Watoto wasafiri kwenye uvungu wa mabasi hadi Dar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Watoto wasafiri kwenye uvungu wa mabasi hadi Dar

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Apr 2, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Apr 2, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  JITIHADA za kupunguza watoto wa mitaani zimeonekana kugonga mwamba baada ya idadi ya watoto wanaoingia jijini Dar es Salaam wakitokea mikoani kuongezeka kwa kasi, huku wengine wakisafiri kwa kujificha kwenye uvungu na buti za mabasi, Mwananchi Jumapili limebaini.

  Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa, watoto saba hadi kumi wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi 14, huingia jijini Dar es Salaam kila wiki wakitokea mikoa mbalimbali ya Tanzania.

  Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Katibu wa Chama cha Mawakala wa Mabasi, (CMMU) Katika Stendi ya Mabasi Ubungo, Hamis Maneno alisema idadi kubwa ya watoto hao hutokea mikoa ya Iringa, Mbeya, Kahama, Morogoro na Tanga.

  “Kila baada ya siku moja au mbili, tunapokea watoto wawili au watatu, wa jinsia zote, wakitokea mikoani,” anasema Maneno.

  Maneno anasema watoto hao wengi huingia stendi ya mabasi wakiwa wamejificha katika buti na uvungu wa mabasi kwenye tanki la mafuta karibu na chesesi.

  Anasema katika tanki kuna sehemu ndogo ambayo inaweza kumtosha mtoto wa mdogo wa miaka sita au saba ambayo ina vyuma ambavyo huvishikilia ili asianguke.

  Hawa watoto wanasafiri kwa shida kweli, kweli, mbali ya hatari kuanguka , lakini vumbi na shida zote za kwake akiwa katika eneo hili, " anasema.

  Maneno anasema watoto hao kila mmoja husimulia hadithi yake huku wengine wakisimulia jinsi walivyotumia usafiri wa hatari kufika jijini.

  “Wengine hupanda gari na kushikilia vyuma vya nyuma ya gari au chini ya gari, wengine hujificha ndani ya buti,” anasema.

  Alisema watoto hao huzitaja sababu za kuzikimbia familia zao kuwa ni kutengana kwa baba na mama.

  Aliongeza: “asilimia 70 hadi 80 ya watoto hawa husimulia kuwa wametoroka nyumbani baada ya familia kusambaratika,”

  Aidha Maneno anasema kuwa udhibiti wa ongezeko la watoto wa mitaani unaonekana kuwa ni mfupa mgumu kwa sababu mihimili stahiki imeshindwa kufanya kazi yake.

  “Kwa mfano mahakama iliamua isiwashikilie watoto wanaoingia jijini kwa sababu haina uwezo wa kuwahudumia,” anasema.

  Anasema ustawi wa jamii nao umeshindwa kufanya msako na kuwarudisha makwao, au ingetafuta mbinu za kuwaweka katika shule au kituo maalum.

  Ramadhani Kidimbe mmoja wafanyakazi wa Kituo cha Mabasi Ubungo, anasema amewahi kushuhudia watoto wengi wakiingia stendi na mabasi ya mikoani wakiwa chini ya uvungu wa gari.

  Anasema watoto hao mbali ya kusafiri kutoka mikoani wakiwa katika eneo hilo, lakini huwa hawana matatizo zaidi ya kuchafuka tu.

  Hata hivyo, anasema ukaguzi mkali unaofanywa na wafanyakazi wa mabasi kabla ya kuanza safari mikoani kumesadia kupunguza idadi yao.

  John Kisute ambaye alisafiri hivi karibuni kutoka Mbeya na moja ya mabasi ya kampuni maarufu aliiambia Mwananchi Jumapili alishangaa walipofika Kituo cha Mabasi Ubungo kuona mtoto mdogo wa miaka sita au mitano ,akitoka chini ya uvungu wa gari akiwa amechafuka vumbi huku akionekana kuchoka sana.

  "Nilishangaa sana kuona mtoto akiwa hajulikani sura kutokana na vumbi aliyokuwana nayo, akiwa hawezi hata kuzungumza vizuri," alisema.

  Mmoja wa watoto hao, Athuman Mohammed (6) anasema aliingia jijini Dar es Salaam, Februari mwaka huu akiwa chini ya uvungu wa gari akitokea mkoani Iringa.

  Anasema aliingia katika uvungu wa gari ya moja ya mabasi ya yanayotoka katika mkoa huu wakati linaoshwa halafu akalala ndani ya uvungu wa gari hadi kesho yake lilipoanza safari yake hadi jijini Dar es Salaam.

  Anasema akiwa katika sehemu hiyo, alishikilia vyuma vya karibu na tanki la mafuta ingawa alisikia njaa, lakini hakuwa na jinsi ya kutoka hadi alipotambua kuwa sasa basi hilo limefika mwisho wa safari.

  Alipata wazo la kuingia jijini baada ya kuambiwa na rafiki yake mmoja ambaye hushinda naye stendi ya mabasi kwamba watoto wasiokuwa na uwezo, wanasafiri chini ya uvungu wa mabasi.

  Ali Rubinza(11) ambaye ametokea mkoani Kagera alidai kuwa, mateso ya mama wa kambo ndiyo yaliyomfanya akimbie nyumbani.

  Anasema: “Simjui mama yangu, baba kila siku ananiahidi atanionyesha mama, lakini hanionyeshi. Halafu mama ananinyanyasa, ananichongea kwa baba kuwa naiba mboga, napigwa sana,”

  Ali anasema kilichomfanya kukimbilia mjini ni hadithi za maisha mazuri yaliyopo hapa ambazo amekuwa akizisikia.

  “Nilijibanza katika viti na konda hakuniona mpaka nikafika hapa,” anasema.

  Kijana huyu alitaja kilichomvutia kuja jijini na si kwingineko kuwa ni hadithi za kuwa Dar es Salaam kuna maisha mazuri.

  “Lakini naona sasa yamenishinda, maji tunanunua, kuoga, kujisaidia mpaka ulipie, kila kitu kinahitaji pesa,” alisema.

  Anasema ugumu huo wa maisha umemfanya ajiajiri kwa kuokota chupa za plastiki ambazo huziuza.

  Mtoto mwingine, Justin Thomas aliyefika jijini akitokea mkoani Singida tangu Novemba mwaka jana, alisema ameamua kuja jijini ili kutafuta pesa kwa sababu ya ugumu wa maisha.

  “Wazazi wangu wote wapo hai, lakini maisha magumu, tunashinda bila kula. Sasa nikasikia kuwa huku unaweza ukafanya biashara ukapata pesa,” alisema Justin.

  Justin ambaye ameacha shule akiwa darasa la nne anasema, anatamani kurudi shule ili baadaye aje kuwa rais.

  Kwa pamoja watoto hao wanasema kutokana na ugumu wa maisha wanaoupata hapa jijini, wanatamani kurudi makwao.

  Maisha yao kituoni

  Maisha ya watoto hawa katika kituo hicho ni magumu kwa vile hawana pa kulala. Wanalala kwenye viti vya sehemu ya kupumzikia abiria na maeneo mengine yaliyopo ya maua yaliyopo katika stendi hiyo.

  Wanapata chakula chao kwa kufanya kazi ya kuokota chupa za plastiki zilizotumika ambazo huziuza kwa Sh500 na kufanya kazi nyingine ndogondogo za kuosha magari ambazo wanaweza kulipwa ujira.

  Maneno anasema watoto hawa hawana mtu ambaye anawaangalia wakati wanapota shida ikiwamo ugonjwa na mambo mengine. "Hawana mtu wa kuwaangalia, labda ikitokea msamaria mwema amchukue kumpeleka hospitali,"

  Anasema huondoka asubuhi ndani ya Stendi kwenda mitaani kutafuta vibarua pamoja na kuokota chupa za plastiki na hurejea kuanzia saa 12:00 hadi saa 1:00 kulala.

  Meneja

  Meneja wa Kituo cha Mabasi Ubungo, Juma Iddi alipotakiwa kueleza wamejipanga vipi kuhakikisha wanakabiliana na watoto hao wanaoingia kila siku kutoka mikoani, alisema hawezi kuongea chochote.
  “Siwezi kuzungumza chochote kuhusiana na suala hili” alisema Iddi.


  Waziri Simba

  Akizungumzia suala hilo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Sophia Simba alisema kuwa kukosekana kwa upendo katika familia ndicho chanzo cha ongezeko la watoto wa mitaani.

  Alisema kuwa watoto hao huzikimbia familia zao kutokana na wazazi kufariki dunia, ugomvi katika familia pamoja na kukosa malezi bora ikiwa ni pamoja na lishe duni

  Waziri Simba alisema licha ya kuwa Serikali kupitia Halmashauri za wilaya inawatumia maofisa wa maendeleo ya jamii kuwahamasisha wazazi, bado suala la upendo kwa watoto linahitajika katika familia.

  “Wazazi wengi maeneo ya vijijini hususa familia zao na kuwafanya watoto kukosa huduma muhimu na kuamua kukimbilia mijini,” alisema Simba.

  Akitolea mfano Stendi ya Mabasi yaendayo Mikoani na Nje ya nchi(UBT), alisema kuwa ndani ya stendi hiyo kuna asasi nyingi zisizo za kiserikali ambazo zinajishughulisha na kuwaangalia watoto hao.

  Hata hivyo, alisema hata kama asasi hizo zitakuwa nyingi kiasi gani,kukosekana kwa upendo ndani ya familia ni moja ya sababu kubwa ya kuongezeka kwa watoto wa mitaani.

  Kamanda Iringa

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa , Evarist Mangala anasema hana taarifa kama mkoa wake kuna watoto wanasafiri kwa kutumia uvungu wa gari na kuahudi kulifanyia kazi suala hilo kabla ya kutoa taarifa rasmi.

  Watoto wasafiri kwenye uvungu wa mabasi hadi Dar
   
 2. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #2
  Apr 2, 2012
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 9,223
  Likes Received: 1,412
  Trophy Points: 280
  Hao ndo wapigakura wetu wa kesho.
   
Loading...