Watumishi wasio na vyeti vya ufaulu kidato cha nne lakini...

Mlenge

R I P
Oct 31, 2006
2,125
2,291
TLDR; Watumishi wasio na vyeti vya ufaulu kidato cha nne, na hawajadanganya sifa zao, wengine wana sifa zilizozidi au zilizo sawa na cheti cha kidato cha nne kutokana na uzoefu na mafunzo mengine, mambo ambayo yanatambuliwa pia kisera.

Mfumo wa elimu Tanzania umegawanywa kwenye ngazi kumi.

Ngazi ya juu kabisa ya elimu Tanzania ni ngazi ya kumi. Hapa tunakuta Shahada ya Uzamivu (PhD). Ngazi ya kwanza kabisa ni elimu ya msingi. Ngazi nyingine nane ziko kwenye baina ya hizo hgazi mbili.

Kwenye utumishi wa umma Tanzania, sera ni kuajiri kuanzia walio kwenye ngazi ya nne.

Kwenye ngazi ya nne, ndiko tunakokuta elimu ya sekondari mpaka kufikia kidato cha nne. Lakini siyo elimu ya sekondari pekee. Ipo pia elimu ya ufundi (Vocational Training, kiwango cha cheti cha Gredi I, yanayosimamiwa na VETA). Kadhalika, katika ngazi ya nne, yapo mafunzo ya stadi (Basic Technical Cetificate, yanayosimamiwa na NACTE). Hali kadhalika, yako mafunzo ya kitaalam (Professional, yanayosimamiwa na Bodi za utaalam husika) ambayo humwezesha mwenye kuwa navyo kwa ngazi fulani kuwa sawa tu na elimu ya kidato cha nne. Kana kwamba hayo yote hayatoshi, elimu inaytokana na uzoefu kwenye kazi, ajira au maisha nayo hutambuliwa kufikia na hata kuzidi elimu ya kidato cha nne. Utambuzi huu hujulikana kwa Kiingereza Recognition of Prior Learning, RPL,au lifelong learning na hutambuliwa na vyombo vyote vinavyosimamia elimu Tanzania.

QualificationsFramework.png Chanzo: Chapisho la Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, TCU.

Jambo la kusikitisha ni kwamba waajiri wengine katika utumishi wa umma hawatambui uwepo wa njia nyingine za kujipatia elimu na milinganyo yake na elimu "rasmi", yaani, ya sekondari. Kwa mantiki hiyo wamekuwa wakitishia kuwaondoa kwenye utumishi wa umma watumishi wasio na cheti cha ufauli kidato cha nne, hata kama watumishi hao wana vyeti vya ufaulu kwa ngazi ya nne ya elimu na hata kuzidi ngazi hiyo. Waajiri hao ndio kabisa hawajali suala la RPL kwenye utumishi wa umma. Tuchukulie mifano kadhaa ya kinadharia watu walioajiriwa mwaka juzi.

Mfano wa Kwanza:
Mtu mwenye shahada ya kwanza (Bachelor) au Shahada ya pili (Masters) au hata Shahada ya tatu (PhD) lakini hana cheti cha ufaulu kidato cha nne.

Hapa waajiri wengine husema, Kanuni za Utumishi wa Umma, Sera ya Utumishi wa Umma na miongozo mingine zinataka cheti cha ufaulu kidato cha nne. Huyu mtu hakustahili kuajiriwa. Aondoshwe kwenye utumishi wa umma. Kwanza aliwezaje kusoma mpaka kufika kote huko bila kuwa na cheti cha kidato cha nne?

Mfano wa pili:
Mhasibu mwenye CPA (T) iliyotolewa na bodi ya wahasibu na wakaguzi Tanzania (NBAA), lakini hana cheti cha kidato cha nne.

Hapa tena waajiri wengine husema, Kanuni za Utumishi wa Umma, Sera ya Utumishi wa Umma na miongozo mingine zinataka cheti cha ufaulu kidato cha nne. Huyu mtu hakustahili kuajiriwa. Aondoshwe kwenye utumishi wa umma. Kwanza aliwezaje kusoma mpaka kufika kote huko bila kuwa na cheti cha kidato cha nne?

Mfano wa Tatu:
Mtaalamu wa manunuzi mwenye Diploma ya Procurement inayotolewa na chuo kinachotambuliwa na NACTE, lakini hana cheti cha kidato cha nne.

Hapa pia waajiri wengine husema, Kanuni za Utumishi wa Umma, Sera ya Utumishi wa Umma na miongozo minginezinataka cheti cha ufaulu kidato cha nne. Huyu mtu hakustahili kuajiriwa. Aondoshwe kwenye utumishi wa umma. Kwanza aliwezaje kusoma mpaka kufika kote huko bila kuwa na cheti cha kidato cha nne?

Mfano wa Nne:
  1. Dereva mwenye mafunzo ya Gredi I ya VETA, lakini hana cheti cha kidato cha nne.
  2. Sekretari mwenye Basic Technician Certificate ya Ukatibu Muhtasi kutoka kwenye chuo kinachotambuliwa na NACTE, lakini hana cheti cha kidato cha nne.
  3. Mtunza kumbukummbu mwenye Basic Technician Certificate ya kutunza kumbukumbu kutoka kwenye chuo kinachotambuliwa na NACTE, lakini hana cheti cha kidato cha nne.
  4. Polisi-msaidizi (auxilliary police) mwenye cheti kilichotolewa na chuo kinachotambuliwa na NACTE, lakini hana cheti cha kidato cha nne.
  5. Dereva/katibu muhtasi/fundi/mtunza kumbukumbu/askari/msaidizi sekta ya afya/kada zingine anuai --- mwenye elimu inayotokana na uzoefu kazini, mwenye kumudu kazi zake murua, aliyepitia mafunzo fulani ya kada yake --- RPL inamtambua sawa au kuzidi elimu ya kidato cha nne, lakini hana cheti cha kidato cha nne.
Hapa kadhalika waajiri wengine husema, Kanuni za Utumishi wa Umma, Sera ya Utumishi wa Umma na miongozo minginezinataka cheti cha ufaulu kidato cha nne. Huyu mtu hakustahili kuajiriwa. Aondoshwe kwenye utumishi wa umma.

Ni wazi taifa linapoteza nguvukazi nyingi kwenye utumishi wa umma isivyostahili, kwa vile tu waajiri wengine hawazingatii mfumo wa ulinganishaji elimu mbalimbali.

Ni vema sasa taifa likarejea UTEKELEZAJI wa uamuzi wa kusimamisha mishahara/ajira ya wasio na vyeti vya ufaulu kidato cha nne. Kwa vile waajiri wengine wamewaondoa watumish hata kama wana sifa zinazoungwa mkono na mfumo wa ulinganifu elimu, serikali iangalie uwezekano wa kuwarejesha watumishi hao wote kwenye utumishi wa umma, na zoezi hilo litekelezwe upya kwa kuzingatia mfumo wa ulinganishaji elimu, ikiwemo na kuzingatia elimu itokanayo na uzoefu (RPL au lifelong learning).

http://www.tcu.go.tz/images/documents/RPLguideLine.pdf
Bachelor of Information and Records Management | Sokoine University of Agriculture
https://www.udom.ac.tz/?p=2603

Kwa kutumia vigezo vya RPL, mtumishi anaweza kujiunga na elimu ya juu; bila shaka vigezo hivyohivyo vinatosha kumfanya abakie kwenye utumishi wa umma.
 
Back
Top Bottom