Waziri Kalemani aitaka TANESCO kubaini vyanzo vipya vya umeme

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
1576822443523.png

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa wanafanya tafiti kubaini vyanzo vipya vya uzalishaji umeme ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini na kuweza kufikia lengo la kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kati ya Wizara ya Nishati na Bodi/Menejimenti ya TANESCO ambapo kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga.

“Lazima tufanye tafiti kubaini vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ukiacha hivi vilivyopo, hata kama tusipotekeleza leo, vizazi vijavyo vitatekeleza miradi hiyo, mfano tafiti za mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) zilifanyika miaka mingi iliyopita, lakini mradi tunautekeleza sasa, hivyo nasi hatuna budi kuibua vyanzo vingine.” Alisema

Aidha, Dkt Kalemani aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa maeneo yote nchini yanaunganishwa na umeme wa Gridi ifikapo mwezi Juni 2022 ili wananchi wapate umeme wa uhakika na pia Serikali kuokoa fedha zinazotumika kununulia Mafuta ili kuendesha mitambo ya umeme kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini, alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ifikapo mwezi Juni mwaka 2021 na asilimia 85 ya wananchi wanapata umeme hivyo TANESCO ina jukumu la kuhakikisha kuwa lengo hilo linafanikiwa.

Vilevile, Dkt Kalemani aliiagiza TANESCO kuhakikisha kuwa, kila kiwanda au Taasisi ya umma inapojengwa, inafikishiwa umeme lengo likiwa ni kuongeza mapato ya Shirika na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.

Aidha, aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Shirika kutoka shilingi Bilioni 46 zinazokusanywa sasa kwa wiki hadi kufikia Bilioni 52 kwa Wiki.

Dkt. Kalemani aliongeza kuwa, Shirika hilo pia linapaswa kumaliza madeni yake ifikapo mwaka 2026, linaboresha nidhamu ya watumishi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha kunakuwa na mpango wa ukarabati wa miundombinu.

Chanzo: Muungwana
 
beth,
Mkoa wa Geita unahitaji budget kubwa au Special request kwa ajili ya kuwafungia au kusambaza umeme kwenye migodi ya wachimbaji wa madini ya dhahabu.

Ombi letu kwa MH Waziri, wachimbaji na wazalishaji wa dhahabu mkoa wa Geita hawana na hawajafungiwa umeme ili waweze kufanya uchimbaji wa dhahabu kwa ufanisi mkubwa ambapo wangechangia mapato ya serikali ikiwa ni pamoja na Tanesco kuongeza mapato.

Changamoto iliyopo mkoa wa Geita ni kwamba Kuna miradi ya REA, ila miradi hiyo inatekelezwa kwenda kwa wananchi ambapo madini hayachimbwi kwa wananchi kuliko na REA, matokeo yake migodi karibu yote hawana na hawapatiwi umemekwa sababu hakuna REA.

Jambo la pili, kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi gharama ni kubwa hivyo wizara inabidi isaidie kuongeza budget ya mkoa wa Geita ili mkoa uweze kutoa huduma husika kwa wakati.

Meneja wa Tanesco mkoa wa Geita anafanya kazi usiku na mchana ikiwa ni pamoja na wafanyakazi anaowaongoza, changamoto ansyoipata na kushindwa kumsaidia kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodini ni ufinyo wa budget au kukosa fedha za miradi hiyo,tunaomba awezeshwe kazi anaiweza kwa asilimia 100.

Tutashukuru iwapo kilio cha wachimbaji wa dhahabu kitasikilizwa na kupatiwa uvumbuzi wa haraka wa kupatiwa umeme ili waweze kuzalisha dhahabu kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia umeme na kurahisisha muda kwa kuongeza uzalishaji na ukizingatia soko la kisasa tunalo,sambamba na wananchi waweze kupata ajira, kuchangia Pato la Taifa na Tanesco kupata fedha za kujiendesha kwa faida.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom