Wazee wakiri Chadema si shwari

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WAZEE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Kigoma, wametaka kurejeshwa kwa amani ndani ya chama hicho baada ya kubaini kuwa, hali kwa sasa si shwari na kusisitiza ni dhahiri jahazi la chama kwa sasa linakwenda mrama.

Hayo yamo katika tamko la wazee wa Chadema mkoani Kigoma lililosainiwa na Katibu wao, Said Kumdyanko na kutolewa jana.

Nakala ya tamko hilo imepelekwa kwa Katibu Mkuu wa Chadema- Taifa, Dk, Willibrod Slaa.

Katika tamko hilo, mbali ya kuupongeza uongozi wa Chadema kwa mafanikio katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu, umeelezea kutoridhishwa na hali ya mambo ndani ya chama wakidai kwa kiasi kikubwa inachangiwa na 'Ukanda’ na tofauti za kimtazamo baina ya viongozi na wanachama.

“Hili linasikitisha sana kwa kuwa mafanikio ya Chadema leo hii ni matunda ya mshikamano wa wanachama na wasio wanachama wa nchi nzima bila kujali eneo wala kanda wanayotoka tofauti na ilivyo sasa ambapo ubaguzi wa wazi wa kikanda na makundi hasimu unaonekana kushika kasi na kumea mizizi ndani ya maamuzi ya chama,” imeeleza sehemu ya tamko hilo.

Kutokana na kuwapo kwa mpasuko unaoashiria dalili mbaya kwa chama hicho, wazee hao wameshauri kufanyika kwa mambo manane wanayoamini yatakisaidia chama, badala ya kuzidi kukisambaratisha, likiwamo la kuutaka uongozi wa chama ngazi ya Taifa kukaa na kujadili kwa kina “ufa wa ukanda” katika kufikia uamuzi wa kichama ili kujenga imani kwa wanachama wanaotoka kanda zingine na kujenga umoja wa kitaifa ndani ya chama.

Aidha, wametaka uamuzi wote ndani ya chama ufanyike kwa kujali hoja ya walio wengi na si wachache wenye sauti. Wametaka pia makundi yote ndani ya chama yavunjwe kwa maslahi ya chama na wanachama kwa ujumla.

Wazee hao pia wameshauri kuzikubali tofauti za kimtizamo ndani ya chama na kutaka zisitafsiriwe kuwa ni uasi, bali chachu ya ujenzi wa demokrasia ya kweli ndani ya Chadema.

Pia wamewashauri viongozi wa juu wa chama hicho kuachana na maamuzi ya kibabe, fitna, kuhujumiana, makundi, ukanda visipewe nafasi kwa mustakabali wa chama katika siku za usoni.

Katika siku za hivi karibuni, umeripotiwa kuwapo kwa mpasuko ndani ya chama, huku Zitto Kabwe akitajwa kuwa mmoja wa walengwa wa kutupiwa virago kutokana na kutokwenda sambamba na 'sera’ za viongozi wengine wakuu ndani ya chama hicho.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom