Waumini wa FGBF wampa zawadi ya nyumba Askofu Kakobe na Mkewe

Elisha Sarikiel

Verified Member
Aug 29, 2020
648
1,000
MAASKOFU, WACHUNGAJI NA WASHIRIKA WA MAKANISA YA FGBF KOTE NCHINI TANZANIA WAMPA ASKOFU MKUU ZACHARY KAKOBE ZAWADI YA NYUMBA WALIYOMJENGEA

Nyumba ya kawaida inayoonekana katika PICHA MBILI ZA KWANZA, ni nyumba binafsi ya pekee, ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe; ambayo amekuwa akiishi yeye na familia yake, kwa takriban miaka 35, tangu alipoijenga, mwaka 1986, miaka mitatu kabla ya kuliasisi Kanisa la FGBF, alilolianzisha tarehe 30.4.1989. Hata hivyo, maisha ya Askofu huyo katika nyumba hiyo, yamehitimishwa siku chache zilizopita. KULIKONI? Tufuatane pamoja katika taarifa ifuatayo:

Maaskofu, Wachungaji na Washirika wa Makanisa zaidi ya 1,000 ya FGBF, yaliyosambaa katika miji na vijiji mbalimbali katika wilaya zote Tanzania Bara; siku ya Jumapili, tarehe 25.10.2020, katika hafla maalum iliyofana sana, iliyofanyika katika Ibada Kuu ya Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, lililoko Barabara ya Sam Nujoma; waliwakabidhi Askofu Mkuu Zachary Kakobe na mkewe, Mchungaji Hellen Kakobe, zawadi ya nyumba nzuri yenye viwango vya juu vinavyolingana na hadhi yao kubwa katika jamii, waliyowajengea, na kuweka pia ndani ya nyumba hiyo, fenicha zote za ndani; ili kuwaenzi kwa utumishi wao uliotukuka, wa zaidi ya miaka 30 tangu walipoliasisi Kanisa la FGBF, mwaka 1989. Watumishi hao wa Mungu, wamekabidhiwa nyumba hiyo waliyojengewa; ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa asilimia 100% BILA KUWA NA DENI LOLOTE KWA YEYOTE, NA POPOTE PALE.

Uratibu wa maandalizi yote ya awali, ikiwemo ukusanyaji wa michango, na usimamizi wa masuala yote ya ujenzi wa nyumba hiyo, uliochukua jumla ya miaka 12, hususan kuanzia mwaka 2008, ulifanywa na makundi mawili yaliyoshirikiana kwa karibu, yaliyojulikana kwa jina, "FGBF GROUP OF DEVOTED MEMBERS".

Kundi la kwanza, liliwajumuisha Maaskofu wote wa Majimbo, Wachungaji wote, na Washirika wote wa Makanisa yote ya FGBF mikoa yote nchini, kasoro FGBF DAR-ES-SALAAM; wenye mzigo na waliojitoa kwa hiari na kupenda, na kwa moyo wa ukunjufu, waliokusudia mioyoni mwao kuona ndoto yao ya kumjengea nyumba Baba Askofu Mkuu, ikitimia.

Kamati ya Ujenzi ya Kundi hili la kwanza, iliongozwa na Mwenyekiti wake, Askofu Nathan Meshack, ambaye pia ndiye Katibu Mkuu wa Kanisa la FGBF, na Askofu wa Jimbo la Iringa. Mwenyekiti huyu, alisaidiwa kwa karibu na Askofu wa Jimbo la Kigoma, Askofu Leonard Mshana; ambaye ndiye aliyekuwa Mratibu wa Kamati ya Ujenzi ya kundi hili.

Kundi la pili liliwajumuisha washirika wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, pia wenye mzigo, waliojitoa kwa hiari na kupenda, na kwa moyo wa ukunjufu, waliodhamiria mioyoni mwao kuona kwamba, ndoto yao ya kumjengea nyumba Baba Askofu Mkuu, ikitimia. Kamati ya Ujenzi ya Kundi hili la pili, ilikuwa na jumla ya wajumbe 26, walioongozwa na Mwenyekiti, Mariam Mwaffisi.

Wajumbe wengine wa Kamati hii, walikuwa hawa wafuatao: Abduel Elinaza, Amos Mhando, Christa Mwambeleko, Cresencia Tarimo, Dayness Minja, Deborah Runyoro, Demetria Ngilwa, Dorcas Mgoye, Emina Kishimbo, Edna Mville, Francisco Mligo, Hannah Salum, Hezekia Mtera, Jane Nico, Julia Mpokera, Juliana Mlalasi, Juliet Kiwelu, Mercy Kanyosa, Miriam Majamba, Naomi Makamba, Rachel Mawole, Reuben Mlalasi, Samuel Kiwelu, Susan Shiyo, na Zawadieli Mpokera.

Katika hafla hiyo, Kundi la Kwanza lililowajumuisha Maaskofu wote wa Majimbo, Wachungaji wote, na Washirika wa Makanisa ya FGBF nchini kote, liliwakilishwa na Watumishi wa Mungu 23 wafuatao: Askofu wa Jimbo la Iringa, Askofu Nathan Meshack; Askofu wa Jimbo la Kagera, Askofu Jacob Magesa; Askofu wa Jimbo la Tanga, Askofu George Swenya; Askofu wa Jimbo la Kigoma, Askofu Leonard Mshana; Askofu wa Jimbo la Mbeya, Askofu Jermina Mwaijande; Askofu wa Jimbo la Ruvuma, Askofu Wilson Mwampote; Askofu wa Jimbo la Dodoma, Askofu Michael Mduma; Askofu wa Jimbo la Pwani, Askofu Mtemi Mathias; Mchungaji Enighenja Sakuye (FGBF Babati); Mchungaji Vedasto Hinjuson (FGBF Mto wa Mbu); Mchungaji Charles Masagati (FGBF Ngerengere); Mchungaji Calistus Mahombo (FGBF Lushoto); Mchungaji Reuben Mlay (FGBF Kijiji cha Kabuku, Handeni); Mchungaji Castory Munuo (FGBF Tukuyu); Mchungaji Magnus Pilla (FGBF Kijiji cha Mang'ola Barazani, Karatu); Mchungaji Dorah Kirumbi (FGBF Kijiji cha Soga, Kibaha Vijijini); Mchungaji William Matonya (FGBF Kijiji cha Haneti, wilaya ya Chamwino); Mchungaji Athanas Chillinga (FGBF Kijiji cha Matemanga, Tunduru); Mchungaji Sylvester Kaisi (FGBF Kijiji cha Mvuha, Morogoro Vijijini); Mchungaji Alfred Kihindo (FGBF Kijiji cha Makoga, Wilaya ya Wanging'ombe); Mchungaji Eliya Kamwela (FGBF Vwawa, Mbozi); na Mchungaji Japhet Bagomwa (FGBF Same).

Katika risala yake kwa Askofu Mkuu Kakobe, aliyoisoma katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Kundi la kwanza, Askofu Nathan Meshack, alianza kwa kusema, "Ninaifahamu kwa miaka mingi, nyumba yako ndogo ya kawaida sana, uliyoijenga mwaka 1986, miaka mitatu kabla ya kuanzishwa kwa Kanisa hili la FGBF, uliloliasisi mwaka 1989.

Ninakumbuka pia, jinsi ambavyo, kwa miaka mingi, ulivyokataa katakata kujengewa nyumba nyingine; pamoja na jinsi Watumishi wa Mungu wengi, na Washirika wengi wa Makanisa yetu ya FGBF kote nchini, tulivyokuwa tukikusihi mara nyingi, ukubali kujengewa nyumba nyingine inayolingana na hadhi yako Kitaifa, na Kimataifa.

Siwezi kusahau pia, yale yaliyojiri mwaka 2008, katika Kongamano la Maaskofu na Wachungaji wote wa Kanisa hili, lililofanyika huko Dodoma, tulipokueleza kwa uchungu mkubwa, jinsi tulivyokuwa tukijisikia kufedheheka sana mbele ya watu walio ndani na nje ya Kanisa hili, kutokana na wewe Baba yetu uliyetuzaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili, na kutupandia vitu vingi vya rohoni; kuendelea kuishi katika nyumba hiyo duni, isiyo na hadhi ya kuwakaribisha wageni wako wa ngazi ya juu Kitaifa, na Kimataifa, waliokuwa wakitamani kukutembelea nyumbani kwako".

"Tukakueleza pia jinsi washirika wengi wa Makanisa yetu ya FGBF, tunayoyaongoza nchini kote, walivyokuwa wakitusumbua sana, wakitamani kupata kibali kutoa michango yao, na kukujengea nyumba nzuri, wewe baba yetu Askofu Mkuu, tunayejionea fahari, kuwa chini ya mafundisho yako na maongozi yako, na jinsi baadhi ya washirika tunaowaongoza, walivyokuwa wakiona aibu kushuhudia hadharani, jinsi walivyobarikiwa kuwa na nyumba zaidi ya moja, zilizo nzuri kwa mbali sana kuliko nyumba yako duni, ingawa Mungu amekutumia wewe Mtumishi wake, kuwabariki na kuwa vile walivyo; na kwa sababu hiyo, walitamani sana kukushirikisha wewe Mkufunzi wetu, katika mema yote, sawasawa na WAGALATIA 6:6. Siwezi kusahau hata kidogo yaliyojiri baada ya maelezo hayo ya kina. Pamoja na kujieleza kwa kina hivyo, bado ulionekana kuwaza tu juu ya kazi nyingine za Mungu; na hali hiyo sasa, ikatufanya baadhi yetu, kukosa namna nyingine ya kufanya, bali kukushurutisha kutupa kibali kukujengea nyumba, kama alivyofanya yule Mshunami katika 2 WAFALME 4:8-11; hali iliyokufanya hatimaye, kutukubalia matakwa yetu. Tulivyopata tu kibali chako, tukajipanga harakaharaka na kwenda kuwashirikisha washirika wa Makanisa tunayoyaongoza, na washirika wengi wakapokea kibali hicho, kwa furaha isiyoelezeka, na kuanza michango mara moja. Hatua kwa hatua, hatimaye tukaweza kununua kiwanja na kuanza kujenga."

"Kufanya hadithi iwe fupi, ndoto yetu ya miaka 12, hususan tangu 2008, sasa imetimia, kwa kuwa ujenzi wa nyumba hiyo, sasa umekamilika kwa asilimia 100%, na tayari tumeweka pia fenicha zote za ndani ya nyumba hiyo. Kazi hii imechukua miaka mingi kukamilika, kwa sababu, tulidhamiria siyo tu kujenga nyumba ilimradi tu ni nyumba, bali tulikusudia kujenga nyumba ya ngazi ya juu, yenye hadhi kubwa, ili mgeni wako yeyote, hata awe wa ngazi ya juu kiasi gani Kimataifa, akija kukutembelea, asifikie hotelini tena. Vilevile, ni muhimu pia ufahamu kwamba, kazi hii tumekuwa tukiifanya kwa ushirikiano na Kundi la Pili, yaani la Washirika wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, ambao nao waliungana nasi mwaka 2010."

"Baba yetu mpendwa, Askofu Mkuu Zachary Kakobe, na mama yetu mpendwa, Mchungaji Hellen Kakobe; tunawasihi muipokee zawadi yetu hii, tunayoitoa kwa ukarimu wote, kama tulivyokusudia kutoka ndani ya mioyo yetu, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; bali kwa furaha isiyopimika, inayotiririka kutoka ndani mwetu, kwa upendo mwingi tulio nao kwenu wazazi wetu; ikiwa ni Shukurani yetu kwenu, kwa kutupandia vitu vingi vya thamani sana vya rohoni, katika Utumishi wenu uliotukuka, wa zaidi ya miaka 30, tangu mlipoanza Ibada ya kwanza ya Kanisa hili, Jamhuri Shule ya Msingi, Mnazi Mmoja, Dar-Es-Salaam; Jumapili tarehe 30.4.1989, ikiwa na jumla ya watu 13 waliohudhuria, hadi hivi leo ambapo Kanisa lina matawi zaidi ya 1000, yaliyosambaa katika miji na vijiji mbalimbali katika wilaya zote Tanzania Bara; kazi mliyoifanya kwa imani kubwa sana, bila kupokea msaada hata wa shilingi moja kutoka nje ya nchi. Biblia inasema katika 2 TIMOTHEO 2:6, "Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi, kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda." Baba na mama, hili ni fungu lenu la matunda, kutokana na taabu yenu ya kazi mliyoifanya ndani yetu. Hakika mnastahili makubwa zaidi kuliko haya. Hatuna cha kuwalipa kinacholingana na kazi yenu mliyoifanya kwetu, bali Mungu atawalipa thawabu za milele, zilizo zaidi sana ya nyumba hii. Naomba sasa kuwasilisha."

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Kundi la Pili, Dada Mariam Mwaffisi, katika risala yake kwa Askofu Mkuu Kakobe, pamoja na mengi mengine, yaliyogusa nyoyo za maelfu ya watu waliohudhuria katika hafla hiyo, alisema, "Baba yetu mpendwa, Mchungaji wetu, na Askofu wetu Mkuu, Zachary Kakobe; na Mama yetu mpendwa, Mchungaji Hellen Kakobe: Sisi ni watoto wenu tuwapendao upeo. Sawasawa na 1 WAKORINTHO 4:15, yawezekana tukawa na waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hatuna baba wengi. Maana wewe ndiye baba yetu uliyetuzaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

Na sawasawa na WAGALATIA 6:6, ni wajibu wetu kuwashirikisha mema yote, ninyi wakufunzi wetu kwa miaka zaidi ya 30. Hivyo, tunayo furaha kubwa, na ya kipekee; kupata fursa hii adimu, kuwakabidhi Nyumba ambayo, sisi Washirika wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, tunaamini kwamba, umejengewa na Mungu mwenyewe; kwa namna ileile Mungu alivyomjengea nyumba, Mchungaji Daudi, nyakati za Biblia; na sisi tumepata neema tu ya kushiriki ujenzi wa nyumba hiyo, kama watumwa wake Kristo, tusio na faida (LUKA 17:10). BWANA Mungu wetu, alimwambia Mtumishi wake Daudi, katika 2 SAMWELI 7:11, ".... Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA ATAKUJENGEA NYUMBA". Kwa msingi huu, vivyo hivyo, sisi Washirika wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, kondoo wa BWANA aliokukabidhi Yesu Kristo, utuchunge na kutulisha; tunaamini kwamba, ni BWANA aliyekujengea Nyumba hii, na sisi ametutumia tu kama watumwa wake, ili kulikamilisha kusudi lake. Kwa zaidi ya miaka 30, hukutafuta nyumba, bali umeutafuta Ufalme wa Mungu kwanza, na haki yake; hivyo Naye amekuzidishia nyumba pia, sawasawa na Neno lake katika MATHAYO 6:33."

"Baba Askofu Meshack, amekwisha kuzungumza sana, jinsi ambavyo, kwa miaka mingi, hukutaka kabisa kujengewa nyumba, pamoja na jinsi Watumishi wa Mungu na washirika wengi, kote nchini, walivyokuwa wakikusihi sana ukubali kujengewa nyumba. Na sisi washirika wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, ni mashahidi wakubwa wa suala hili.

Baadhi yetu vilevile, tulifanya jitihada nyingi za kukushawishi ili ukubali kujengewa nyumba, tangu mapema sana, bila mafanikio. Hata hivyo, kwa kuwa maelezo yaliyotangulia, yaliyotolewa na Baba Askofu, yamejitosheleza; isingekuwa vema tena kukuchosha kwa historia ndefu yenye mambo mengi yanayojirudiarudia, hata hivyo, tunakusihi uturuhusu kutaja jambo moja tusiloweza kulisahau."

"Mwaka 2006, katika somo ulilolifundisha kupitia katika luninga, lenye kichwa, "SHETANI BABA WA UONGO", pamoja na mambo mengine, ulionesha katika Televisheni kadha, nyumba yako ya pekee ilivyo nje na ndani, mpaka ukaonesha chumba chako cha kulala, huku ukieleza kwamba, nyumba yako ni hiyo moja tu iliyoko Kijitonyama, Dar-Es-Salaam; uliyoijenga mwaka 1986, miaka mitatu kabla ya kuliasisi Kanisa hili, tofauti kabisa na uzushi uliovuma wakati ule, kwamba, una nyumba nyingi za kifahari; maneno yaliyokuwa ya uongo wa mchana kweupe, na ukaeleza kwamba, yeyote anayeifahamu nyumba yako yoyote nyingine, popote pale duniani, ajitokeze hadharani. Ingawa hakuna yeyote aliyejitokeza, na uzushi huo ukawa dhahiri kwa wote waliodanganywa, hata hivyo, kwetu sisi washirika wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, kurushwa katika TV, kwa nyumba hiyo, kulizidi kututia aibu kubwa mbele ya jamii inayotuzunguka, na kutonesha vidonda vya uchungu katika mioyo yetu, tulipotafakari kwamba jamii yote imeuona utupu wetu, kwa jinsi tusivyomthamini baba yetu. Suala hilo liliichochea sana shauku ya kupata kibali kukujengea nyumba, iliyokuwamo ndani mwetu, kwa muda mrefu."

"Kufanya hadithi iwe fupi, hatimaye Mungu alikiona kilio chetu, na tukafarijika sana pale ulipotupa kibali hicho cha kukujengea nyumba. Sasa tena, tukio la leo, kwetu ni kama tunaota ndoto! Kwamba, leo tarehe 25 Oktoba 2020, tumesimama hapa pamoja na Watumishi hawa wa Mungu, tukiwa tayari kuwakabidhi nyumba hii iliyokamilika ujenzi wake??!! Ni ajabu na kweli! Lugha haina maneno mazuri ya kueleza furaha iliyopitiliza, tuliyo nayo leo! Itoshe tu kusema, Mungu wetu atukuzwe sana!"

"Baba, ni vigumu kumtaja kwa jina, kila mshirika aliyechangia kwa namna moja au nyingine, katika kufanikisha kazi hii, maana ni wengi mno. Sisi wanakamati tuliotajwa majina yetu hapa, ni wawakilishi tu wachache wa maelfu ya washirika waliojitoa kwa hali na mali, kwa miaka mingi; ambao baadhi yao, ndiyo maelfu ya washirika hawa walioko mbele yako hivi leo; na pia walikuwepo wanakamati wa kamati nyingine ndogondogo, zilizokuwa mstari wa mbele katika majukumu mbalimbali ya utendaji. Sadaka na juhudi ya kila mmoja, ifike juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu wetu, kama nyakati za Kornelio, na BWANA amtendee mema kila mmoja, sawasawa na kujitoa kwake. Wapendwa Baba na Mama yetu, mwisho kabisa, kwa unyenyekevu na heshima kubwa mbele zenu, kwa niaba ya washirika wote wa Kanisa la FGBF Dar-Es-Salaam, tunaomba muipokee zawadi hii kutoka mikononi mwa watoto wenu. Mioyo yetu inabubujika wingi wa furaha isiyo na kifani, tunapowakabidhi zawadi ya nyumba hii, wakati huu ambapo kazi yako kubwa Baba yetu, ni uandishi wa Vitabu, unaohitaji utulivu mkubwa sana. Ni matumaini yetu kwamba, nyumba hii itakuwa na utulivu unaohitajika katika kazi hii kubwa ya Uandishi wa Vitabu, iliyoko mbele yako. BWANA aibariki kazi hiyo ya uandishi wa vitabu itakayofanyika katika nyumba hii, na Mungu awape afya njema na maisha marefu, ili muyaone kwa macho yenu ya nyama, matunda ya uandishi wa vitabu hivi. Na kwa kila Kitabu kitakachoandikwa chini ya dari ya nyumba hii, BWANA amhesabie kila mshirika aliyejitoa kwa moyo mkunjufu kuifanikisha kazi ya ujenzi wa nyumba hii, kuwa na sehemu katika thawabu za milele zitakazoambatana na kazi ya kubadilisha maisha ya watu wengi, kupitia katika Vitabu hivyo. Naomba kuwasilisha".

Baada ya risala hizo kuwasilishwa kwa Baba Askofu Mkuu Zachary Kakobe, Mtumishi wa Mungu, Askofu Nathan Meshack, alitoa ufafanuzi wa kile kitakachofuata, kwa kusema, "Sasa, muda umewadia wa kuwakabidhi Baba yetu na Mama yetu, zawadi ya nyumba tuliyowajengea, iliyowekwa fenicha zote za ndani. Hata hivyo, kuna jambo muhimu la kuzingatia: Kwa makusudi kabisa, TUSINGEPENDA KUIONESHA NYUMBA TUTAKAYOWAKABIDHI HADHARANI, HATA KWA NJIA YA PICHA, KWA SABABU, NI SADAKA YETU YA SIRI TUNAYOITOA KWA WATUMISHI WA MUNGU HAWA, SAWASAWA NA MATHAYO 6:2-4. Hivyo basi, mahali hapa, tutawakabidhi Nyumba hii, kwa kutumia mfano wa Ufunguo mkubwa, nitakaoushika upande mmoja, kwa niaba ya Maaskofu na Wachungaji wote wa Kanisa la FGBF; na upande mwingine wa Ufunguo huo, utashikwa na Dada Mariam Mwaffisi, kwa niaba ya washirika wote wa Kanisa la FGBF nchini kote. Kisha, baada ya tendo hili, tutawakabidhi pia Hati ya Umiliki wa Kiwanja, na hati nyingine mbalimbali za Nyumba."

Baada ya makabidhiano hayo kufanyika, Askofu Mkuu Zachary Kakobe, alitoa Neno fupi la Shukurani, na kisha kuwabariki wote waliohusika katika kujitoa huko, na baada ya hapo, Maaskofu na Wachungaji wote, wakahitimisha hafla hiyo, kwa kuambatana na Askofu Mkuu Kakobe, na kwenda kuiweka wakfu nyumba hiyo. "Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina." (WAEFESO 3:20-21).

Chanzo cha makala ni ukurasa wake Facebook; Askofu Zachary Kakobe
 

Attachments

 • FB_IMG_1606448504927.jpg
  File size
  22.1 KB
  Views
  0
 • FB_IMG_1606448516771.jpg
  File size
  25.7 KB
  Views
  0
 • FB_IMG_1606448550664.jpg
  File size
  23.3 KB
  Views
  0

mng'ato

JF-Expert Member
Oct 27, 2014
28,599
2,000
Hiyo nyumba nadhan naijua. Ni kasri kubwa balaa.

Ipo junctiin ya rainbow mbezi chini, next to GBP petrol station.

Hiyo kighorofa ni balaa kubwa. Jioni nitakipiga kapicha aisee
Hahah nilihisi tu ni dude la maana ndio maana hawataki kulionyesha.

Huyu jamaa nilikuja kushtuka kile kipindi amemzingua jiwe wale vijana wa TRA wakivyokuta kwny a/c ya yake kuna mabilioni nikajua tu ni mpigaji kama wenzake tu.
 

Philipo D. Ruzige

Verified Member
Sep 25, 2015
6,927
2,000
Hahah nilihisi tu ni dude la maana ndio maana hawataki kulionyesha.

Huyu jamaa nilikuja kushtuka kile kipindi amemzingua jiwe wale vijana wa TRA wakivyokuta kwny a/c ya yake kuna mabilioni nikajua tu ni mpigaji kama wenzake tu.
Hilo jumba ni next level. Ile exterior ni balaa. Ukuta tu nadhan unapata kibanda uswahilini.

Kubwa mno hilo jumba
 

MoseKing

JF-Expert Member
Jul 5, 2017
1,632
2,000
Hiyo nyumba nadhan naijua. Ni kasri kubwa balaa.

Ipo junctiin ya rainbow mbezi chini, next to GBP petrol station.

Hiyo kighorofa ni balaa kubwa. Jioni nitakipiga kapicha aisee
Waumini wake wamenyong'onyeaaaa kama wanaumwa.

Wako full radicalized aisee.

Katika maisha haya kuna vitu ni underated sana.

Uhuru wa fikra ( hasa ukidhibiti njaa ), Utu, na

Kujitegemea kimawazo
 

mng'ato

JF-Expert Member
Oct 27, 2014
28,599
2,000
Waumini wake wamenyong'onyeaaaa kama wanaumwa.

Wako full radicalized aisee.

Katika maisha haya kuna vitu ni underated sana.

Uhuru wa fikra ( hasa ukidhibiti njaa ), Utu, na

Kujitegemea kimawazo
'Uhuru wa fikra ( hasa ukidhibiti njaa ), Utu, na Kujitegemea kimawazo'.

Bonge la point.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom