Watumishi hewa nchini wafikishwe mahakamani

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
RAIS John Magufuli wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa Machi 15 mwaka huu, aliwapa siku 15 kuhakikisha wanabaini watumishi hewa katika mikoa yao na kuwaondoa katika mfumo wa malipo.

Baada ya siku hizo kumalizika, jumla ya watumishi hewa 7,795 walibainika na kwamba wameisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 7.5. Watumishi hao hewa ni ama wagonjwa, wamekufa, walishastaafu au kuacha kazi. Aidha, katika gazeti letu la jana, kulikuwa na habari kuwa “Wazalisha watumishi hewa kikaangoni” .

Kwa mujibu wa habari hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka makatibu tawala wa mikoa nchini, kuchukua hatua kali kwa wote waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa.

Kwa ujumla, tunaunga mkono kauli hizo za Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa kuhusu suala hilo la watumishi hewa, ambao wameisababishia serikali hasara kubwa. Tunaomba watumishi hewa wote, wabainishwe na wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria za utumishi ili kuokoa fedha nyingi za serikali, ambazo walikuwa wakilipwa.

Makatibu Tawala wa mikoa ndio wakuu wa watumishi katika mikoa. Hivyo, ni lazima wachukua hatua kali kwa wote waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa ; na si kukaa kungoja maagizo ya Rais na Waziri Mkuu.

Tuna imani kazi ya kubaini watumishi hewa, itakuwa endelevu na kutakuwa na timu za kufanya uchunguzi nchi nzima, kubaini sababu zilizosababisha watumishi waliokufa, wagonjwa, walioacha kazi au kustaafu kuendelea kulipwa.

Tunampongeza pia Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sulemani Jafo kwa taarifa yake aliyotoa wakati akifunga mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT), ambako alisema fedha za mishahara ya baadhi ya watumishi hewa, zilizokuwa zikilipwa kwenye halmashauri nchini, zimeanza kurudishwa.

Jafo alieleza kuwa halmashauri moja, tayari imerejesha Sh milioni tano na kwamba fedha zote zinazorudishwa, zikatiwe risiti. Wakurugenzi watano pia walisimama, kuthibitisha kufanya hivyo kwenye halmashauri zao, ingawa hawakutaja halmashauri zao.

Wakurugenzi wa halmashauri nchini, wahakikishe watumishi wote hewa, wanarudisha fedha walizokuwa wakilipwa. Pia, tunasisitiza kuwa mabilioni yote ya Shilingi, waliyolipwa watumishi hao hewa, lazima yarejeshwe serikalini. Tunaomba watu wote waliobainika kuwa watumishi hewa, akaunti zao zifungwe, wakamatwe na kufikishwa haraka mahakamani.
 
Back
Top Bottom