Wazee Yanga `wamshukia` Musonye

JuaKali

JF-Expert Member
Nov 14, 2007
776
118
Wazee wa klabu ya Yanga, `wamemkalia kooni` Katibu Mkuu wa Baraza la soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye kwa kumtaka kuiomba radhi klabu hiyo pamoja na kulipa fidia kutokana na kauli za matusi alizozitoa kwa uongozi wa klabu hiyo.

Musonye, alitoa kauli kali dhidi ya viongozi wa klabu ya Yanga siku moja mara baada ya viongozi wa klabu hiyo kukataa timu isiende uwanjani kumenyana na Simba katika mchezo wa kumsaka mshindi wa tatu wa michuano ya Kagame, iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wanachama wote wa klabu hiyo jana, Mwenyekiti wa matawi ya Yanga, Mohamed Msumi, ambaye pia aliwawakilisha wazee hao, alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Musonye cha kuitukana na kuivunjia heshma klabu hiyo kimewakera, ambapo wameutaka uongozi wao kutoa ripoti polisi juu ya suala hilo ili Musonye akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.

Msumi, alisema kuwa pia wameutaka uongozi wao kumuandikia barua ya madai ya fidia Musonye, ambapo kama atashindwa kulipa watamburuza mahakamani ili iwe fundisho kwa viongozi wengine.

Mbali ya kumshukia Musonye, wazee hao pia wamemtaka Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Leodger Tenga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CECAFA, kuiomba radhi klabu hiyo kutokana na matusi yaliyotolewa na katibu wake pamoja na kumchukulia hatua za kinidhamu.

Msumi, alimponda Tenga na Makamu wake wa kwanza wa Rais, Crescentius Magori kuwa wamejigeuza walalamikaji, waendesha mashtaka na mahakimu, ambapo adhabu ya CECAFA waliitoa wao na kesho yake walibadilika na kuwa TFF na kutoa adhabu nyingine.

``Tenga na Magori ndio walifanya maamuzi wakiwa CECAFA na kesho yake wakajibadilisha na kufanya maamuzi wakiwa kama TFF, je ingewezekana vipi mtu awe mlalamikaji, mwendesha mashtaka na hakimu, maamuzi waliyotoa hayakuzingatia utaratibu,``alisema Msumi.

Kwa upande wa adhabu iliyopewa Yanga na CECAFA ya kutocheza michuano ya Kagame kwa miaka mitatu pamoja na ile iliyotolewa na TFF, ya kutoshiriki michuano ya kimataifa kwa miaka miwili, Msumi alisema kuwa wanazipinga adhabu hizo na watahakikisha uongozi wao unakata rufaa.

Alisema adhabu iliyotolewa na CECAFA inapingana na ibara ya 12 ya kanuni za michuano hiyo, ambayo imeweka wazi kuwa adhabu ya timu itakayoshindwa kufika uwanjani itatolewa kwenye mashindano na kupoteza haki zake zote, ambapo pia itarudishwa nyumbani mapema.

Msumi, aliongeza kuwa ni kitu cha kushangaza kwa timu yao kuadhibiwa mara mbili kwa kosa moja,ambapo CECAFA na TFF wanajua wazi kuwa walichofanya ni sawa na kuvunja haki za binadamu.

Wazee hao kwa kauli moja walisema kuwa watakuwa nyuma ya viongozi wao katika kutetea maslahi ya klabu yao, ambapo wamewataka wanachama wa klabu hiyo nchi nzima kushikamana ili kuyakosesha nafasi malengo ya watu wachache ya kutaka kurudisha makundi yasiyo na manufaa kwenye klabu hiyo.

SOURCE: Nipashe
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom