Waziri Kigwangalla Atoa Siku Saba Kwa Tanapa na Tawiri

b nyangi

Member
Apr 5, 2013
14
12
Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla ametoa siku saba kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) kushauri njia bora kutumika eneo la Kwakatende ambalo ni maarufu mapito ya Nyambu katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa uendeshaji Tanapa katika viwango vya kimataifa, mkataba huduma kwa wateja na utoaji tuzo za Utalii mwaka 2019 jana Jumatano Juni 19,2019, Waziri Kigwangalla alisema eneo hilo ni muhimu katika uhifadhi.

"Nawapa siku saba Tanapa, Tawiri na wizara ya maliasili kukaa na kunishauri njia bora ya kulihifadhi eneo hili ambalo watalii wamekuwa wakipenda kufika kwani wanashuhudia vizuri nyumbu wakivuka mto Mara," alisema

Alisema inawezekana kuongeza gharama kwa watalii wanaotaka kufika eneo hilo au kuwa na njia bora zaidi ya kulitunza eneo hilo.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Willy Chamburo alikabidhi msaada wa magari mawili kwa Tanapa kwa ajili ya kulitunza eneo hilo la Kwakatende.

"Magari mengi yamekuwa yakiharibu eneo hili sasa natoa gari lifanye kazi ya kulinda eneo hili," alisema

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Allan Kijazi alisema shirika hilo limekuwa na mafanikio makubwa katika uhifadhi na kulinda rasilimali.

Alisema wameamua kufanya kazi kwa viwango vya kimataifa na kuwa na mkataba wa huduma bora kwa wateja ili kuendelea kuboresha huduma.

Katika hafla hiyo, Kampuni za Zara Tours ilishinda tuzo ya kuingiza mapato mengi Tanapa ikifuatiliwa na Leopard Tours na Rangers Safari.

Kampuni nyingine zilizoshinda ni pamoja na KIBO Guide tours,Hoteli za Serena,hoteli na kambi za Asilia .
 
Back
Top Bottom