Waziri Biteko: Mchango wa sekta ya Madini umekua hadi kufikia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa, katika kipindi cha Mwaka Mmoja wa Rais Samia

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,807
11,969
HOTUBA YA WAZIRI WA MADINI MHE. DKT. DOTO BITEKO (MB) AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI WAKATI WA MAADHIMISHO YA MWAKA MMOJA WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA MADARAKANI TAREHE 10 MACHI, 2022 KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WIZARA YA MADINI, DODOMA

Bw. Adolf Nadunguru, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,

Dr. Abdulrahman Mwanga, Kamishna wa Madini,

Mha. Yahya Samamba, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Madini,

Bw. Augustine Olal, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Madini,

Wakurugenzi wa Sheria wa Wizara na Tume ya Madini,

Wawakilishi wa STAMICO na GST,

Watumishi wengine wa Wizara na Taasisi zake mliopo,

Wanahabari kutoka vyombo vyote vya habari mliohudhuria hapa,

Mabibi na Mabwana.

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

Ndugu Wanahabari,
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturehemu afya njema na kutuwezesha kukutana tena mahali hapa siku ya leo baada ya kukutana mara ya mwisho wakati tukizungumzia mwenendo wa Sekta ya Madini kabla na baada ya uhuru wa nchi yetu. Aidha, napenda kumshukuru kwa namna ya pekee Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoisimamia Sekta ya Madini na kutokana na maelekezo yake ya mara kwa mara ambayo yameiwezesha sekta hii kupiga hatua zaidi.

Ndugu Wanahabari,
Sote tunafahamu kwamba tarehe 19 Machi 2021, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Samia Suluhu Hassan, utatimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani. Kwetu sisi Sekta ya Madini mwaka huu umekuwa ni mwaka wa kazi na matokeo makubwa ambayo yanaendelea kuleta mageuzi ya kisekta na kiuchumi kwa nchi yetu.

Ndugu Wanahabari,
Chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka robo moja ya mwaka hadi nyingine Katika kipindi cha Januari – Septemba, 2021 wastani wa mchango wa sekta hii umekua hadi kufikia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Aidha, katika robo ya tatu (Julai – Septemba) mwaka 2021, mchango wa sekta ya madini umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.9 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 ya Pato la Taifa katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Matokeo haya yanaakisi dhamira ya Serikali kuhakikisha sekta hii inaimarika na kuweza kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyotangazwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa na Mpango wa Maendeleo.

Ndugu Wanahabari,
Kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa serikali ya awamu ya sita sekta ya madini imeweka historia kwa kushuhudia mauzo ya moja kwa moja yenye thamani ya Shilingi Trilioni 8.3 kutokana na mauzo ya madini ya aina mbalimbali. Mauzo hayo yanatokana na madini ya dhahabu, madini ya fedha, madini ya shaba, makaa ya mawe, madini ya kinywe, madini ya vito na madini ya ujenzi na viwandani. Kutokana na biashara ya madini hayo, Wizara imekusanya Shilingi Bilioni 597.53 kama maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kupitia Wizara yetu. Vile vile, ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za madini umekuwa kutoka asilimia 48 hadi asilimia 63 na hivyo kuongeza thamani ya huduma migodini kufikia thamani ya Dola za Marekani Milioni 579.3 sawa na Shilingi Trilioni 1.33 kutokana na huduma zilizotolewa migodini.

Kwa sasa Wizara imeongeza usimamizi kwenye madini ya ujenzi na viwandani ambapo tayari mifumo ya kielekronik imeanza kutumika katika usimamizi wa mapato ya Serikali yatokanayo na madini hayo. Katika juhudi za kusimamia upatikanaji wa mapato kutokana na mdini ya ujenzi na viwandani, Wizara ya Madini imeanza ushirikiano na Wizara ya TAMISEMI ili kuweza kuwafikia wananchi wanaotumia madini hayo waweze kuchangia fedha zitokanazo na shughuli za uchimbaji madini hayo kwa mujibu wa Sheria ya Madini.

Ndugu Wanahabari,
Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhesimiwa Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki kikamilifu na kwa ufanisi kwenye uzalishaji madini hapa nchini. Katika usimamizi huo, kwa sasa wachimbaji Wadogo wanachangia zaidi ya asilimia 30 kwenye mapato yatokanayo na madini. Kiasi hiki ni cha juu ikilinganishwa na kiasi kidogo (asilimia 4 kabla ya marekebisho ya Sheria) kilichokuwa kikichangiwa na kundi hili muhimu katika Sekta ya Madini. Mafanikio haya ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Tanzania katika kuhakiksha wananchi wa kipato cha chini wanashiriki kwenye shughuli za madini na kunufaika na rasilimali za madini. Mchango huu wa wachimbaji Wadogo kwenye Sekta ya Madini unatokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha huduma muhimu kwa wachimbaji kama masoko zinapatikana. Hadi sasa kuna masoko 44 na vituo vidogo vya kununulia madini ya dhahabu 70. Masoko haya na vituo vya kununulia dhahabu vimeongeza uaminifu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa biashara sasa inafanyika kwa uwazi na uaminifu zaidi.

Ndugu Wanahabari,
Uwepo wa masoko umeongeza imani kwa Taasisi za fedha katika kutoa huduma za kifedha kwa wachimbaji Wadogo.Taasisi hizo ni mabenki ya NMB Bank; CRDB Bank; NBC Bank; Stanbic Bank; Azania Bank, Ecobank; and Standard Chartered Bank. Kwa sasa mabenki ya NMB, CRDB yameanza kutoa mikopo kwa wachimbaji madini. Naomba nizipongeze benki za NMB na CRDB kwa kuonesha mfano katika ushiriki wao wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wachimbaji na wafanya biashara ya madini hapa nchini. Hii ni dalili nzuri na yakutia moyo katika maendeleo ya Sekta ya Madini na nchi yetu.

Ndugu Wanahabari,
Katika awamu hii tumeshuhudia utoaji wa leseni mbalimbali kwenye shughuli za madini ukiongezeka. Jumla ya leseni 8,172 zimetolewa, kati ya leseni hizo, leseni 5,937 ni za uchimbaji mdogo wa madini (Primary Mining Lecence), leseni 282 ni za utafutaji wa madini (Prospecting Licence); leseni 5 ni za uchimbaji wa kati wa madini (Mining Licence); leseni 2 ni za uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining Licence); leseni 49 ni za uchenjuaji wa madini (Processing Licence); leseni 2 ni za usafishaji wa madini (Refinery Licence); leseni 1,531 ni za biashara ndogo ya madini (Broker Licence) na leseni 364 kubwa za biashara ya madini (Dealer Licence) zilitolewa kwa wawekezaji na wananchi, ikilinganishwa na jumla ya leseni 6,334 zilizotolewa katika kipindi cha kuanzia Machi 2020 mpaka hadi Februari 2021.

Aidha, hadi kufikia tarehe Desemba, 2021, jumla ya Leseni zilizo hai ni kama ifuatavyo: Leseni za uchimbaji mdogo (Primary Mining Licence) ni 36,400; leseni za utafutaji (Prospecting Licence) ni 1,309; leseni za uchimbaji wa kati (Mining Licence) ni 221; leseni 17 za uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining Licence); na leseni 210 za uchenjuaji madini (Processing Licence). Vilevile kuna jumla ya leseni hai 6 za usafishaji madini (Refinery Licence); leseni 6 za uyeyushaji madini (Smelting Licence); leseni 1,649 za biashara ndogo ya madini (Broker Licence) na leseni za 618 za biashara kubwa za madini (Dealer Licence).

Ndugu Wanahabari,
Kati ya leseni zilizotolewa, takribani leseni 6 zenye uwekezaji mkubwa na kati zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji miradi hiyo. Miradi ambayo ipo tayari kuanza shughuli za uzalishaji ni mradi wa Uchimbaji dhahabu wa Shanta Singida, mgodi wa Jumbo Lindi wa Uchimbaji Madini ya Kinywe (graphite) ambayo ipo katika hatua za ujenzi wa miundo mbinu, mgodi wa Tembo Lickel ambao umepata leseni kubwa ya uchimbaji madini ya Nickel, Mgodi wa Nyanzaga ambao baada ya kusainiwa makubaliano umeshaanza shughuli za ujenzi wa mgodi. Aidha, kati ya leseni nne za Usafishaji madini (refining) tayari leseni tatu zimekamilisha ujenzi wa miundombinu ya Usafishaji ambapo Refinery ya Mwanza imeshaanza shughuli za usafishaji madini ya dhahabu baada ya Mheshimiwa Rais Kufungua mradi huo mkoani Mwanza mwezi Juni, mwaka 2021.

Ndugu Wanahabari,
Miradi iliyoingiwa makubaliano na Serikali na inayoendelea na uzalishaji itahitaji malighafi mbalimbali ikiwa ni pamoja na chokaa, magadi soda, saruji, sulphuric acid na hydrochloric acid zitakazochochea kukua na kuanzishwa kwa viwanda vya uzalishaji kemikali na kuendeleza na kufunguliwa kwa migodi mipya ya kuzalisha malighafi hizo. Manufaa mengine ni: Kukua kwa mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa; kuchochea kukua kwa Sekta nyingine za kiuchumi kama vile Viwanda, Biashara na Sekta za Kifedha; kuongezeka kwa fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini yaliyosafishwa nje ya nchi; huduma za Bima na Sheria kutokana na kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta hizo.

Ndugu Wanahabari,
Katika mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, kwa mara ya kwanza katika historia ya Sekta ya Madini, Serikali ilifanikiwa kusaini mikataba mipya minne ya uchimbaji na uanzishwaji wa migodi mikubwa na ya kati ya madini kwa wakati mmoja. Ilikuwa tarehe 13 Desemba, 2021 ambapo dunia ilishuhudia Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na yeyé mwenyewe akiwepo kwenye tukio, ikisaini mikataba ya uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani milioni 735.79, Mikataba hiyo ilihusisha uchimbaji wa madini muhimu ya viwandani yanayotokana na mchanga wa baharini, madini ya dhahabu, almasi na madini ya kinywe (Graphite).

Ndugu Wanahabari,
Kukamilika kwa mikataba hii ya ubia kati ya Serikali na Makampuni ya madini kunaifanya Serikali yetu kunufaika kwa kupitia hisa maalum (free carried interest) za asilimia 16. Mikataba hiyo iliyosainiwa na utekelezaji wake ukiendelea inahusisha kampuni ya Jacana Resources (Tanzania) Limited inayounda kampuni ya ubia ya Nyati Mineral Sands Limited; mkataba na kampuni ya Mahenge Resources Limited na Serikali unaounda kampuni ya ubia ya Nyati Graphite Corporation Limited; mkataba wa kampuni ya ubia ya Tembo Nickel Corporation kati ya Serikali na kampuni ya Kabanga Nickel; mkataba wa kampuni ya ubia ya Sotta Mining Corporation Company kati ya Serikali na Kampuni ya Nyanzaga na mkataba wa kampuni ya ubia ya Williamson Diamonds kati ya Serikali na kampuni ya Petra Diamonds; Utolewaji wa leseni mbili za uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining Licences) kwa kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited na kampuni ya Sotta Mining Corporation. Aidha, Serikali kwa sasa kupitia Wizara ya Madini ipo katika hatua ya mwisho ya ukamilishwaji wa mkataba wa ubia na utolewaji wa leseni kubwa ya uchimbaji wa madini ya Rare Earth Elements kwa Kampuni ya PR NG Resources.

Ndugu Wanahabari,
Matokeo na mafanikio hayo yanatokana na jitihada mbalimbali za Serikali ya awamu ya sita ikiwa ni pamoja na kuimarisha Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini. Katika kuimarisha taasisi hizo, Serikali imewezesha ushiriki wa taasisi katika maonesho na shughuli mbalimbali za kutangaza fursa na shughuli zinafanywa taasisi hizo kupitia Wizara ya Madini. Hivyo kupitia, Maonesho Makubwa ya Biashara ya Dubai Expo2020 Serikali kupitia STAMICO hivi karibuni imesaini mkataba wa uchorongaji kati yake na Buhemba Gold Company wenye thamani ya shilingi bilioni 11.5. Kandarasi hii inahusu kuchoronga mita 10,000 za miamba kwa teknolojia ya DD na mita 30,000 kwa teknolojia ya RC. Mkataba mwingine ni wa makubaliano ya utafiti na uendelezaji wa leseni za madini za Shirika na kampuni ya ASME ya Singapore wenye thamani ya karibu Dola za Marekeni milioni 300. Pia, hivi sasa Shirika hili linapata kandarasi kubwa za uchorongaji kwenye sekta ya madini kwa kushindana na taasisi binafsi. Tayari shirika limefanya uchorongaji katika mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) wenye thamani ya shilingi bilioni 18 na katika Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) shilingi bilioni 1.4. Aidha, STAMICO imefanya ukarabati wa mgodi wake wa chini wa makaa ya mawe Kiwira ili uweze kuendelea na uzalishaji wa makaa hayo. Aidha, katika kipindi hiki, STAMICO imefanikiwa kuanza uzalishaji mkubwa wa dhahabu katika Mgodi wa dhahabu wa Buckreef uliopo Geita; kuendeleza mradi wa kuchimba Dhahabu Buhemba kwa kutengeneza miundombinu ya mgodi, kuagiza mtambo na shughuli za uchorongaji. Pia, Shirika limeweza kutoa gawio Serikalini la jumla ya Shilingi bilioni 1.2 katika mwaka wa fedha 2020/21.

Ndugu Wanahabari,
Aidha, STAMICO imeendelea kuwa mlezi wa wachimbaji wadogo ili hatimaye waweze kukua na kuongeza tija katika kufanya shughuli zao. Katika kutekeleza hii, STAMICO imesaini mikataba na benki mbalimbali za biashara nchini kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupatiwa mikopo na kuwaunganisha na benki kadhaa, zikiwemo Benki za NMB, KCB na CRDB, hivyo wadau wote na hasusan wanawake mnahamasishwa kuzichangamkia fursa hizo.

Kwa haika, ipo tofauti kubwa sana kati ya STAMICO ya sasa na ya zamani kutokana na matokeo makubwa ambayo shirika hili linaendelea kufanya. Kupitia juhudi hizi, Shirika lilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 19.97 kati ya Machi 2021 na Februari 2022 kutoka vyanzo vyake vya ndani.

Ndugu Wanahabari,
Katika kuhakikisha kuwa Wizara inaongeza wigo wa kukusanya maduhuli ya Serikali, Serikali ya awamu ya sita ilitoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 11.28 ili kuiwezesha Tume ya Madini kufanya ununuzi wa magari pamoja na vifaa vya masoko kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini. Aidha, kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita ndicho kipindi ambacho kwa mara ya kwanza ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha kusafisha dhahabu nchini ulikamilika na kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais. Kiwanda hiki kinachojulikana kama Mwanza Precious Metals Refinery kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku katika kiwango cha kimataifa cha 999.9. (Purity) Kiwanda hiki ni cha kwanza cha aina yake kwa ukubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Aidha, mitambo ya kiwanda hiki imewekewa uwezo (Installed capacity) wa kusafisha hadi kilo 960 za dhahabu kwa siku na Dhahabu iliyosafishwa ya kiwanda hiki, kutokana na ubora wake, inaweza kununuliwa na benki kuu yoyote duniani na kuwekwa kama amana ya serikali.

Ndugu Wanahabari,
Juhudi mbalimbali zimefanyika katika awamu hii za kuwapunguzia adha za tozo zisizokuwa na tija kwa wananchi na wawekezaji katika sekta ya madini. Marekebisho yamefanyika katika Sheria ya Madini, Sura 123 kwa vipengele ambavyo vilikuwa vinaleta mkwamo katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali. Tume ya Madini sasa inatoa leseni ndogo za biashara ya madini ya ujenzi na ya viwandani ambazo zitachochea na kuhamasisha wananchi kushiki kwenye uchimbaji na biashara ya madini haya na hivyo kuongeza wigo wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia madini ujenzi na viwandani. Pia, marekebisho mengine ya kisheria yaliyofanyika ni pamoja na kuruhusu Tume ya Madini kuruhusu uingizwaji wa madini kutoka nje ya nchi kuuzwa katika masoko ya ndani bila kutozwa VAT. Awali uingizwaji wa madini nchini ulikuwa mdogo kutokana na kodi za VAT. Kwa upande mwingine, kumefanyika marekebisho ya Kanuni za Mirerani ili biashara zote za madini ya tanzanite na uongezaji thamani kufanyika Mirerani pekee ili kuitambulisha Mirerani kama kitovu cha madini ya Tanzanite duniani na kudhibiti utoroshaji wa madini hayo.

Ndugu Wanahabari,
Kwa upande wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), katika kuhakikisha inatimiza malengo yake ipasavyo, imefanikiwa kusogeza karibu na wachimbaji wadogo wa madini huduma za maabara kwa lengo la kuwasaidia wachimbe kisayansi na hivyo kuongeza tija na mapato ya serikali. Tayari Ofisi hizo zimefunguliwa katika mkoa wa Geita na lengo ni kuendelea kufungua ofisi hizi kwenye kanda zenye shughuli nyingi za uchimbaji madini. Aidha, huduma za maabara na utafiti zimeboreshwa zaidi kwa GST kupatiwa mashine mbalimbali za kisasa za uchunguzi wa madini na tafiti za jiosayansi zikiwemo Tanuru kubwa na la kisasa la uchunguzi wa sampuli za dhahabu lenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa sampuli 50 kwa mkupuo kwa muda wa saa moja ukilinganisha na uwezo wa sampuli 16 kwa mkupuo kwa muda wa saa moja kwa tanuru lililokuwepo; Mashine kubwa ya kisasa ya kuzalisha vyungu vya kuyeyushia sampuli za dhahabu (crucible); Mashine za tafiti za madini ikiwemo magnetometer ambazo zimeongeza uwezo wa GST wa kuwahudumia wadau wengi zaidi hasa wachimbaji wadogo.

Ndugu Wanahabari
Kupitia maboresho hayo, maabara ya GST imefanikiwa kuongeza wigo wa ithibati kwa njia za uchunguzi wa sampuli za madini zinazotambulika kimataifa kutoka njia moja (1) iliyokuwepo hadi tatu (3) mwaka 2022. Kupatikana kwa ithibati hizo kumeendelea kuvutia wateja wengi zaidi kuitumia maabara ya GST ambapo idadi ya sampuli zinazochunguzwa imeongezeka kutoka wastani wa sampuli 9,800 mwaka 2020/21 hadi kufikia wastani wa sampuli 15,000 mwaka 2021/22; Wachimbaji wadogo wa madini zaidi ya 2,000 katika mikoa tisa (9) ya Tanzania Bara wamejengewa uwezo katika shughuli zao za uchimbaji na uchenjuaji madini kwa lengo la kuongeza tija, pato lao na la taifa kwa ujumla.

GST imeweza kufanya utafiti na uhakiki wa taarifa za uwepo wa madini (Mineral Occurrences) katika mikoa ya Arusha, Manyara, Lindi, Mtwara na Kilimanjaro kwa lengo kuandaa ramani za uwepo wa madini katika kila Mkoa na kuboresha kanzidata ya madini na kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania.

Ndugu Wanahabari
Majukumu mengine yaliyotekelezwa na wizara katika uongozi wa Serikali ya Awamu ni pamoja na kufanyika kwa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini ulishirikisha washiriki wapatao 1,200 kutoka ndani na nje ya nchi na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao. Mkutano huu unatumika kuvutia uwekezaji, kutangaza fursa za kibiashara zilizopo katika sekta ya madini na umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu katika kuvutia uwekezaji.

Ndugu Wanahabari
Aidha, Uongozi wa Mheshimiwa Rais umetoa nafasi kwa sekta ya madini kushiriki katika maonesho na mikutano ya kimataifa ambapo wizara imeendelea kutangaza fursa za kiuwekezaji zilizopo katika sekta ya madini ambapo mara nyingi Tanzania imekuwa mfano bora kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini. Kwa lugha nyingine, kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mfano wa ushirikiano mzuri uliopo baina ya wawekezaji katika Sekta ya Madini na Serikali hasa kupitia kuwekeza kwa ubia.

Ndugu wana habari,
Kwetu sisi sekta ya madini haya ni matokeo makubwa kutokana na namna Sekta inavyojifungamanisha na sekta nyingine kiuchumi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya madini.

Ndugu Wanahabari,
Kufuatia uwekezaji inaofanywa na Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu na watu wetu kwa ujumla, niwaombe wananchi wa maeneo ya miradi hiyo na watanzania wote kwa ujumla tujenge tabia ya kutowasumbua wawekezaji kwa namna yoyote ile ikiwemo kuacha tabia inayofanywa tegesha inayofanywa na watu wachache kwenye miradi mipya inayoanzishwa.

Ndugu Wanahabari,
Kwa kumalizia naomnba niwashukuru nyinyi wenyewe kwa kuendelea kuwahabarisha wananchi mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya madini na kuwezesha wananchi wengi kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hii.
 
Masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini karibia yatafungwa maana sio kwa utoroshwaji wa madini awamu hii.... Sina takwimu official ila mark my word! Nipo zangu machimboni hapa ila ela ya bila tozo za serikali ni tamu Sana, ukiionja kamwe huwezi kuacha, SSH aongozee hadi kifo katiba kitu gani bana!!
 
Masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini karibia yatafungwa maana sio kwa utoroshwaji wa madini awamu hii.... Sina takwimu official ila mark my word! Nipo zangu machimboni hapa ila ela ya bila tozo za serikali ni tamu Sana, ukiionja kamwe huwezi kuacha, SSH aongize hadi kifo!
Ni kula kwa urefu wa kamba ako mkuu ni kutafuna haswa
 
Wakati tunafanya mageuzi kwenye sheria za madini Lisu alikuwa anaimba tutashitakiwa MIGA
Kitu rilo mbona wewe una chuki na chama hicho na watu wake, hata waboronge unaona sawa, almuradi ni WA upande uupendao.
 
Back
Top Bottom