Waziri Lukuvi awaagiza wataalamu wa Wizara ya Ardhi kuwakabidhi mradi wa viwanja 20,000 viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,813
4,547
Waziri wa Ardhi Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewaagiza wataalamu wa wizara anayoiongoza kuwakabidhi mradi wa viwanja 20,000 viongozi wa Halimashauri ya Wilaya ya Kigamboni.

Waziri Lukuvi amesema makabidhiano hayo yafanyike wiki hii ambapo michoro yote inayohusiana na viwanja hivyo ikabidhiwe kwa uongozi wa halmashauri ya Wilaya

Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo leo Jumatano, Juni 30, 2021 bungeni alipokuwa likuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Mbagala Abdallah Chaurembo (CCM) ambaye ametaka kujua ni lini hasa taratibu za kukabidhi viwanja hivyo zitafanyika.

Akijibu swali hilo Waziri Lukuvi amesema kuanzia sasa Wilaya ya Kigamboni itakuwa na mamlaka kamili kuhusu ardhi katika viwanja hivyo na watapitia kuona nani aliendeleza au hajafanya maendelezo.

"Naagiza kuanzia leo Wizara ya ardhi ikabidhi taarifa zote kwa Wilaya ya Kigamboni ikiwemo michoro yote ya viwanja elfu 20 kwa kuwa Wilaya hiyo ina haki na mamlaka ya kamili katika kusimamia ardhi,"amesema Lukuvi.

Katika swali la msingi Chaurembo ameuliza Serikali ina mpango gani wa kuyarudisha kwenye Halmashauri maeneo yote yasiyoendelezwa na Mashirika ya Umma kwa zaidi ya miaka kumi ili halmashauri zijenge miundombinu ya huduma za jamii.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amesema haki ya kumiliki ardhi hutolewa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi.

Mabula amesema sheria hizo zimeweka masharti ya umiliki wa ardhi ikiwemo kufanya maendelezo ndani ya muda husika pamoja na hatua za kuchukua endapo kuna ukiukwaji wa masharti hayo.

"Ni kweli baadhi ya Mashirika ya Umma yaliyomilikishwa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini hayajaendeleza ardhi zao, katika kutatua changamoto hiyo, mamlaka za upangaji imekuwa ikichukua kushughulikia ardhi iliyomilikishwa na kuachwa bila kuendelezwa," amesema Mabula.

Amesema katika Mkoa wa Dar es Salaam, Wizara imeanza kwa kufanya ukaguzi wa maeneo yaliyomilikishwa kwa watu binafsi, wawekezaji wakubwa na mashirika ya umma ili kubaini ukiukwaji wa masharti ya umiliki yaliyotolewa.

Ameagiza halmashauri zote nchini kuendelea kufanya ukaguzi wa maeneo yaliyotolewa kwa mashirika ya umma, kampuni na watu binafsi na kuanzisha taratibu za kubatilisha endapo itabainika uwepo wa ukiukwaji wa masharti ya umiliki.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom