Waziri atumia madaraka vibaya kumlinda mtoto wa kigogo

Zanaki

JF-Expert Member
Sep 1, 2006
545
75
*Ashirikiana na mtoto wa kigogo kuvunja sheria za Uhamiaji
*Ala njama kuwakamatisha kwa rushwa maofisa Uhamiaji, afeli

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Wizara nyeti katika Serikali ya Awamu ya Nne anadaiwa kutumia madaraka yake kutoa amri zisizo halali kwa kumlinda mtoto wa kigogo na kusababisha maofisa kadhaa wa Uhamiaji kukamatwa wakisingiziwa kupokea rushwa.

Tukio hilo anadaiwa kulifanya hivi karibuni baada ya maofisa wa Uhamiaji kukamata raia 12 wa Kenya na mmoja wa Ufilipino wanaodaiwa kufanya kazi katika kiwanda cha mtoto wa kigogo huyo ambaye ni Mbunge bila kuwa na vibali vya kuwaruhusu kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ambacho kinaaminika, tukio hilo lilitokea Juni 14 mwaka huu wilayani Kinondoni ambapo raia hao wa nje walikuwa wanajihusisha na ajira katika kiwanda cha Huawei ambacho kinadaiwa kumilikiwa na mtoto wa kigogo.

"Baada ya maofisa hao kufika hapo na kuwakamata watuhumiwa hao nao walipiga simu kwa bosi wao (mtoto wa kigogo), ambaye kwa muda huo inadaiwa alikuwa na Waziri huyo, hivyo walichofanya ni kupiga simu kwa ofisa wa ngazi za juu katika Jeshi la Polisi na kutoa maelekezo na Waziri ya kukamatwa kwa maofisa hao kwa tuhuma za rushwa," kilidai chanzo hicho.

Wakati ukamataji huo ukiendelea, ghafla gari la askari Polisi lilifika mahali hapo na kuwakamata wale maofisa Uhamiaji ambao waliwapeleka moja kwa moja katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, Kinondoni, wakiwa na hao wahamiaji haramu.

Chanzo kilidai kuwa wakiwa pale na mahojiano yakiendelea, jopo la upelelezi lilibaini kuwa wale maofisa hawakuwa na hatia yoyote na wala hapakuwa na ushahidi wa rushwa, hivyo ilikuwa ni vigumu kuwalaza rumande.

"Huwezi kuamini, yule Waziri alifika kituoni hapo tena akiwa amevaa kaptula na alipofika aliwauliza wale maofisa kama wanamfahamu yeye...mimi ni Waziri wa...," kilisema chanzo chetu.

Kutokana na hali hiyo maofisa hao walibaki wanalalamika na kusema wanapoteza ari ya kufanya kazi kwani walikuwa kwenye kazi zao za kawaida, lakini Waziri kwa kumlinda mtoto wa kigogo mwenziwe alilazimika kuwasaliti wafanyakazi wake.

Wahamiaji ambao walikuwa wamekamatwa na maofisa hao ni Bw. Emmanuel Mkuro (35), Bw. David Mwinzi (34), Bw. Benjamin Gitau (28), Bw. Felix Mositeti (26), Bw. Bernard Owiti (28), Bw. Raphael Nzyuka (30) na Bw. Joseph Ntini (23).

Wengine ni Augustine Kimanzi (34), Bw. Samwel Gichiengu (33), Bw. Muteiti Kingesi (35), Bw. Justus Njogu (27) ambao ni raia wa Kenya na Bw. Rufino Martin (43) raia wa Ufilipino.

Walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Bw. John Msafiri, na kudaiwa kuwa Juni 14 mwaka huu, walikutwa wakijiingiza kwenye ajira katika kampuni ya Huawei bila vibali vya kuishi nchini.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapo walikiri kutenda makosa hayo na mahakama iliwaamuru kulipa faini ya sh. 50,000 kila mmoja na walilipa faini hiyo.

Jitihada za kuwapata wahusika katika sakata hilo zilifanyika lakini simu zilikuwa zikiita tu bila majibu yoyote huku zingine zikijibiwa kuwa mmliki wa simu hiyo hayupo.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom