Watoto waliokulia familia korofi wana uwezo wa kukabili matatizo ya kimaisha

Daudi1

JF-Expert Member
Dec 14, 2013
8,761
8,640
mchoro.jpg

Agatha na mumewe Jackob wanaishi katika nyumba ya kupanga ambayo kila mwezi wanatakiwa kulipa bili ya umeme kwa zamu, cha kushangaza Jackob anapokosa fedha hiyo hachanganyikiwi wala kuona aibu kusema sina.

Kwa mujibu wa simulizi ya Agatha, hata anapomsihi mumewe ajitahidi wapate fedha hiyo alipe kwa sababu wapangaji wenzao wapo gizani alijibiwa kirahisi, "Hilo ni tatizo dogo katika makubwa niliyopitia".

Anasema Kinachomshangaza ni tabia ya mumewe ya kutoshtushwa na jambo hata kama limeshtua watu wengi.

Kwa mujibu wa Agatha kuna siku chemba ya choo chao ilikatika na kutumbukia ndani na kutoa mtikisiko uliosababisha watu wa ndani ya nyumba hiyo kutoka na majirani pia, lakini mumewe hakutoka wala kujali.

Alipomuuliza jibu lilikuwa ni lile lile , "hakuna tatizo lisilokuwa na jawabu, likikosa jawabu ujue na maisha yamefikia mwisho, kukimbilia ndiyo dawa, watu tumeona matatizo hilo halijafikia hata robo,"

"Vitu hivi na vingine vingi vya kuogofya ambavyo mume wangu hashtuki vinanishangaza sana, najiuliza ana tatizo gani," analalama na kuuliza Agatha.

Malalamiko hayo ya Agatha yananishawishi kuwatafuta wataalamu wa masuala ya saikolojia waeleze inatokana na nini hasa.

Wataalamu wa saikolojia wakubaliana na hilo

Dk Rebeca Sima kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitengo cha Saikolojia anasema kuwa hali hiyo inatokana na historia ya maisha ya mhusika, kama alikulia katika mitafaruku ya kila kukicha huwa na tabia hiyo ya kutoshtushwa na mambo hata kama yataonekana makubwa.

Anaeleza kuwa mara nyingi mtu kama huyo kujiua, kujitoa muhanga, ni kitu cha kawaida, ingawa anakuwa na uwezo mkubwa wa kumtuliza mtu ambaye ana tatizo.

Dk Sima anafafanua kuwa hata akiwa hakimu katika kesi, anakuwa na ufumbuzi wa haraka kuliko waliokulia katika familia zilizotulia kwa sababu hana jazba katika kufanya uamuzi.

"Kwangu mimi naona hilo ni tatizo, japo wanachukulia mambo kikawaida sana hata yale magumu kuyatolea uamuzi, mtu kama huyu haoni hasara kufanya jambo lolote, kwani hakuna anachoona ni tofauti," anasema Dk Sima.

Kauli hiyo ya Sima inatofautiana kidogo na ya Modester Kamongi mtaalamu wa masuala ya saikolojia kutoka katika Chuo Kikuu cha Dodoma, anayesema kuwa hali hiyo hutokana na kuzoea migogoro na kuamini kila mtu anaishi katika familia za aina hiyo.

Anasema mbali na kuwa wazuri katika kufanya uamuzi hasa unaohusu migogoro, watu hao huwa na kitu kinachoitwa kitaalamu (Mood Disoders), ambapo hawaungi mkono kitu kinachofanywa na mtu yeyote hata kama ni kizuri.

"Watu hao wanahitaji msaada kwani huwa ni walalamishi na hawaridhiki na ni watu wa kulaumu mara nyingi," anasema Kamongi.

Anasema mbali na hilo ni muhimu kuwa nao katika jamii kwani lile linaloonekana kuwa gumu kutatuliwa likifika kwao huwa dogo na huamuliwa bila jazba wala hasira, kwa sababu ya kuzoea kwao migogoro.

Tafiti zaunga mkono

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na wataalamu kutoka katika Chuo Kikuu cha Rollins kilichopo katika Jimbo la Florida nchini Marekani, umeonyesha kuwa migogoro wanayoshuhudia watoto, huwajenga kisaikolojia kupambana na matatizo yanayowakabili, ikiwamo kupata ufumbuzi bila jazba.

Utafiti huo uliosimamiwa na Dk Lindsey Aloia, ulibaini kuwa watoto hao wakiwa wakubwa inakuwa siyo rahisi kwao kupata msongo wa mawazo, kwani wanaweza kuamua kukiacha kitu kama kilivyo na kukitafutia ufumbuzi taratibu na kisiwe ndani ya mawazo yao.

Dk Aloia anasema kuwa watoto hao licha ya kuwa makini katika uamuzi ya masuala magumu, pia wana uwezo mkubwa wa kubishana hasa kwa vitu wanavyoviamini.

Alifafanua kuwa kama kuna ubishi wa kitu fulani hata wawepo watu zaidi ya 10, yeye husimama katika upande anaouamini hata kama hana mifano hai, na hubaki kuwa hivyo na hakuna anayeweza kubadili mawazo yake.

"Watu hawa hawapendi kuwa na mawazo hujali kile wanachokiamini na hawakubaliani na yeyote isipokuwa aliye upande wao," anasema Dk Aloia.

Anaeleza kuwa utafiti huo uliwahusisha wanandoa 50, kutoka katika familia zenye migogoro na zisizokuwa nayo, kwa kuweka mada na kuijadili kwa pamoja.

Dk Aloia anasema kuwa baada ya mjadala huo uliokuwa na mvutano mkali, waliokuja na jibu kamili la utatuzi wa suala lililokuwa mezani walikuwa kutoka katika familia zilizo na migogoro, huku wale wa kutoka kwenye familia tulivu wakisema kuwa suala hilo linahitaji uamuzi wa mahakama.

Anasema kabla ya kuwakutanisha kwa ajili ya mjadala huo waliwachunguza maisha yao ya utotoni kila mmoja na kupata makundi hayo mawili.

"Tuliwachunguza maisha yao kwa siri, lakini tuliwafanyia mahojiano huku tukiwashawishi waeleze maisha yao ya utotoni kwa kuwa majibu tulikuwa nayo tulihitaji uthibitisho ambao tuliupata ingawa kwa shida kwani wengi wao hawakuwa tayari kueleza wakiona ni hali ya kawaida," anasema Dk Aloia.

Wataalamu washauri wazazi waepukane na migogoro mbele ya watoto.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa saikolojia kutoka katika katika Chuo Kikuu cha Brigham Young cha nchini Uingereza, ulionyesha kuwa baadhi ya watoto huathirika na tabia hizo na kupenda kuishi peke yao katika maisha ya baadaye.

Dk Ross Flom aliyesimamia utafiti huo alisema kuwa ni vyema wazazi wakatumia lugha ya upole hata wanapowakemea watoto na kuepuka kugombana mbele yao kuwalinda na maisha ya ajabu hapo baadaye.

"Watoto hushika sana yale waliyofundisha kwa lugha ya upole, kuliko ya kukemewa, hivyo ili wawe na akili na kuelewa masomo yao ni bora kuepuka kugombana na kuwafokea, "anasema Dk Floim.

Wataalamu wa masuala ya watoto kutoka katika Jarida la Tabia na Maendeleo ya Watoto, liliandika kuwa kuwaepushia watoto na migogoro kwa kutowafokea, huwafanya wawe waelewa na huwaongezea mapenzi kwa wengine.

Profesa Denise Solomon, kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania alisema kuwa watu 50 kati ya 100 waliowahoji kama wana msongo wa mawazo walisema hawana, huku historia ya maisha yao inaonyesha kuwa walikulia katika familia zenye migogoro.

Utafiti mwingine uliounga mkono tafiti hizo ni kutoka katika Jarida la Human Communication Research, ulionyesha kuwa watu waliokulia katika familia hizo wana uwezo mkubwa wa kubishana.

Jarida hilo liliwakusanya watoto waliokulia katika mazingira magumu na kuwapa mada ya kujadili kwa mtizamo wa kukubali na kukataa, kilichotokea hakuna aliyeshindwa kati yao huku kila mmoja akijiona na haki ya kusikilizwa.


Source
:http://www.mwananchi.co.tz/habari/W.../-/format/xhtml/item/0/-/xw4jmnz/-/index.html
 
Back
Top Bottom