Watoto milioni 77 duniani hawapati maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa, huchangia asilimia 80 ya vifo vyao

FikraPevu

JF-Expert Member
Jan 2, 2010
303
236
Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) limesema watoto milioni 77 ambao ni sawa na mtoto 1 kati ya 2 wanaozaliwa hawapati maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa ambapo wanakosa virutubisho muhimu, kinga ya mwili na kugusana na mama zao ili kuwakinga na magonjwa na vifo.

Wataalamu wa Afya wanashauri kuwa mtoto apewe maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa ili kumkinga na maambukizi ya magonjwa ya utotoni. Kutokana na sababu mbalimbali za kuchelewa kumnyonyesha mtoto baada ya kuzaliwa huwaongezea hatari ya kufa mapema kwa zaidi ya asilimia 80.

“Nilimzaa mtoto wangu nikiwa nyumbani, hakupata chanjo wala sikumyonyesha alipozaliwa”, hayo ni maneno ya Asha Maulid msichana wa miaka 17 mkaazi wa Mtwara ambaye ana mtoto wa miezi 6. Anasema mtoto wake anaumwa mara kwa mara na anatumia gharama kubwa kumtibu lakini hapati nafuu.

“Mwanangu anaumwa mara kwa mara, amedhohofika sina pesa ya kumpeleka hospitali na mimi nina maisha magumu sina uwezo kumtunza na kumpa lishe kamili”, amesema Asha.

Asha kama walivyo wasichana wengine ambao wanapata mimba za utotoni, wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa kuwatunza watoto wakiwa wadogo na kuwaweka katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa na kufariki katika umri mdogo.

Inaelezwa kuwa kadiri mtoto anavyocheleweshwa kunyonyeshwa maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa hatari ya kufa katika miezi mitano ya maisha yake inaongezeka. Kuchelewa kunyonya kati ya saa 2 hadi 23 baada ya kuzaliwa kunaongeza hatari ya kufa kwa mtoto aliye na siku 28 kwa 40%. Hivyo hivyo kwa saa 24 au zaidi hatari huongezeka hadi asilimia 80.

UNICEF inasema kuwa maziwa ya mama ni kinga na ulinzi wa kwanza kwa mtoto dhidi ya udhaifu na magonjwa. Kukosa maziwa ya mama kunachangia karibu nusu ya vifo vyote vya watoto wachanga lakini maziwa ya mama yakiwekewa msisitizo italeta tofauti katika maisha na kifo kwa watoto.

Zaidi, soma hapa => Watoto wachanga milioni 77 hawapati maziwa ya mama muda mfupi baada ya kuzaliwa, huchangia asilimia 80 ya vifo vyao | FikraPevu
 
Back
Top Bottom