Wauaji Kilimanjaro waondoka na kichwa,moyo na utumbo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
INAWEZEKANA likawa moja ya matukio mabaya ya kufungua mwaka 2011 mkoani Kilimanjaro, baada ya watu wasiojulikana kumuua mwanamke na kuondoka na viungo mbalimbali vya mwili wake kikiwamo kichwa.

Mwili wa marehemu,Serapia Lucas (62) uligunduliwa na mumewe jana saa 12:00 asubuhi nyuma ya nyumba yao eneo la Manda Juu, Tarafa ya Mengwe Wilaya ya Rombo na kusababisha eneo hilo kuzizima kwa vilio.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yusuph Ilembo alilithibitishia Mwananchi kuuawa kwa mwanamke huyo na kueleza kuwa wauaji hao waliondoka na viganja vyote vya mikono, nyayo zote na sehemu za siri.

Pia wauaji hao ambao wanasakwa na polisi, waliukata moyo wake nusu na kuondoka nao huku utumbo wa marehemu ukikutwa mita nane kutoka kilipokuwa kiwiliwili na kipande cha moyo kilikutwa mita tano kutoka kilipokuwa kiwiliwili hicho.

Kaimu Kamanda Ilembo alifafanua kuwa jana asubuhi, mume wa marehemu aitwaye Lucas Kisera ambaye ni mlinzi wa usiku katika zahanati ya Manda Juu, aligundua mwili huo wa mkewe aliporejea nyumbani kutokea kazini.

“Mwili wa marehemu umekatwa kabisa sehemu ya kiuno kutenganisha na kiwiliwili kingine na uchunguzi wa awali unaonyesha huenda mauaji hayo yamesababishwa na imani za kishirikina”alisema Kaimu Kamanda Ilembo.

Habari zaidi kutoka ndani ya Jeshi hilo zililidokeza Mwananchi kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa kabla ya kumtwaa mwanamke huyo, wauaji hao walivunja mlango wa mbele na kisha kumtoa nje na kumchinja.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mazingira ya eneo la tukio yanaonyesha kuwa wauaji hao walitumia muda mrefu kufanya mauaji hayo na kukatakata viungo hivyo na kutoweka navyo huku majirani wakiwa hawajui kinachoendelea.

Habari zaidi zilidai kuwa huenda viungo vya mwanamke huyo vikawa vimepelekwa katika machimbo ya madini ya Tanzanite ya Mererani kwa ajili ya makafara au kuchukuliwa na mfanyabiashara mmoja kwa imani kama hizo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kuliibuka madai kuwa baadhi ya wamiliki wa machimbo ya madini huko Mererani wamekuwa wakitambikia kwa viungo vya binadamu ili machimbo hayo yaweze kutoa madini mengi zaidi.

Machimbo hayo kwa sasa yanakabiliwa na ukame mkubwa wa kutoa madini hali ambayo imesababisha umasikini mkubwa kwa wachimbaji ambao wamewekeza mamilioni ya fedha kwa baruti na chakula lakini wakiambulia patupu.
 
Back
Top Bottom