miwili (Kigoma na Lindi) ujenzi umefikia asilimia 95. Serikali imeishatoa Shilingi bilioni 1.80 kutekeleza miradi hii. Miradi hii inagharimu jumla ya Shilingi bilioni 2.08

4. MAENDELEO YA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU

Serikali imeendelea kuimarisha ubunifu na teknolojia nchini. Katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali iliandaa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanayojulikana kama (MAKISATU) yaliyohusisha wabunifu zaidi ya 700 kutoka katika makundi mbalimbali nchini. Lengo la Mashindano haya ni kuibua, kutambua ubunifu na teknolojia zilizozalishwa na vijana wa Kitanzania; kukuza hamasa ya ubunifu na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika shughuli za kiuchumi. Maonesho hayo pia yametoa fursa kwa wabunifu na wagunduzi wachanga kujitangaza mbapo, washindi 70 kila mwaka huendelezwa na Serikali.

Hadi sasa tayari bunifu 26 zilizoendelezwa na Serikali zimebiasharishwa na zinatumika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta za kilimo, maji, nishati, afya na elimu. Aidha, kwa mwaka 2021/22, Serikali imeongeza bajeti ya kuwezesha kuibua wabunifu wachanga kutoka Shilingi milioni 500 hadi Shilingi bilioni 1

UTEKELEZAJI WA MAENEO MENGINE

Sekta ya Elimu, Sayansi na teknolojia kama zilivyo sekta nyingine, katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza afua nyingine zenye kulenga kuimarisha utendaji wa Serikali katika Sekta ya Elimu kwa lengo la kuimarisha huduma ya utoaji wa elimu nchini. Kupitia Wizara ya Elimu, Serikali imewapandisha Vyeo Jumla ya Watumishi 1,724. Upandishaji wa Vyeo watumishi unategemea utaongeza ari kwa watumishi katika utoaji huduma za Wizara kwa wateja.

HITIMISHO

Serikali ya Awamu ya Sita, katika kipindi cha Mwaka mmoja iliyokaa madarakani imeendelea kutoa kipaumbele cha kipekee kwa Sekta ya Elimu. Uwekezaji mkubwa unaendelea kufanyika ili kuimarisha miundombinu ya Elimu kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu. Aidha, maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufanya mapitio ya mitaala ili kutoa wahitimu wenye ujuzi na maarifa stahiki yanaendelea kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuanza taratibu za mapitio ya Sera zinazosimamia Sekta ya Elimu pamoja na Sayansi na Teknolojia.

Wizara inaendelea kushirikiana na waajiri pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa vyuoni yanaendana na mahitaji ya soko la ajira. Hivyo, nitumie fursa hii pia kuwaomba wadau wa maendeleo ya Sekta ya Elimu kuendelea kutoa michango yao mbalimbali katika kuhakikisha tunafikia malengo ya nchi katika kutoa elimu na kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika agenda ya maendeleo ya nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania
 
Back
Top Bottom