Wazanzibari wasifukuzwe kwenye mwungano lakini wakitaka kutoka wasizuiwe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wazanzibari wasifukuzwe kwenye mwungano lakini wakitaka kutoka wasizuiwe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Bams, Jul 22, 2012.

 1. Bams

  Bams JF-Expert Member

  #1
  Jul 22, 2012
  Joined: Oct 19, 2010
  Messages: 3,607
  Likes Received: 2,992
  Trophy Points: 280
  Mwungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanywa kwa kuamini kuwa tukiwa pamoja kila upande utanufaika. Manufaa makubwa yaliyotarajiwa ni manufaa ya kiusalama na ya kiuchumi. Mwungano wetu haukufanywa kwa sababu tu mataifa mengine yanaungana au kwa sababu tu tunataka tuwe na eneo kubwa la nchi au kwa nia tu ya kuutangazia ulimwengu kuwa na sisi tumeweza kuungana. Kwa kulifahamu hilo, ndiyo maana Mzee Karume alitamka kuwa, 'Mwungano ni kama koti, likikubana unalivua'. Kwa maneno ya Mzee Karume, uwepo na kuendelea kwa Mwungano kati ya Zanzibar na Tanganyika ulitegemea zaidi upatikananji wa manufaa yaliyotegemewa na pande zote mbili.

  Mwungano wa Zanzibar na Tanganyika haukuanzishwa kwaajili ya kujenga manung'uniko kwa upande wowote ule wa Mwungano, haukuanzishwa kuleta chuki, kejeli, au kuwafukarisha watu wake. Kuwepo kwa Mwungano kulikusudiwa kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali na taasisi zake, kuongeza ufanisi wa serikali na taasis zake na wala siyo kuongeza gharama au kufanya mambo yawe holela.

  Jambo lililo muhimu siyo kuwa na Mwungano bali ni faida na manufaa tuyapatayo kutokana na Mwungano wetu. Lazima tuangalie ni kwa namna gani mwungano wetu umetufanya tusonge mbele haraka zaidi kiuchumi na kitekinolojia, namna gani Mwungano wetu umetusaidia kiusalama na namna gani Mwungano wetu umetufanya kuwa wamoja zaidi kama watu wa Taifa moja.

  Sina uhakika sana kwenye manufaa ya kiuchumi, kitekinolojia na kiusalama lakini kwa sasa lililo wazi zaidi ni umoja wetu kati ya Watanganyika na Wazanzibari kama watu wa Taifa moja. Katika upande huu, ukisikiliza mitaani, bungeni na kwenye mijadala ya baraza la WawakilishiiMwungano unazungumzwa kama adui mmojawapo wa maendeleo, hasa kwa upande wa Zanzibar. Leo hii ni rahisi kuisikia Kenya au Uganda ikizungumzwa vizuri zaidi na Wazanzibari kuliko inavyozungumzwa Tanzania Bara (Tanganyika), yaani jirani anaonekana ni mwema na mzuri zaidi kuliko mwanafamilia. Na katika hili, ni sawa na kuwa na ndugu wanaoishi pamoja lakini kila siku ni ugomvi, badala ya kutumia muda mwingi kujadili na kupanga mikakati ya maendeleo, wanajikuta muda mwingi wanahangaika kujadili na kutafuta suluhu ya ugomvi wao. Mkifikia kwenye hali hiyo, ni aheri kila mmoja akaishi kwenye nyumba yake, akakifanya kilicho chema, mkakutana kwa wakati fulani fulani. Kwa kufanya hivyo ugomvi wenu utapungua, muda wa kufanya kazi utaongezeka, chuki zitapungua na hamu na tamaa ya kuonana na ndugu yako itaongezeka.

  Tanganyika na Zanzibar wamekwishakuwa kama wanafamilia ambao kila siku wana chokochoko. Kamati lukuki zimekwishaundwa kwa wakati mbalimbali, zote zikitumia rasilimali kubwa, kujadili kero za Mwungano, na siyo kujadili miradi mikubwa ya kimaendeleo ya pamoja.

  Dunia ya leo, ambapo demokrasia inasisitizwa kila mahali Duniani, huwezi kuwa na Mwungano wa Mataifa mawili kwa kulazimisha. Ukilazimisha utazidi kujenga chuki, na mtatumia muda na rasilimali nyingi kuushikilia Mwungano lakini mwisho wa yote, kama walioungana, mmojawapo haoni faida, kuna siku utakufa tu. Na mwungano ukifa baada ya kulazimishwa kwa miaka mingi, na hasa kwa kutumia nguvu, mataifa hayo mawili yana uwezekano wa kuwa maadui. Cha kujiuliza, ni aheri nini, kuishi na ndugu yako ndani ya nyumba moja, mkisimamiwa na sheria moja lakini kila siku mnagombana au kumwacha nduguyo awe na nyumba yake lakini akaendelea kuwa ndugu yako na jirani yako mwema?

  Tuliungana kwa amani kama tunaona kuna haja ya kutengana, basi vile vile tutengane kwa amani. Wazanzibari na Watanganyika wapewe uhuru wa kujadili na kuamua juu ya nini wanachotaka na ikionekana mahitaji ya pande mbili yanashabihiana, basi kile wakitakacho pande zote mbili ndiyo kifanyike. Hiyo itatupa muda mzuri zaidi wa kushughulika mipango ya maendeleo kwa pande zote mbili kuliko kila mara kushughulikia kero za Mwungano ambazo siku zote ni kudaiana, kwa kudhania kuwa upande mmoja unapata zaidi.
   
Loading...