Wazawa wanalea Ufisadi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,044
Wazawa wanalea Ufisadi

Awadhi Kimito Februari 6, 2008
Raia Mwema

JOSEPH Mihangwa ameeleza jinsi gani ufisadi unavyolelewa na dhana ya kumilikishwa uchumi. Ametoa mifano mingi ambayo baadhi nakubaliana nayo.

Hata hivyo, nalazimika kupingana naye kuhusu dhana nzima ya kuhusisha ufisadi na umilikishwaji wa uchumi kwa wageni. Nakubaliana naye kwamba, kashfa nyingi na nzito zenye gharama kwa Taifa zimekuwa zikuhusisha wenye asili ya Asia.

Sikusudii kujenga chuki kati ya jamii moja na nyingine ndani ya nchi yetu, lakini ni ukweli ulio dhahiri kwamba baadhi ya watu ndani ya kundi hilo wanahusika. Jambo ambalo linatisha si kwa sababu ya uzito wa hasara bali namna linavyoshughulikiwa. Jamii hii ya 'wageni' imekuwa ikikwepa mkono wa sheria kana kwamba katika nchi hii kuna sheria za wazawa na zile za wageni.

Haiwezekani fedha zipotee halafu mhasibu aachiwe akizurura. Kwanza atakamatwa na kuozea lupango. Lakini wale wanaokomba mamilioni wanaachwa watambe nje na kuvuruga ushahidi, ili wapate nafasi ya kuhamisha familia zao nje ya nchi. Mwisho wa yote ni mwendesha mashitaka kudai mshitakiwa hajulikani alipo.

Kinachofuata ni viongozi kuanza ziara mikoani kujiandaa na uchaguzi, uchumi kuhujumiwa si miongoni mwa ajenda zao za uchaguzi.Hoja inakufa na mwizi analea watoto wake huko aliko kwa kodi za walala hoi.

Mimi sina tatizo na kukaribisha wawekezaji,na kwa hakika nchi zote duniani zinafanya hivyo.Tatizo tulilo nalo, ni sisi Watanzania hasa wale waliopewa dhamana ya kumwaga wino katika mikataba na kusimamia sheria za nchi wanapokosa uzawa kwanza na hapo ndipo sula la uchumi linapokosa wazawa wa kulisimamia.

Labda nimkumbushe ndugu yangu Mihangwa kuwa ofisi zote za uhamiaji zina watendaji wazawa, sasa tujiulize ni vipi wageni wanakuja kusoma kozi za mwaka mmoja na baada ya hapo wanapata pasipoti za Kitanzania tena kuajiriwa katika taasisi za Serikali. Ni vipi Wasomali na Wakongo ambao hawajui hata neno 'jambo' wana pasipoti za Kitanzania tena wamejaa tele huko nje ya nchi kuliko hata hao wazawa.

Ni vipi wawekezaji wanaweza kuja na wafagizi wa ndani ili hali sheria za uwekezaji zipo wazi.Ni nani anatoa vibali hivi kama si Uhamiaji kule ambapo mkurugenzi hadi mfagiaji ni mzawa. Ni vipi mwekezaji aje awekeze na apewe msamaha wa kodi miaka mitano na kituo cha uwekezaji na kila baada ya miaka mitano anabadili jina la uwekezaji wake na anaishi bila kodi.Ni akina nani waliotunga sheria na kuzisimamia kama si wazawa?

Hakuna mahali palipojaa wazawa kama bungeni Dodoma. Hapo ndipo mambo yanayohusu mstakabali wa nchi yanapojadiliwa. Unakumbuka ni jinsi gani Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alipoomba iundwe tume kuchunguza masuala ya mikataba ya madini. Ni wazawa waheshimiwa wabunge waliomgeuzia kibao hadi wakamzuia asiingie bungeni. Kwani kulikuwa na wasiwasi gani juu ya hoja hiyo? Hapa utaona ni wazawa walikuwa wanalinda masilahi yao na yale wezi wa rasilimali zetu.

Huko huko bungeni Wilbroad Slaa akasema kuna harufu ya uozo Benki Kuu (BoT). Unakumbuka alivyokejeliwa na uongozi wa Bunge na vyama vya kisiasa vyenye dhamana ya kutunza uchumi na rasilimali zetu. Hatimaye suala likatoka pale bungeni na kuongelewa mitaani. Wazawa halisi wakawa na manun'guniko ndipo ikalazimu Kamati iundwe na ukweli umejulikana.

Kwa mantiki hiyo, uozo ule uliwahusisha mafisadi na wazawa. Haiwezekani shilingi bilioni 133 zitoke katika uchumi wa nchi bila viongozi wakuu wa Serikali kujua nini kinaendelea. Hata pale wanapoombwa kujibu tuhuma wamekaa kimya kama vile hakuna kilichotokea. Siku zote hakuna shoka linalokata bila kuwa na mpini. Mafisadi wawe wa Kizungu, Kihindi au Kiarabu wana mkono wa wazawa ambao wamedharau zamana walizopewa na kiburi kimewajaa.

Tujiulize kama kiongozi anaweza kusaini cheki ya mabilioni bila kujua zinakwenda wapi, hapa tatizo ni nini, mgeni anayetaka kuiba au mzawa alisiyejua kusimamia sheria na kanuni za utoaji fedha? Tuelewa pia kuwa uzawa hauishii kwa viongozi tu, hata umma wa kawaida ndio chanzo kingine cha ufisadi. Pale tunaponunuliwa fulana na kofia ili tuwapigie kura hawa viongozi, hapo ndipo mwanzo wa kudhalilisha uzawa wetu, na ndio mwanzo wa kuwapa mwanya viongozi mafisadi kushamiri.

Kabla hatujamiliki uchumi ni lazima kwanza tuheshimu sheria za nchi.Hakuna mkato katika hili. Kama sheria hazifuatwi hata hao wazawa wakimilikishwa uchumi ni kazi bure, kwani wao ndio 'wachonga misheni'. Ukiwakabidhi uchumi ni sawa na kumkabidhi bunduki mtu asiyeweza kuitunza.

Lakini mimi nadhani si vema tukalaumu kuwa wazawa hawakuwezeshwa kiuchumi. Dhana hii inatakiwa iangaliwe kwa undani zaidi. Pale Mwalimu Julius Nyerere alipochukua viwanda na taasisi na kuzifanya mali ya umma,watu waliopewa dhamana ya kuzitunza ni wazawa. Hapa tukawa na mameneja wazawa. Nina hakika hili lilifanyika makusudi ili kuwawezesha wazawa kujifunza namna ya kuendesha shughuli za kiuchuimi.

Lakini tujiulize viko wapi viwanda vya Bora, Tanganyika Packers, viwanda vya nguo na baiskeli. Vyote vimekufa kwa sababu wazawa waliopewa dhamana ya kuviendeleza wamekula mitaji. Hawakujali sheria za nchi na za uendeshaji.

Leo tunaoana kile kilichotushinda akapewa mgeni kinatoa faida na kuongeza pato la Taifa. Sasa sijui tatizo ni wageni dhidi ya uzawa au ni uzawa usioweza kujisimamia.

Tatizo si uchumi wala uzawa, bali ni udhaifu wa wazawa waliopewa dhamana na Watanzania kusimamia uchumi na rasilimali zao, kutofuata sheria, kuoneana haya na kulindana. Katika hali kama hii yeyote yule ajae hapa nchini atapata mwanya wa kuiba kila atakacho.

Kama hatutakuwa wachungu wa kulinda sheria na kuzisimamia hata wazawa wakipewa na kuwezeshwa namna gani uchumi utazidi kuporomoka.

Ufisadi ni matokeo ya uzembe wa kusimamia sheria na taratibu. Ni matokeo ya kulindana na kuoneana haya. Kama hatuwezi kusimamia sheria hatuwezi kusimamia uchumi hata kama ni wazawa kwa maana ya kuwa uchumi ni jambo linaloendeshwa kwa sheria kanuni na taratibu.Kabla hatujawawezesha wazawa kiuchumi ni lazima tuwajengee dhana ya uzawa ambayo misingi yake mikuu ni uchungu wa nchi, halafu tuwamilikishe sheria ili wakabiliane na mafisadi baada ya hapo tuwamilikishe uchumi. 
Bubu,

Saa ingine nasema may be tunahitaji 'Wachina' wakodishiwe kuendesha nchi yetu kwa miaka 10 tu- potelea mbali tuwalipe ili kurudisha discpline ya kazi, uadilifu na kujali sheria!

Sijui kama hii ngozi yetu ina laana!
 
Bubu,

Saa ingine nasema may be tunahitaji 'Wachina' wakodishiwe kuendesha nchi yetu kwa miaka 10 tu- potelea mbali tuwalipe ili kurudisha discpline ya kazi, uadilifu na kujali sheria!

Sijui kama hii ngozi yetu ina laana!

We acha tu ndugu yangu, hawa watu wanatutia uchungu wa hali juu kwa jinsi wanavyoiangamiza nchi yetu hawafai hata kuitwa viongozi bali tuwaite wafujaji na mafisadi wanaoingamiza Tanzania.
 
Hata ma MODS nao ni wazawa wa hapa, ni mafisadi. Wajiuzulu. Hawa wanaangamiza Forum na Demokrasia yake.
 
Back
Top Bottom