SALAAM ZA PONGEZI KWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA USHINDI WA RAIS WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 2010 2015
----
Chama cha Mapinduzi Tawi la UK kinatuma salaam za pongezi kwako Dr. Jakaya M Kikwete kwa ushindi wa nafasi ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2010 2015.
Wana CCM na Watanzania UK waliridhika sana nawe Dkt. Kikwete kwa uwezo wako mkubwa wa kuzielezea na kuzitetea kwa uwazi sera endelevu za CCM na pia kumudu kuwahamasisha Watanzania kuielewa na kuikubali ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2010 2015.
Aidha awali kabla na wakati wa kampeni za kuinadi ilani ya uchaguzi ya CCM 2010 2015 uliendelea kudhihirisha ukomavu na uzoefu wa uongozi wa kidemokrasia ndani ya chama na baina ya vyama kitaifa na mfano wa kuiga katika medani za siasa za kimataifa.
Ushindi wako ni ishara ya IMANI ya Watanzania kwako na kwa CCM. Ni matumaini yao utekelezaji wa ilani ya CCM 2010 2015 utaendelea kuzingatia kasi na uwezo mkubwa katika ngazi zote za utawala na uwakilishi kuanzia chini waliko wananchi wanaoathirika na kero za umasikini.
Kwa kuwa umekiongoza Chama na Serikali yake vizuri na kusajili mafanikio makubwa toka mwaka 2005 hadi 2010, kipindi hiki cha pili ni DHAMANA nyingine tena kwako na kwa CCM kuendelea kuvuna na kutumia rasilimali za Taifa letu kuongeza maendeleo na maisha bora yenye usawa kwa kila Mtanzania. Aidha kuapishwa mbele ya halaiki ya Watanzania ni MKATABA mpya na rasmi wa kuwalinda na kuwatetea Wananchi na mali zao ndani na nje ya nchi.
Kwamba utaendelea kujenga Demokrasia yenye nidhamu kama ilivyoshamiri leo Tanzania na kuimarisha Utawala Bora ambao hautamvumilia mtu awaye yote kuchochea na kuhatarisha ulinzi na usalama wa raia au kuhujumu uchumi wa taifa letu katika kiwango chochote.
Kwa kuwa wewe ni MWASISI wa ushirikishwaji wa Watanzania ughaibuni, CCM-UK inaamini utaendelea kuiongoza serikali kufungua milango ya uwezeshaji na uwekezaji na kuhamasisha asasi binafsi kushirikisha na kuvuna rasilimali za Watanzania ughaibuni kwa maendeleo ya Taifa letu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MAPINDUZI DAIMA.