Wazimbabwe: Wanahitaji msaada wetu

Sammy Sr.

Member
Oct 21, 2008
23
0
WATANZANIA tulijitolea kwa hali na mali kuwasaia ndugu zetu wa Zimbabwe wakati wa vita vya ukombozi, lakini kwa sabubu moja au nyngine hivi leo wakati wanahitaji tena msaada wetu wa hali na mali tumewasahau.

Miaka 21 baada ya uhuru Wazimbabwe walio wengi wanateseka na kudhalilika kutokana na kukosa chakula na mahitaji yao mengine ya msingi. Nchi za Magharibi zimechoshwa na uongozi uliopita lakini zinashindwa kusaidia uongozi mpya. Watu wengi duniani wanaizungumza Zimbabwe zaidi ya wanavyoisaidia. Na kinachohitaji hivi sasa kwa Wazimbabwe wanaoteseka sio maneno bali vitendo. Watanzania na umasikini tulio nao bado tuna sababu na uwezo wa kuwasaidia. Kinachokosekana ni nia na dhamira ya kufanya hivyo.

Hata kama wewe sio muumini wa dini yoyote lakini huwezi kukataa kwamba kitendo cha kumsaidia mtu yeyote yule aliye katika taabu kina raha ya aina yake. Hii ndyo raha tunayostahili kuitafuta. Lakini raha hiyo inaweza pia ikatuweka katika ngazi mpya ya utu na ubinadamu hapa Afrika. Tuliwasaidia Wazimbabwe wakati wa kupigania uhuru, leo tujipange kuwasaidia wakati wa kupambana na njaa, kiu na umasikini wa kutisha.

Hali ilivyo sasa Zimb abwe ni kwamba ingawa katika baadhi ya miji na hasa ile mikubwa vyakula vimeanza kuingia watu wengi wanaviona tu katika madirisha ya vyuo ya supermarkets. Maana hawana fedha ya kununua chakula hicho sio dola ya Kimarekani au randi ya Afrika kusini, mfukoni hawana!

Baadhi ya wazazi wameanza kuwakimbia au kuwatupa watoto wao. Hili linauma sana. Baadhi yetu tuliopitia katika hali kama hii hatustahili hata kidogo kuruhusu hili kuendelea katika miaka hii ambayo tunazungumzia Afrika moja. Afrika moja bila kusaidiana wakati wa matatizo leo ina maana gani ?

Kwa sababu ya taabu hizi familia nyingi zinavunjika na tatizo likiwa ni ukata na ufukara wa kutisha.

Matokeo yake sasa watoto wa kike wanalazimika kuwa malaya na kuuza miili yao ili wapate chakula na mahitaji yao ya msingi ndio waweze kuendelea na masomo. Walimu wameshindwa kufanya lolote juu ya hili. Na mahala kama Victoria falls sasa pamegeuka kwa mahayawani duniani kwenda kuwinda vitoto vya miaka 13 vyenye njaa na dhiki. Hivi Waafrika na hasa sisi Watanzania kweli tunalikubali hili.

Viongozi wetu wa dini wa kukosa la maana kufanya katika dunia hii wamo katika kugombana wenyewe kwa wenyewe au kugombana na serikali lakini wanashindwa kushika mafundisho ya waasisi wao ikiwa ni pamoja na kuacha ubinafsi na kuwasaidia wenye shida wanaokuzunguka.

Hili la Zimbabwe lilikuwa linahitaji Askofu au Shehe mmoja tu kusimama kwenye mimbari na Watanzania wote wangelitoa majibu ya kushangaza. Lakini inavyoelekea wana yao bora zaidi yanayowashughulisha. Au wanaogopa kuuona ukweli wa madai yao ya kujivika kofia ya kisiasa na yanayoweza kuikumba nchi yetu siku za mbele kama wasipokuwa na uwezo wa kuona mbali na mbele kuepusha hatari nyingi zinazotukabili kutokana na matamshi na misimamo yao isiyo na kiasi wala kipimo.

Watoto Zimbabwe wanashindwa kusoma kwa sababu ya njaa, wazazi wasioweza kuvumilia kuendelea kuona watoto wao wakiteseka na wao hawana uwezo wa kuwasaidia wanajiua masikini !


Kwa kuwa viongozi wetu wa kisiasa na wa dini wanaona ya kwao ni muhimu zaidi kuliko uhai na hali ya Wazimbabwe ninatoa wito kupitia JamiiForums kwa wananchi wa kawaida kuja pamoja na kuweka mikakati ya kuwasaidia Wananchi wa Zimbabwe kama tulivyowasaidia wakati wa kupigaania. uhuru. Bila kujali hali zetu, dini zetu, jinsia zetu, vyama vyetu, ukubwa au udogo wetu -----jiungeni ndugu mpate thawabu ya kuwatoa Wazimbabwe katika dhambi wanazolazimika kuzifanya ili kuishi.

Ninapendekeza Watanzania tuwe mstari wa mbele kuanzisha AFRIKA -4- ZIMBABWE SOS mfuko maalum utakaokuwa unakusanya shilingi 100 tu kwa siku toka kwa wasamaria wema Tanzania na kwingineko Afrika na duniani. Hili linaweza kufanyika vizuri zaidi kwa kuanzisha wavuti kwa shughuli hii na kisha kushirikiana na kampuni za simu za mkononi kuwaandikisha wanachama au wasamaria wema wanaotaka kuwasaidia Wazimbabwe.

Kampuni za simu za mkononi zitapokea fedha kwa niaba ya
AFRIKA -4- ZIMBABWE SOS na zikishafikia kiwango cha kununua chakula, maji, madawa na bidhaa nyingine taasisi hiyo mpya inanunua vitu na kwa kushirikiana na wasamaria wema katika sekta ya usafiri na uchukuzi vinapelekwa kwa ajili ya usambazaji mara moja. Ninatarajia kutakuwa na ofisi dada ya AFRIKA -4- ZIMBABWE SOS huko Harare na Bulawayo ili kurahisisha kazi hiyo. Kuna Wazimbabwe wengi tu wanaozungumza Kiswahili kuliko Mswahili ambao mtaweza kushirikiana nao.

Nina hakika kama kazi hii itatangazwa ipasavyo na vyombo vya habari nchi nyingine kadhaa za Kiafrika na hata za nje zitajiunga nasi ili kufanikisha vizuri zaidi jambo hili. Watu hawali siasa za nje, watu wanakula chakula, watu hawatibiwi na siasa za nje, watu wanahitaji dawa, watu hawaelimishwi na siasa za nje, wanaelimishwa na shule na walimu walioshiba na wenye nguvu ya kufanya kazi. Wakati ni huu wa kuziweka siasa za nje pembeni na sisi Watanzania wa kawaida kuonesha kuwa sio watu wa maneno tu kama walivyo watu na viongozi wengi duniani bali watu wa vitendo. Na hili kizazi kijacho cha Zimbabwe kitalikumbuka daima

Udugu wetu hautaishia tu wa kuwa wa damu, bali utakuwa wa kati ya yule aliyekuwa na njaa, akapewa chakula, aliyekuwa anaumwa, akauguzwa na kupewa dawa; aliyekuwa uchi, akapewa nguo akavaa!
 
Back
Top Bottom