Watu zaidi ya 50 wajitokeza kuwania ukurugenzi TANESCO

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
WATU zaidi ya 50 wamejitokeza kuomba nafasi ya Mkurugenzi Mkuu Tanesco iliyotangazwa Septemba 18, mwaka huu na Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo.

Taarifa ilizozifikia Mwananchi kutoka ndani ya kamati iliyoundwa kupitia mchakato wa kuajiri Mkurugenzi Mkuu huyo, zimesema hatua za awali za kupendekeza majina matatu kati ya walioomba kushika nafasi hiyo zimekamilika. Mapendekezo ya kamati hiyo yanatarajiwa kukabidhiwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco baada ya taratibu zote kukamilika; ambayo itateua jina moja kati ya hayo baada usaili kufanyika.

“Pamoja na kwamba kazi ya kuchuja majina ya watu zaidi ya 50 walioomba nafasi hiyo kuwa ngumu, kila kitu kimekwenda vizuri,” kilisema chanzo hicho.

Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco Septemba 18 ilitangaza nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiriwa na Dk Idris Rashid kuwa wazi na kuwataka watu wenye sifa za kushika nafasi hiyo kwenye shirika hilo nyeti wawe wamewasilisha barua zao za maombi kabla ya Oktoba 2.
Nafasi hiyo ilitangazwa kufuatia Mkurugenzi Mkuu wa sasa, Dk Idris Rashid kuwa katika hatua za mwisho kumaliza mkataba wake wa miaka mitatu unaomalizika Novemba mwaka huu. Alijiunga na Tanesco mwishoni mwa mwaka 2006.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya kutangazwa kwa nafasi hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ilikataa mchakato wa kupokea na kuchuja majina ya watu wenye sifa kufanywa na Tanesco na kuamua kuunda kamati ndogo iliyowahusisha wataalamu kutoka nje ya shirika hilo.

Chanzo hicho kinaongeza kuwa kamati hiyo ndogo inakaa chini ya uenyekiti wake, Beatus Segeja kutoka Benki ya CRDB ikishirikiana na kampuni ya kutoa ushauri ambayo mara nyingi hutumiwa na Tanesco.

“Bodi ya Wakurugenzi iligundua kuwa mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu mpya ukifanywa na watu kutoka ndani ya Tanesco ungeleta minong'ono ya kimaslahi, hivyo iliamua kuipa jukumu hilo kamati hiyo,” kilibainisha chanzo hicho.

Alipoulizwa kuhusiana na mchakato huo, Mwenyekiti wa kamati, Segeja ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Benki ya CRDB alisema hawezi kueleza lolote kwa kuwa si msemaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco.

“Kamati yangu imeagizwa kushughulikia mchakato mzima wa kupitia na kuchuja majina na kisha kuyapeleka katika Bodi ya Wakurugenzi, kwa maelezo zaidi wasiliana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi wa Tanesco, Peter Ngumbulu,” alisema Segeja.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Mwananchi imezipata, zinasema kamati hiyo ikishirikiana na kampuni hiyo ya ushauri ilikutana juzi na jana kuchuja majina ya watu 50 walioomba kazi hiyo, ili kubaki na majina matatu yatakayo wasilishwa kwenye bodi tayari kwa usaili.

“Juzi na leo (jana) kamati hiyo ndogo na kampuni ya ushauri zilikutana kuchuja majina ya waliyoomba, ili kubaki na matatu yatakayopelekwa katika bodi kwa ajili ya hatua zaidi hadi kumpata Mkurugenzi Mkuu mpya wa Tanesco,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa mchakato wa kupokea barua zilizotumwa kwa ajili ya kuwania nafasi haikufanywa na watu wa Tanesco.

Alipoulizwa kuhusu mchakato huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Peter Ngumbulu alisema yuko kwenye mkutano hivyo hawezi kuzungumza lolote kuhusiana na suala hilo.

“Samahani ndugu mwandishi, muda huu siwezi kuongea na wewe, nipo kwenye kikao,” alisema Ngumbulu.

Baadaye gazeti hili lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Semindu Pawa ambaye alikiri kuwa bodi hiyo imeteua kamati ndogo kufanya mchakato wa awali wa kuchuja majina ya waombaji na kubakiza matatu yatakayowasilishwa kwenye Bodi na kisha wahusika kufanyiwa usaili.

“Ni kweli suala hilo kwa sasa halipo kwetu, ila kuna watu wanalishughulikia na tulifanya hivyo kwa makusudi ili kuondoa migongano ya kimaslahi, lakini litarudishwa kwetu mara baada ya kupata majina ya watu watatu katika hatua za mwisho za kumpata Mkurugenzi Mkuu,” alisema Pawa.

Tangazo la bodi hiyo kuhusiana na nafasi hiyo lilibainisha dira ya Tanesco katika kufanikisha huduma za shirika hilo kwa jamii na taifa kwa jumla.

“ Dira ya Tanesco ni kuongeza thamani na kuifanya kampuni iwe na uwezo wa kibiashara na kifedha, ili kupanua huduma ya umeme nchini, hasa maeneo ya vijijini. Kwa mtazamo huo, Tanesco ingependa kuajiri mtu mwenye elimu, mwenendo, mzoefu na mwenye sifa ya kujaza nafasi ya mkurugenzi mkuu ili aweze kuendesha kampuni kwa ufanisi na weledi,” ilisema sehemu ya tangazo hilo.

Tangazo hilo lilisema Mkurugenzi Mkuu mpya atashikilia nafasi hiyo kwa miaka mitatu na mkataba wake unaweza kusainiwa upya mwishoni mwa ule wa mwanzo.

Dk Idris alichukua shirika hilo wakati nchi ikiwa imekumbwa na tatizo kubwa la ukame uliosababisha kupungua kwa uwezo wa Tanesco kuzalisha umeme na hivyo taifa kujikuta likiingia kwenye mkataba tata wa uzalishaji umeme wa dharura na Kampuni ya Richmond Development (LDC).

Kashfa ya mkataba huo ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na baadaye kufuatiwa na mawaziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha.

Hata hivyo, udhaifu wa mkataba huo uliendelea kuitafuna nchi na mwaka jana, Tanesco ilisitisha mkataba na Dowans Tanzania, kampuni iliyorithi mkataba wa Richmond, hatua ambayo imesababisha Dowans kuishtaki serikali.

Katika hatua isiyo ya kawaida, serikali na Tanesco zilianza mchakato wa kununua jenereta za Dowans kwa madai kuwa nchi ilikuwa haizalishi umeme wa kutosha na hivyo mitambo ambayo inaweza kupatikana kwa urahisi ni ya Dowans, jambo lililopingwa vikali na Bunge kupitia kamati yake ya Nishati na Madini.

Msimamo huo wa Bunge ulisababisha Dk Idris kuibuka hadharani na kutoa taarifa kuwa suala hilo lilizingirwa na mizengwe ya kisiasa huku akitahadharisha kuwa iwapo giza litaikumba nchi, asilaumiwe.

Mkurugenzi huyo pia amewahi kutamba kwenye vyombo vya habari wakati iliporipotiwa kuwa ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake baada ya kutofautiana na mwenyekiti wake wa bodi, Balozi Fulgence Kazaura na waziri aliyekuwa akihusika na nishati wakati huo, Karamagi kuhusu uamuzi wa Tanesco wa kukata umeme kwenye kiwanda cha Saruji cha Tanga (TCC).

Inadaiwa kuwa baada ya kupata habari kwamba kiwanda hicho kimechezea mita ya umeme, Dk Idris aliagiza kikatiwe umeme, lakini akapokea maelekezo kutoka kwa wakuu hao kuwa aurejeshe na alipokaidi, walimuagiza meneja wa Tanesco wa Tanga aurejeshe, ndipo Dk Idris alipojiuzulu na bodi kuridhia uamuzi wake.

Hata hivyo, Rais Kikwete alikataa barua yake ya kujiuzulu.
Inadaiwa pia kuwa Dk Idris aliagiza Mwenyekiti wa bodi wa wakati huo, Balozi Kazaura apokonywe gari la kifahari alilokuwa akitumia kwa gharama za Tanesco na pia kumuondoa kwenye ofisi ambayo mwenyekiti huyo alikuwa akiitumia kwenye makao makuu ya zamani ya Tanesco.
 
Khaa!! Mkuu umeiona tarehe? Ndiyo uzuri wa jumamosi usiku..

Hata hivyo ni bora tujikumbushe. Dkt. Idriss kwenye msimamo namkubali sana huyu mtu, hizi bodi za mashirika ndizo zinaxoua mashirika kwanza wengi wao ni vizee hivyo vinafanya bodi za mashirika kama vijiwe vyao vya kupiga ulanzi.
 
Back
Top Bottom