Waziri Mkenda atoa wito kwa Wabunifu kujisajili ili kushiriki Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,801
11,961
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inaanda Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama (MAKISATU) kwa mwaka 2022. Ameyasema hayo leo 16 Februari 2022 wakati akiongea na Wanahabari.

Waziri Mkenda amesema Mwaka huu 2021/22, Wizara imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza watakaoibuliwa katika MAKISATU 2022.

Akitoa takwimu, Waziri Mkenda amesema kwamba kupitia MAKISATU 2019, 2020 na 2021, Wizara imefanikiwa kuibua na kutambua wabunifu wachanga 1,785. Kupitia wabunifu hao bunifu 466 zilikidhi vigezo, zimetambuliwa na kuhakikiwa. Aidha kati hizo bunifu mahiri 200 tayari zinaendelezwa na Serikali ili kufikia hatua ya kubiasharishwa. Aidha amesema kuwa kati ya bunifu zinazoendelezwa na Serikali, 26 zimeshafikia hatua ya kubiasharishwa, wakati 95 ziko katika hatua ya Sampuli kifani (prototype) na nyingine katika hatua za awali za kuandaa sampuli kifani.

Waziri Mkenda ametoa wito kwa wabunifu Nchini kuendelea kujisajili ili kushiriki MAKISATU 2022. Mwongozo na Fomu za maombi ya kushiriki zinapatikana katika tovuti za Wizara na Taasisi zake. Usajili wa washiriki unafanyika kupitia tovuti ya MAKISATU: MAKISATU Pia Milango ya Wizara, VETA, NACTVET, DIT na COSTECH iko wazi kwa ajili ya kutoa ushauri na maelezo juu ya usajili.

Waziri Mkenda ameongeza muda wa usajili wa Wabunifu hadi tarehe 28 Februari, 2022. Hadi kufikia jana tarehe 15 Februari 2022, Wabunifu zaidi ya 480 kwa ajili ya Mashindano walikuwa wamesajiliwa.
 
Back
Top Bottom