Waziri Dkt. Stergomena ashiriki ufungaji zoezi ushirikiano imara Nchini Uganda

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
421
1,048
IMG-20220610-WA0077.jpg

Waziri akiwasili kwa ajili ya kuongea na wawakilishi wa Tanzania walioshiriki Zoezi la Ushirikiano Imara.

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) ameshiriki hafla ya ufungaji wa zoezi la kimedani la ‘Ushirikiano Imara’ lililofanyika Jinja Nchini Uganda lililozishirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki isipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Zoezi hilo ni moja ya jitihada za pamoja za nchi washiriki katika kujiweka tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiulinzi na kiusalama.

Zoezi limejikita katika maeneo kadhaa yakiwemo Ulinzi a Amani (Peacekeeping), kukabiliana na majanga (Disaster management), kukabiliana na uharamia (Counter piracy) na kukabiliana na ugaidi (Counter Terrorism) na mengine mengi.
IMG-20220610-WA0079.jpg

Waziri Dkt. Stergomena L. Tax akiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Rebbeca Kadaga, Naibu wa Kwanza wa Waziri Mkuu na Waziri anayehusika na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashari, na Jacob Oboth Oboth, Naibu Waziri anayehusika na masuala ya Ulinzi wa Uganda, pamoja na viongozi mbalimbali wa Afrika Mashariki waliowakilisha nchi zao katika zoezi hilo.


Mara tu baada ya kumalizika kwa hafla hiyo, Waziri alipata fursa ya kuongea na Washiriki wa zoezi hilo kutoka Tanzania ambao wanatoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vya Usalama kama vile polisi, magereza, uhamiaji, na vyombo vingine vya dola.

Katika kuongea na washiriki hao, Dkt. Tax amewapongeza kwa moyo wao wa kujituma na ari kubwa waliyoionesha muda wote wa zoezi na hatimaye kuweza kufanya vizuri.

Aidha, amewafikishia salaamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan amabye amesema kuwa Serikali inajivunia na kuthamini mchango wao katika kulitumikia Taifa ndani na nje ya nchi, jambo linaloendelea kuiletea nchi yetu sifa kubwa.

Waziri pia, amewaasa washiriki hao kuendeleza na moyo wa uzalendo katika kulitetea Taifa letu pamoja na ari waliyoionesha wakati wa zoezi na hata watakaporejea nyumbani Tanzania.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.
 
Back
Top Bottom