beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,879
- 6,356
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kinondoni, tarehe 02/02/2016 imewafikisha washitakiwa wafuatao mahakamani:-Bw.Bryceson Kajigiri Mwangoma mwenye umri wa miaka 54, Bw.Abel Sebabil Slaa mwenye umri wa miaka 44 na Bw.Bernard Thomas Mkude mwenye umri wa miaka 42 kwa kuiibia Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Tsh.33,681,780.
Washitakiwa hawa Bw.Mwangoma na Bw.Slaa wakiwa Maafisa watendaji wa Kata ya Kimara kwa vipindi tofauti, na Bw.Mkude akiwa Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Kimara Baruti walitenda makosa kinyume na kifungu cha 31, 22, 28 (1) 3 vya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 pamoja na kifungu cha 258, 270 vya sheria ya Kanuni za Adhabu.
Washitakiwa wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kujipatia manufaa kwa kufanya wizi wa fedha hizo zilizokua zimewekwa na Wananchi katika akaunti ya Urasimishaji Ardhi kata ya Kimara iliyopo benki ya Wananchi wa Dar – es- Salaam (DCB) tawi la Magomeni kwa ajili ya kupimiwa maeneo yao.
Mshitakiwa wa kwanza Bw. Mwangoma akiwa mtendaji wa kata kwa kipindi cha tarehe 01/04/2011 hadi tarehe 30/11/2011 kwa kushirikiana na Mshitakiwa wa tatu Bw.Mkude ambaye ni mshitakiwa wa pili walitumia madaraka yao kwa kushirikiana kuiba kiasi cha Tsh. 24,764,280. Bw. Slaa akiwa mtendaji kata kwa kipindi cha tarehe 01/06/2013 hadi tarehe 31/01/2014 kwa kushirikiana na Bw.Mkude waliiba kiasi cha Tsh. 8,917,500.
Washitakiwa walifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kufunguliwa kesi namba 51/2016 inayosimamiwa na Mhe. Hakimu Mushi. Watuhumiwa wako nje kwa dhamana na kesi imepangwa kusikilizwa tena tarehe 16/02/2016.
IMETOLEWA NA MKUU WA TAKUKURU (M) KINONDONI
BENN LINCOLIN
04/02/2016