WAZAZI WANAVYOWEZA KUCHANGIA KUFAILU AU KUFELI KWA WANAFUNZI

MMASSY

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
290
193
Ushiriki wa wazazi katika mchakato wa ujifunzaji wa watoto ni suala lisilo na mjadala. Matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika hapa nchini yanasisitiza kuwa wazazi wanaposhirikiana na walimu inakuwa rahisi kwa mtoto kupata mafanikio yanayotarajiwa. Ushirikiano unategemea namna wazazi wanavyowajibika kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni sambamba na kuwawekea mazingira mazuri yanayowawezesha kujifunza tangu wanapokuwa nyumbani.
Hali halisi inaonesha wazazi wengi hawajajenga desturi ya kushirikiana kwa karibu na walimu. Pamoja na kuwa na matarajio makubwa kwa mafanikio ya watoto wao, wazazi wamewaachia walimu kazi ya kuhakikisha mtoto anafaulu. Jukumu kubwa linalofahamika kwa wazazi wengi ni kutafuta nafasi ya mtoto kusoma kwenye shule inayosifika kwa kufaulisha watoto. Nafasi hiyo inapopatikana mzazi huhakikisha amefanya malipo ya ada na kumpatia mtoto vifaa kama vinavyooneshwa kwenye orodha ya mahitaji inayotolewa na shule husika. Kwa wazazi wengi, wajibu wao unaishia hapo.
Kazi kubwa inayobaki kwao, ni kusubiri mwisho wa muhula kupata matokeo mazuri ya mitihani. Matokeo hayo ndiyo yanayotumika na wazazi kutathmini kazi inayofanywa na walimu ili kufanya uamuzi wa ama kulipa kiasi cha ada kinachotakiwa kwa muhula unaofuata au kutafuta shule nyingine inayojua wajibu wake. Ingawa ni kweli mwalimu ana nafasi yake katika kumwezesha mtoto kujifunza, sehemu kubwa ya kazi inabaki kuwa ya mzazi mwenyewe. Mtazamo wa kukasimu majukumu yote kwa mwalimu ni kielelezo cha tatizo letu kama jamii kwa sababu kadhaa.
Kwanza, zoezi la mtoto kujifunza halianzii shuleni. Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza mwenye wajibu wa kuweka mazingira sisimushi nyumbani yatakayomsaidia mtoto kufyonza maarifa hatua kwa hatua. Kwa mfano, mzazi ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha mwanawe anapenda kusoma. Inapotokea mzazi hajamjengea mwanawe tabia ya kupenda kusoma, mwalimu atakayempokea mtoto huyu shuleni atakuwa na kazi ya ziada ya kufanya kufidia kazi muhimu ambayo haikufanyika nyumbani.

Lakini pia, mwalimu anayetarajiwa kufidia upungufu wa kimalezi ulioanzia nyumbani, naye kwa upande mwingine anakabiliana na changamoto nyingi ikiwamo idadi kubwa ya wanafunzi. Kinadharia, mwalimu analazimika kumfahamu kila mwanafunzi si tu kwa jina lake, lakini hata kufahamu mahitaji yake ya kibinafsi yanayomwezesha kujifunza vizuri. Idadi kubwa ya wanafunzi anayokuwa nayo mwalimu inafanya kazi hii nyeti isiwezekane. Katika mazingira kama haya, mzazi anapotambua wajibu wake na kusaidiana na mwalimu anakuwa sehemu ya suluhisho.
Mambo kadhaa yanaweza kufanyika. Mosi, ni kuweka mazingira sisimushi nyumbani yanayomkuza mtoto kiufahamu, kimwili, kimahusiano, kimaadili na kiroho. Ili hilo liwezekane, hakikisha unajenga ukaribu na mtoto tangu anapozaliwa.
Tenga muda mfupi kwa siku kuzungumza na mwanao. Mfanye akuamini na asiwe na wasiwasi na wewe. Mtoto anayewaamini wazazi wake huwa mwepesi kujiamini zaidi na hivyo hujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kujifunza kuliko mtoto ajiyejiamini. Pia, mpe vifaa vya kujifunzia vinavyomfanya afikiri. Msimulie hadithi zenye maudhui mbalimbali kumjenga kimaadili na kiroho. Kwa kufanya hivyo utakuwa umerahisisha kazi ya mwalimu shuleni.
Jambo la pili kubwa unaloweza kulifanya kama mzazi ni kumsaidia mtoto kazi za nyumbani anazopewa shuleni. Mwalimu anapompa mwanafunzi kazi za kufanya nyumbani, ana matarajio kwamba mzazi atashirikiana na mtoto kuzifanya na hivyo kumsaidia mtoto kujifunza.
Jitahidi kutenga muda jioni kumsaidia mtoto kukamilisha kazi anazorudi nazo nyumbani. Hiyo ni sehemu ya malezi. Sambamba na kumsaidia kazi za nyumbani, mwekee mazingira rafiki ya kujifunzia. Ondoa vitu vinavyoweza kuchukua uzingativu wake na mtengenezee ratiba ya kuifuata. Mtoto anayeongozwa na ratiba, ana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa.
Vile vile, fuatilia maendeleo ya mwanao shuleni. Walimu wengi wanalalamika kuwa wazazi hawajishughulishi kujua maendeleo ya watoto wao. Jione unao wajibu kamili wa kujua mwenendo wa mwanao kitaaluma na kitabia. Wapo wanafunzi wenye sura mbili. Wanapokuwa nyumbani wanaweza kuonesha tabia fulani, lakini wanapokuwa na wenzao mbali na mazingira ya nyumbani, hujifunza na kufanya mambo tofauti. Unapokuwa karibu na walimu wake, ni rahisi kupewa taarifa mwanao anapobadilika na hivyo kukuwezesha kuchukua hatua mapema.
Kwa ujumla, mafanikio ya mwanafunzi, si kazi ya mwalimu peke yake. Tunao wajibu wa kushirikiana na walimu katika kuhakikisha kwamba watoto wetu si tu wanajifunza masomo, lakini pia wanaendelea kukiishi kile tulichowafundisha katika mazingira ya nyumbani.

Jipatie kitabu chako cha NIFANYEJE ILI NIWEZE KUFAULU MITIHANI YANGU" ili upate mbinu mbalimbali za kumsaidia mwanao aweze kufaulu mitihani yake.Pia kitamsaidia kuweza kujua mbinu za kujibu na kufaulu vizuri mitihani yake.

JEROME MMASSY
Holy Hands Book Project
+255(0) 758673441
FB_IMG_1539368722487.jpg
 
Back
Top Bottom