Wawakilishi Zanzibar Waichachafya Kamati Ya Mzee Mwinyi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wawakilishi Zanzibar Waichachafya Kamati Ya Mzee Mwinyi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Junius, Oct 19, 2009.

 1. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #1
  Oct 19, 2009
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  Salma Said, Zanzibar

  KAMATI ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambayo imeundwa kuchunguza mwenendo wa vikao vya Baraza la Wawakilishi na mpasuko katika bunge, imeanza vibaya baada ya wawakilishi kugomea kuhojiwa kwa faragha na kutaka wahojiwe kwa pamoja.

  Kamati hiyo iliundwa mjini Dodoma baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ambacho kilielezwa kuwa kilitawaliwa na wajumbe kurushiana maneno makali, baada ya kundi moja kusimama kidete kutaka kumvua spika wa Bunge, Samuel Sitta uanachama wa chama hicho kwa madai kuwa amekuwa akiruhusu mijadala inayokichafua chama na serikali.

  Pia visiwani Zanzibar kumekuwa na matamshi yanayoashiria kutikisika kwa mshikamano ndani ya chama hicho tawala kutokana na baadhi ya wawakilishi kukomalia masuala ambayo yanaonekana kuyumbisha Muungano, kitu ambacho ni kinyume na sera ya CCM.

  Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa wawakilishi hao jana walikataa kuhojiwa kila mmoja peke yake kwa madai kuwa walishapewa taarifa kuwa kamati hiyo ingewahoji kwa pamoja.

  "Tumegoma kuhojiwa mmoja mmoja; kwa nini watufanyie hivyo? Kama wanataka kutuhoji au kuchukua maoni yetu, basi ni vyema watuhoji tukiwa pamoja kwa sababu tabia ya kumwita mtu mmoja mmoja inaleta fitina," alisema mmoja wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

  "Inaweza kusababisha tofauti kubwa kati yetu maana kwa wale waoga lazima watatetereka. Watapofika huko ndani, wataanza kubabaika na ndio maana tukaamua tuwepo sote kama ni kutusulubu basi iwe kwa wote."

  Kamati hiyo iliwasili juzi visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuwahoji wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na baadhi ya viongozi wa serikali kutokana na kauli kali zilizojitokeza dhidi ya viongozi wa Serikali ya Muungano, hasa baada ya kuelezwa kuwa Zanzibar si nchi na uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutaka suala la mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.

  Habari hizo zinadai kuwa wawakilishi hao walielezwa sababu za kamati hiyo kuja Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kupata maoni yao baada ya kutokea maneno mazito na mpasuko, huku ikiweka bayana kuwa haikwenda kumuhukumu mtu yeyote.

  Habari zinaeleza kuwa kamati hiyo ilifanikiwa kuongea na wawakilishi wote kwa pamoja, lakini ilipobaini kuwa majibu yanafanana ilitaka kuzungumza kwa faragha na mjumbe mmoja mmoja na ndipo walipogoma kufanya hivyo.

  Habari zilizopatikana juzi zinaeleza kwamba kamati ya uongozi ya Baraza la Wawakilishi ilianza kikao chake majira ya saa 4:00 asubuhi na kuendelea hadi sasa 12:00 jioni kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, Kisiwandui.

  Habari zinawataja waliohudhuria kikao hicho kuwa ni pamoja na wajumbe wa kamati hiyo ya uchunguzi, ambao ni Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, makamu mweyekiti wa CCM, Pius Msekwa na aliyekuwa spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana huku Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, ambaye ni msimamizi wa shughuli za serikali bungeni, akiongoza wawakilishi.

  Baadhi ya mawaziri ambao habari zinasema walisimama na kuzungumza katika kikao hicho ni pamoja na Mansour Yusuf Himid, ambaye ni Waziri wa Maji, Nishati na Ardhi. Mansour ndiye aliyetoa kauli mwishoni mwa wiki kuwa msimamo wa SMZ ni kuondoa suala la mafuta na gesi asilia kwenye mambo ya Muungano.

  Pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mawasiliano na Uchukuzi), Machano Othman Said alisimama kuzungumza kwenye kikao hicho hali kadhalika Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Mwinyihaji Makame Mwadini na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma.

  Habari zinasema kuwa wazungumzaji wengi kwenye kikao hicho walionekana kusimama kidete na kutetea uamuzi wao wa kutaka suala la mafuta na gesi asilia libakie katika mamlaka ya Zanzibar na pia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.

  Habari zinasema kuwa wazungumzaji wengi walidai kwamba Zanzibar imekuwa ikionewa kutokana na kutokuwa na fursa katika maamuzi yake, hasa katika suala la uchumi ambako imekuwa haipewi nafasi na Bara.

  Katika madai yao wazungumzaji wengi walisema pia kuwa kamwe hawawezi kurudi nyuma katika kusimamia kile wanachokiamini na wanataka kuwa wawazi katika kuitetea Zanzibar kiuchumi na kiutamaduni.

  Wajumbe hao mbali ya kuwa ni vinara wa kuzungumza bila ya hofu, lakini pia wamewatoa woga wajumbe wenzao ambao walikuwa na hofu kuinua mikono na kutaka kutoa maoni yao.

  Imeelezwa kuwa wajumbe walitumia muda mwingi kutoa maoni yao, wakiwemo waliochukua zaidi ya saa moja kujieleza, lakini hakuna aliyeonekana kuchoshwa na uendeshaji wa kikao na kutaka kuondoka.

  Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na mawaziri wote walihudhuria kikao hicho pamoja na wakuu wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba, isipokuwa wale waliokuwa na dharura kama Waziri wa Mwasiliano na Uchukuzi, Adam Mwakanjuki ambaye amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na Mwanasheria Mkuu Idi Pandu Hassan ambaye pia ni mgonjwa.

  Awali kamati hiyo ilikutana na uongozi wa Baraza la Wawakilishi ulioongozwa na Spika Pandu Ameir Kificho pamoja na mwenyekiti wa wajumbe wa CCM kwenye baraza hilo, Haji Omar Kheri.

  Baadhi ya kauli ambazo zinaonekana ni chanzo cha kuundwa kwa kamati hiyo ni suala zima la mafuta na gesi asilia ambalo lilizua mjadala mkali kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi.


  SOURCE: MWANANCHI
   
 2. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #2
  Oct 19, 2009
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  Hapa patamu hasa...enhee...awamu ya pili!
   
 3. K

  K4jolly JF-Expert Member

  #3
  Oct 19, 2009
  Joined: May 21, 2009
  Messages: 366
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nadhani Dodoma ndo kutakuwa kutamu zaidi kwani pale inahusu mafisadi kuondoka ndani ya chama kwa upande wa Bara.
   
Loading...