Waziri awashauri wahitimu kujiendeleza kielimu ili kuendana na mabadiliko ya kidunia

fellali

Member
Aug 14, 2013
17
2
WAZIRI AWASHAURI WAHITIMU KUJIENDELEZA KIELIMU ILI KUENDANA NA MABADILIKO YA KIDUNIA

Na Felix Lugeiyamu (Mutagaya) (0712 246001; flugeiyamu@gmail.com)


Mh. Mathias Chikawe (mb), Waziri wa Katiba na sheria, amewashauri wahitimu wa Astashahada na Stashahada ya Sheria wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa mwaka wa masomo 2012/13 kujiendeleza kimasomo ili kuendana na mabadiliko ya kidunia yanayotokea kwa kasi kubwa sana. Akizungumza kwenye sherehe ya 13 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama iliyofanyika leo tarehe 06/12/2013 katika Ukumbi wa Nyalali Spuare Mh. Waziri amesema, ili wahitimu wakidhi kwenye soko la ajira la taifa na kimataifa ni vyema wahitimu husika wakajiendeleza kimasomo kwa ngazi za juu ili waweze kunufaika na ajira za mahakama na Wizara husika zinazotoka kila mwaka hususani kada ya mahakimu wa mahakama za mwanzo ambao wanahitajika kuwa na kigezo cha shahada ya kwanza ya sheria baada ya mabadiliko ya sheria ya kuajiri mahakimu wa mahakama za mwanzo. Wizara ya katiba na sheria kila mwaka hutoa nafasi 300 za ajira kwa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na makarani na washauri wengine wa kisheria kwenye wizara husika, vilevile mahakama hutoa nafasi 300 za ajira kila mwaka kwa ajili ya kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na mahakimu na makarani, akizungumza kama Waziri mwenye dhamana amewashauri wahitimu kuchangamkia nafasi hizo pindi zinapotangazwa.


Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilicho anzishwa chini ya sheria sura ya 405 toleo la 2002 la sheria za Tanzania kikiwa na lengo la kutoa elimu endelevu kwa watumishi na viongozi wa kada mbalimbali za Mahakama. Chuo hiki kilifunguliwa na Mh. B. Mkapa Rais (Mstaafu) wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania mnamo mwaka 2002. Tangu hapo hadi sasa Chuo kimeendelea kutoa mafunzo ya Sheria kwa ngazi za Astashahada na Stashahada.


Awali Mh. Waziri akijibu hotuba ya Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Mkuu wa Chuo, ameahidi kupatikana kwa Sh. 1.5 bilion kwa ajili ya kumalizia jengo la bweni la kiume ambalo kwasasa ujenzi wake umesimama kabla ya mwezi June, 2014. Na kuahidi kuendelea kufuatilia malipo ya luzuku kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji ambayo hivi sasa yanacheleweshwa kutoka; na hata yanayopatikana hayatoshelezi. Pia Mh. Waziri amemshauri mwenyekiti wa baraza la chuo kuandaa andiko na kuliwasilisha ofisini kwake ili kuweza kutafuta wafadhiri wa ndani na nje ya nchi watakao kubali kukifadhiri Chuo kwa ajili ya maendeleo.


Akielezea changamoto kubwa zinazokikabili Chuo mweneyekiti wa Baraza la Chuo Mh. Jaji Mstaafu John A.Mrosso alisema, kwenye mwaka wa masomo 2013/14 Chuo kilishindwa kusajili wanachuo wengi kwa sababu kadha wa kadha akizitaja kuwa ni pamoja na Ufinyu wa kumbi za Mihadhara, Kukosekana kwa vyanzo vya maji, na Udogo wa jengo la Maktaba. Naye akiwashauri wahitimu alitumia maneno ya “mhitimu wa leo asipojiendeleza kimasomo ni mjinga wa kesho”.


Naye mkuu Chuo Mh. Jaji wa Mahakama kuu F. Wambali akitoa nasaha zake kwa wahitimu alitumia maneno ya “Don’t live down to expectations. Go out there and do something remarkable” kwa maana “Usiishi kwa matazamio. Nenda jitoe ukafanye kitu chenye kuonekana”. Akitangaza idadi ya wahitimu alisema jumla ya wahitimu 896 watatunukiwa Stashahada na Astashahada ya sheria, kati ya hao wahitimu 267 ni wa stashahada. 629 ni wa Astashahada ya sheria kwa kampasi ya Lushoto na Tawi la Mwanza.
Nao wanafunzi wahitimu wakitoa maoni yao baada kutunukiwa vyeti vyao walikishauri Chuo kutoa elimu endelevu kwa maana ya Shahada ili wanafunzi wanapohitimu Chuoni hapo waenedelee hapo hapo kwa ngazi ya shahada ili kuendelea kupata misingi na maadili ya kimahakama yanayotolewa chuoni hapo. Pia wameishauri serikali kuangalia utaratibu wa mikopo ya elimu kwa ngazi za chini wa kuwasaidia wanachuo wasiojiweza ili nao waweze kupata elimu sawa na wenzao.
 
Back
Top Bottom