Watanzania watupime kwa utekelezaji wa Ilani – Kinana | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Watanzania watupime kwa utekelezaji wa Ilani – Kinana

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Rutashubanyuma, Sep 25, 2010.

?

HIVI TUNAWEZA KUIPIMA CCM KAMA INAKWEPA MDAHALO?

 1. CCM KWA KUKWEPA MDAHALO NI DHAHIRI INATAKA KUJIPIMA YENYEWE

  25.0%
 2. HOTUBA TU ZINATOSHA ZA JK NA WENZIE

  0 vote(s)
  0.0%
 3. HIVI ARI MPYA NGUVU MPYA NA KASI MPYA HAMUIONI?

  0 vote(s)
  0.0%
 4. CCM WANATAKA TUWAPIME KWA KUCHUNGULIA MAKARATASI NA WALA SIYO VITENDO

  75.0%
 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Sep 25, 2010
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,592
  Trophy Points: 280
  Watanzania watupime kwa utekelezaji wa Ilani – Kinana

  [​IMG]
  Godfrey Dilunga​
  Septemba 22, 2010 [​IMG] [​IMG]Awashangaa wanaosema Kikwete anatoa ahadi nyingi sana
  Ifuatayo ni sehemu ya pili na ya mwisho ya mahojiano ya mwandishi wetu GODFREY DILUNGA na Mwenyekiti wa Kampeni za CCM, Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana, aliyoyafanya hivi karibuni mjini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za CCM-Lumumba.

  Raia Mwema: Ukiwatazama wagombea hawa wawili, Dk. Slaa na Profesa Lipumba kwa kuzingatia nguvu au mwenendo wao kisiasa, ni mikoa au majimbo gani ambayo tunaweza kusema wanaiweka CCM kwenye hali ya hati hati?
  Kinana: Sidhani. Sisi tunaangalia majimbo yote. Sisi ni chama cha siasa kilicho makini. Tunaangalia kila jimbo, kura tulizopata tangu 1995 hadi 2000 na 2005. Tunafanya uchambuzi, tunaangalia uwiano kati ya kura walizopata Upinzani na tulizopata sisi.
  Pale ambapo wapinzani walipata kura nyingi si za ushindi, lakini za kutosha tunapeleka nguvu kubwa zaidi, pale ambapo sisi tumepata nguvu tuna uhakika yapo maeneo ambayo kwa kweli tunayaita safe seats yaani seats ambazo hazina tatizo hata kidogo.
  Raia Mwema: Kwa mfano?
  Kinana: Kwa mfano Isimani pale, hatuna tatizo kubwa sana. Yapo majimbo mengine mengi tu. Lakini yapo majimbo mengine ambayo ni lazima tupeleke nguvu ya ziada. Ni lazima tuhakikishe kwamba tunaweka mkakati mzuri zaidi wa ushindi.
  Raia Mwema: Tarime ni kati ya hayo majimbo?
  Kinana: Yaah, kwa mfano Moshi Mjini, Karatu, Kigoma Kaskazini, haya ni maeneo ambayo yameshikwa na Upinzani. Lazima tupeleke nguvu zetu kuhakikisha kwamba tunapata ushindi kwa sababu ni maeneo ambayo yanashikiliwa na Upinzani. Na kuna maeneo ambayo tulishinda labda kwa asilimia kidogo, hayo maeneo ni lazima tupeleke nguvu kubwa zaidi ili kuhakikisha tunapata ushindi mzuri.
  Raia Mwema: Kazi yako kubwa ukiwa Mwenyekiti wa Kampeni ni kuhakikisha mgombea urais wa CCM, Kikwete anashinda. Ni mambo gani ya msingi unadhani yatasababisha si ushindi tu bali ushindi wa kishindo kama mnavyotamba?
  Kinana: Ni mambo matatu. La kwanza, watu watatazama ahadi alizotoa mwaka 2005 zimetekelezwa kwa kiwango gani. Hili ni namba moja na labda inawezekana Rais Kikwete mwenyewe asiweze kuwaambia kila hatua ya utekelezaji, lakini alikuwa akiongoza Serikali.
  Kuna Serikali Kuu na Serikali za Mikoa na Wilaya…halmashauri za wilaya. Kila wilaya, kila kata imetoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani, imeelezea shughuli gani imefanyika na kwa kiwango gani.
  Lakini yapo maeneo kadhaa ambayo hatukutekeleza Ilani kwa kiwango kilichotakiwa kwa ngazi ya kitaifa, mkoa au wilaya. Tumeelezea kwa nini imeshindikana.
  Tumeeleza kama ni tatizo ni upungufu wa fedha au mipango haikuwa mizuri na ya uhakika, na kama ni utendaji mbovu wa watendaji. Lakini tumewaambia kilichotokea na vile vile tumewaambia tutafanya nini kwenye kipindi kijacho.
  Kwa hiyo hili ni la kwanza kwamba Watanzania watatupima kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na wengi wameridhika.
  La pili, Watanzania wanataka kujua tunaahidi nini katika kipindi kijacho. Nitakupa mfano mzuri tu. Katika kipindi kilichopita kuna barabara ambazo tuliahidi kujenga. Watanzania wengine walituletea ujumbe kutuambia kwamba kabla uchaguzi haujaanza tunaomba mradi wetu uwe umeanza na miradi mingi imekwishaanza, barabara kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga ilikuwa ni barabara ambayo kwa kweli ni kero.
  Barabara kutoka Tanga kwenda Horohoro, Songea - Tunduru zimekwishaanza. Tunduru - Mangaka imekwishaanza, kwa hiyo mambo mengi kwa kweli yanakwenda vizuri na tunaomba ridhaa ya wananchi ili tuendelee kukamilisha shughuli hizi.
  Yapo matatizo, kwa mfano, wewe unayajua, shule za kata. Shule hizi zimejengwa, kuna matatizo, hakuna walimu, maabara na kadhalika. Rais Kikwete anaomba ridhaa ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano ili aweze kukamilisha kazi kubwa ya kwanza katika hii miaka mitano.
  Kazi ya kwanza ilikuwa kujenga shule hizi, kuweka vifaa vya msingi na kuweka walimu wachache.
  Kazi inayofuata ni kuimarisha shule hizi kwa vifaa, walimu na vitabu. Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Serikali imejiandaa vizuri sana kuhakikisha vitabu vya kutosha, walimu wa kutosha, vifaa vya maabara vinapatikana ili kuhakikisha shule hizi zinakuwa nzuri na za kisasa.
  Na niseme na unaweza kufanya utafiti mwenyewe, katika kipindi cha miaka 40 ya Uhuru wa nchi yetu, yaani ukichukia mwaka 1961 hadi 2001, vyuo vikuu vimekuwa na wanafunzi wasiozidi 15,000.
  Wakati Rais Kikwete anaingia madarakani kulikuwa na wanafunzi wa vyuo vikuu vyote nchini ni 37,000. Leo kuna wanafunzi 118,000 katika vyuo vikuu, mimi, nadhani haya ni mafanikio makubwa sana ya kupigiwa mfano.
  Mfano mwingine ambao haupo kwenye Ilani ya Uchaguzi wala kwenye ahadi za mgombea, lakini ni jambo lililotoka kwenye kichwa cha Rais Kikwete na akaamua, akatekeleza na leo tunafurahia ni Chuo Kikuu Dodoma, ambacho kufikia mwaka 2014 kinatarajiwa kuwa na wanafunzi 40,000. Kitakuwa Chuo Kikuu kikubwa kuliko chochote barani Afrika.
  Sasa kuna wanaosema Rais Kikwete anatoa ahadi nyingi sana inakuwaje, mfano mzuri ni ule, hakutoa ahadi kwenye ilani na ahadi zake binafsi, lakini akafanya. Sasa sijui ile unaiitaje..ni ahadi au ni…
  Raia Mwema: Unataka kusema ni ubinifu?
  Kinana: Ndiyo. Ni ubinifu, nadhani hilo ni neno zuri zaidi. Ni ubunifu ambao ameufanya na umeweza kuleta mafanikio makubwa zaidi.
  La mwisho ambalo nadhani linamfanya Rais Kikwete ashinde kwa kishindo ni huko anakopita (kwenye kampeni) wananchi wanachukua fursa hiyo kumuelezea matatizo yao ya pale walipo madogo madogo na anawaahidi niachieni mimi mtakaponichagua nitashughulika nayo.
  Na wakati mwingine ahadi hizo anazozitoa rafiki zetu wa Upinzani wanapiga kelele. Amekwenda kule amesema nitaleta meli katika Ziwa Victoria, amefika Kigoma akasema msiwe na tatizo mv. Liemba (meli) imeadhimisha miaka 100 ya kuwapo ziwani sasa tutaiondoa ziwani tutapeleka meli mpya, amekwenda Kyela amesema tutaleta meli nyingine katika Ziwa Nyasa.
  Lakini hivi ni vitu ambavyo vipo kwenye mipango ya Ilani na mipango ya muda mrefu ya Serikali. Msisahau kwamba yeye amekuwa Rais, ni tofauti na wagombea wengine ambao hawakushika uongozi.
  Hizi ni ahadi nzuri na zenye manufaa kwa wananchi. Kinachonishangaza ni kwa nini wagombea wengine walalamike wananchi wasipate meli katika Ziwa Victoria, au Ziwa Nyasa au Ziwa Tanganyika.
  Raia Mwema: Msingi wa hoja yao hiyo si wananchi kunyimwa meli, bali ni kile kinachoelezwa ni matakwa ya Sheria ya mpya ya Gharama za Uchaguzi.
  Kinana: Sheria inasema ukinichagua nitaweka meli, yaani ukiifanya ile ahadi ikakaa ki-rushwa inakuwa tatizo lakini ahadi iliyokuwapo kwenye Serikali kwa sababu ilani inasema tutaimarisha usafiri wa baharini kuondoa kero za wananchi katika usafiri baharini au kwenye ziwa au anga au barabarani hilo si tatizo.
  Na kama utatizama hii ni miradi ambayo Serikali ya Rais Kikwete katika kipindi cha miaka mitano ni miradi ambayo ilifikiriwa, inafanyiwa kazi na kama akipewa ridhaa ya wananchi ataikamilisha na wananchi wa maeneo hayo watafurahia na kunufaika.
  Raia Mwema: Toa ufafanuzi kwa utata unaojitokeza kwenye msafara wa mgombea urais wa CCM, Kikwete. Amekuwa akitumia gari lisilo la Serikali lakini anaambatana na wasaidizi wa Ikulu wanaotumia magari au vifaa vya Serikali.
  Kinana: Kwanza lazima tukubali kwamba chini ya uongozi wa Rais Kikwete sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi ilitungwa kwa hiyo nataka nikuhakikishie yeye ni mtu wa kwanza anayehakikisha kwamba sheria hii inafuatwa.
  Magari anayotumia ni ya CCM, magari wanayotumia wasaidizi wake walioko naye kwa ajili ya kampeni ni magari ya CCM.
  Magari ambayo mimi nina hakika si ya CCM ni magari ya walinzi. Hayo si ya CCM na utaona yamekaa kiulinzi na nadhani duniani kote Rais aliyeko madarakani na ameteuliwa na chama chake pamoja na kwamba ni mgombea wa chama lakini vile vile ni Rais na nchi lazima iwe na Rais wakati wote mpaka Rais mwingine atakapoapishwa au yule yule atakapoapishwa.
  Kwa hiyo si kweli hata kidogo na kama kuna ushahidi wa kutosha ushahidi huu unaweza kuwasilishwa kwenye Tume ya Uchaguzi na tume kama kuna ushahidi wataufanyia kazi.
  Kwa hiyo sisi tunafanya kwa umakini kwa kufuata sheria na Rais mwenyewe…mgombea wetu amesisitiza na kutuagiza lazima tuhakikishe tuna magari mengi ya kwake pamoja na wasaidizi wake na yale yanayochukua waandishi wa habari…yote ni ya CCM.
  Raia Mwema: Tukirudi nyuma kidogo, kuna hoja CCM imejimilikisha mali zilizopatikana kwa jasho la Watanzania wote wakati wa chama kimoja. Dk. Slaa na Profesa Lipumba wanaahidi kurejesha mali hizi serikalini wakichaguliwa. Suala hili lenye sura ya uporaji mali linaweza kuwapunguzia kura?
  Kinana: Nadhani haliwezi kupunguza kura. Si mara ya kwanza. Jambo hili limewahi kuzungumzwa 1995 na wapinzani, 2000 na 2005 na leo wanazungumza hivyo hivyo.
  Labda niseme tu kwamba wote hawa wanaosema hivyo walikuwa CCM. Tulifanya nao kazi ya kujenga viwanja, ofisi za chama, huwezi kuniambia kwamba ofisi za chama ambazo tulizijenga wote pamoja, tuliomba hati na tukapata hati ya viwanja hivyo pamoja halafu wewe ukiondoka unasema hapana mimi nadhani viwanja hivi itabidi tugawane ni jambo ambalo haliwezekani.
  Raia Mwema: Wanasema hoja ya kurejesha mali hizi serikalini ni sehemu ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali, katika ripoti ya kurejesha mfumo wa vyama vingi. Kwa hiyo wao watasimamia mapendekezo hayo.
  Kinana: Mimi sijasoma mapendekezo hayo kiasi hicho lakini siamini kama ni sawa. Ni sawa sawa na kusema kwamba mtu anataka kuoa, anaalika watu halafu wanamchangia na baadaye anasema mimi nadhani huyu mke wako awe mke wetu wote, mimi nadhani ni jambo ambalo haliwezekani, ni jambo gumu.
  Ni bahati mbaya kwao lakini ni bahati nzuri kwetu kwamba tuna viwanja vizuri, tuna ofisi nzuri, tatizo wao hawana kwa hiyo wajiimarishe ili wawe na mali za namna hii.
  Tatizo kubwa ninaloliona wapinzani wanakuwa wanajitokeza na kusikika zaidi wakati wa uchaguzi lakini wana miaka mitano baada ya uchaguzi ya kufungua matawi, kukutana na wananchi, kueleza sera zao, kutembea nchi nzima hawatembei. Mara nyingi wapo kwenye vyombo vya habari ndipo wanakowasiliana na wananchi kwa hiyo uchaguzi unapokuja wanaanza kuzungumza mambo ambayo hayaeleweki kwa wananchi.
  Raia Mwema: Umesema hawaimarishi vyama baada ya uchaguzi. Lakini ukiangaliwa nchi kama Uingereza, hakuna masuala ya matawi ya chama kwa hiyo si jambo la msingi. Mazingira haya unayazungumziaje kwa kulinganisha na hapa kwetu.
  Kinana: Si kweli. Unajua kuna nchi nyingi, sisi kidogo ni tofauti. Mifumo ya vyama vya siasa kwenye nchi nyingi inaendeshwa na wabunge. Yaani wabunge ndiyo chama, ndiyo maana kwa mfano nchi kama Uingereza hakuna kura za maoni miongoni mwa watu wanaotaka kuwa wabunge.
  Chama kinakaa kinatazama mbunge wetu pale yukoje, amekiimarisha chama kiasi gani, ana nguvu kiasi gani na kinakaa kinamteua bila hata kura za maoni, lakini sisi tuna kura za maoni kila mahali kwa hiyo kwa kweli ni tofauti kidogo na unaweza kusema wakati mwingine sisi tuna demokrasia zaidi kuliko wao.
  Kwa sababu sisi hata yule mbunge wetu ambaye ni hodari, mchapa kazi tunampeleka tena kwenye kura za maoni ili kuwapa nafasi tena wanachama wetu ya kumpima na kuona kama kweli amefanya kazi yake vizuri…kama kweli bado anakubalika.
  Lakini zipo nchi nyingi sana duniani ambazo kura za maoni hazipo katika vyama vyao. Mtu anateuliwa tu chama kinakaa, kinafanya tathmini tu kwenye jimbo, wakiona huyu mtu ananguvu anakubalika, wanamteua bila kura za maoni au kuruhusu mwanachama mwingine kushindana naye.
  Raia Mwema: Lakini kuna mifano ya nchi jirani, Mwai Kibaki wa NARC-Kenya au Malawi, Dk. Bingu Mutharika, walishinda bila vyama kuwa na mtandao au matawi. Ni vuguvugu fulani lilikuwapo. Vipi kuhusu mazingira haya?
  Kinana: Lakini vile vile katika nchi zote hizo utaona, nirudie niliyosema awali. Nchi zote hizo ambazo chama kimeshinda kwa haraka haraka kama unavyosema ni kwamba vyama vyenyewe vilivyokuwa madarakani havikuwa vyama hai, havikuwa vyama vyenye demokrasia, havikuwa vyama vilivyokuwa karibu na wananchi ambavyo vilijali maslahi na maendeleo ya wananchi. Havikuwa vyama vyenye uwezo na machinery ya kujisahihisha vyenyewe ili kwenda na wakati.
  Raia Mwema: Kuna nyingine, mara nyingi CCM imekuwa ikitumia wingi wa wabunge wake kulinda maslahi yake na hata kuwatisha wabunge wake. Wagombea wa vyama vingine wanajenga hoja msichaguliwe kutokana na hili, unasemaje?
  Kinana: Unajua kila chama kinapogombea kinakuwa na sera na ilani. Kikishachaguliwa kinakuwa na hiari, kinakuwa na jukumu la kutekeleza yale yaliyoahidiwa kwa wananchi.
  Chama cha upinzani kazi yake kubwa ni kuendeleza shughuli za kipinzani ndani ya Bunge na kama ulivyoona mwenyewe kule ndani, sisi tunatekeleza yetu na wao wakati mwingine kazi yao kubwa ni kusema hapana kwa kila jambo hata kama wakati mwingine hilo jambo ni la busara na faida kwao.
  Tunatumiaje wingi wetu. Lazima tutumie wingi wetu. Dunia nzima iko hivyo. Marekani, Uingereza katika nchi za Latin America, India na nchi nyingi.
  Raia Mwema: Lakini wakati mwingine mmekuwa mkitumia wingi huo kuzima hoja zinazoaminika kuathiri viongozi wenzenu, mkitaka iaminike zinaathiri chama au Taifa. Huko nchi nyingine ni hivyo kweli?
  Kinana: Hapana, si kweli hata kidogo. Unajua kila chama kinaangalia yale mambo kinachosimamia, tumeahidi nini.
  Hivi kweli unategemea sisi tutakaa, tutekeleze sera au ahadi kwa kuangalia matakwa ya chama cha upinzani ndiyo tutekeleze, nadhani si kweli.
  Baadhi ya mambo, hata sisi tunabusara, tunaona yapo, mambo mengine ni kwa manufaa ya nchi ,tunayatekeleza, yapo mengine tunazungumza na wapinzani tunayatilia maanani, si kweli kwamba yote wanayozungumza hayana maana moja kwa moja.
  Ndiyo maana kwa mfano, wao wana nafasi ya kuwa wenyeviti katika Kamati za Bunge ambazo ni muhimu sana, Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma wamo kule na wanatoa ushauri wao na unazingatiwa si kwamba kila wanachosema tunakipuuza.
  Raia Mwema: Wenzenu wanalalamika na wakati mwingine kuitilia shaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Ninyi (CCM) mnasemaje…mnaridhika?
  Kinana: Wenye nafasi nzuri zaidi ya kujibu hilo nadhani ni NEC. NEC ndiyo yenye kuweza kujibu juu ya shutuma dhidi yake kutoka popote.
  Na NEC ni wakali, kwa mfano, hata sisi, wakati mwingine tunataka kubadilisha ratiba wanatukatalia. Mgombea wetu anataka kubadilisha ratiba wanatukatalia, tumekuwa tukichelewa wakati mwingine.
  Raia Mwema: Kwa mfano?
  Kinana: Kwa mfano, hivi karibuni hapa tulikuwa na tatizo. Mgombea wetu ilikuwa atumie helkopta eneo fulani na bahati mbaya helkopta haikuweza kutua eneo lile kwa hiyo alikuwa amechelewa kwa muda mrefu sana tukasema tunataka kubadilisha ratiba na wakasema jamani hatutabadili ratiba.
  Raia Mwema: Unadhani kuna jambo lolote kama mkishinda mnaweza kulichukua kutoka Ilani za CHADEMA na CUF?
  Kinana: Kwa kweli tutawasilikiza, nimesoma mimi ni kwamba sijaona jambo kubwa sana kwanza ni lazima ujue kwamba hawana uzoefu wa uendeshaji wa Serikali na bahati mbaya hawana taaluma pana kama kilivyo Chama Cha Mapinduzi kuweza kuelewa mambo ya msingi.
  Sisi tuna uzoefu wa muda mrefu, tunaelewa yale ambayo yanawezekana na yasiyowezekana.
  Tatizo letu ni kwamba tunaona wamejiingiza kwenye ahadi nyingi ambazo si za kweli na hayo ni makosa ambayo wameendelea kuyafanya tangu 1995 hadi leo, sidhani kama wanakaa na kufanya tathmini ya kutosha kuhakikisha kwamba hawarudii makosa kama hayo na wanawachukulia wananchi kwamba hawawezi kupima, hili ndiyo tatizo jingine.
  Wanafika pale wanasema kila kitu kitakuwa bure, ushuru hautakuwapo…wananchi nao wanao uwezo wa kupima kama gharama za uendeshaji zitakuwa bure utasema ushuru hautakuwapo na kila kitu kitakuwa bure, gharama za uendeshaji zitatoka wapi.
  Wao wanafikiria tu kwamba ni jambo zuri kuwaeleza wananchi na watawachagua, nadhani wananchi nao uwezo wao wa kuelewa mambo ni mkubwa sana na sisi hilo katika kipindi chetu cha miaka kadhaa kwenye uongozi imetudhihirishia kwamba wananchi ni waelewa wazuri sana.
  Raia Mwema: Sekta gani unadhani Rais Kikwete amejitahidi na zinaweza kutumika kama kigezo cha kuongeza kura zake.
  Kinana: Ukitazama katika eneo la biashara, mauzo ya nje wakati anaingia madarakani ilikuwa Sh bilioni moja lakini kwa wakati huu imefikia Sh bilioni 1.2 dola za Marekani na ukitazama kwa mfano vitu kama viwanda.
  Alipoingia madarakani, uwezo wa viwanda kufanya kazi ilikuwa Sh bilioni 1.8 lakini leo hii mauzo yetu ya nje ni bilioni nne na laki mbili kwa hiyo ni zaidi ya mara tatu kwa hiyo kuna ukuaji wa hali ya juu sana.
  Ukichukua kwa mfano viwanda vya nguo, nguo ambazo tulikuwa tunazalisha wakati anaingia madarakani thamani yake ilikuwa Sh bilioni 171, leo ni Sh bilioni 410.
  Ukitazama viwanda vyetu uwezo wa uzalishaji ulikuwa ni asilimia 30 sasa ni asimilia 62 kwa hiyo kuna ongezeko kubwa sana.
  Ngozi kwa mfano uzalishaji ulikuwa kutoka mita za mraba milioni sita kwenda milioni 37 kwa ngozi zinazosindikwa nchini, hii ni karibu mara tano ya uwezo.
  Kwa hiyo tumeweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.
  Sekta ya elimu: Shule za sekondari kutoka 1700 mwaka 2005 hadi 4,200. Ukichukua uwiano kati ya mwalimu na mwanafuzi wakati Jakaya Kikwete anachukua Serikali ilikuwa mwalimu mmoja wanafunzi 84, sasa hivi mwalimu mmoja wanafunzi 54 na kufikia 2014 itakuwa mwalimu mmoja wanafunzi 45.
  Walimu ambao wamekuwa wakipatikana kwenye vyuo vyetu mbalimbali wakati Jakaya Kikwete anaingia madarakani walikuwa chini ya 1,000 lakini leo hii kwa mfano mwaka huu watapatikana walimu 15,000 kutoka vyuo mbalimbali.
  Raia Mwema: Pamoja na idadi kuongezeka, tatizo ni kwamba walimu hawabaki kufanya kazi ya ualimu kutokana na maslahi. Huoni mnabaki na takwimu ambazo hazitatui tatizo.
  Kinana: Hapana, nadhani wengi wao wanabaki labda tu muda unakuwa mdogo kwa sababu kuna masharti ambayo mtu ni lazima atekeleze.
  Utagundua kuwa nadhani miaka mitatu imepita Rais Kikwete alisema kwamba yuko tayari kutoa mikopo kwa ajili ya wanaosemea ualimu ili kupata wengi ili kuondoa tatizo la walimu.
  Lakini kufikia mwaka 2015 tatizo la walimu nchi hii litakuwa limemaliza na yatakuwa mafanikio makubwa saa hata ukichukua kwa mfano uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza sasa hivi tumefikia asilimia 80 na kufikia 2014 wanafunzi wote wenye umri wa kwenda shule watapata nafasi ya kwenda shule.
  Lakini suala la mikopo ni eneo lenye mafanikio, mikopo kwa wanafunzi wakati anachukua madaraka ilikuwa Sh bilioni 56 leo ni bilioni 197 na asilimia 96 ya wanaopata mikopo wanatoka kwenye familia zilizo masikini sana. Kwa hiyo ni mafanikio pia kwa upande wa Kikwete.
  Vitivo vitatu vya masuala ya afya vitaanzishwa kimoja katika Chuo cha Afya Muhimbili kitakachofamishiwa Mkoa wa Pwani, kitakuwa Chuo Kikuu cha afya, pale Dodoma kitawekwa kitivo maalumu kwa ajili ya kuzalisha madaktari.
  Katika sekta ya afya ukiangalia eneo la afya kuna mfuko umeanzishwa unaitwa Mfumo wa Afya ya Jamii ambao unawahudumia Watanzania kwa asilimia 18 kufika 2015 asilimia 40 ya Watanzania watakuwa wamefikiwa na mfuko huu.
  Lakini pia kuna mpango unaitwa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ukihusisha ujenzi wa vituo vya afya katika kila kata. Kutakuwa na Hospitali za Rufaa katika kila Mkoa, kutakuwa na huduma zilizoimarishwa, vyuo vitatu vingine vikuu vya masuala ya afya.
  Katika suala hili la afya pia chini ya uongozi wa Kikwete tumepunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 95 kwa kila watoto 1,000 leo ni 58 na lengo ni sifuri kufikia 2015.
  Na suala la maji safi na salama, hatua kubwa imepigwa alipochukua uongozi asilimia 58 ya wananchi vijijini walikuwa wakipata maji safi na salama lakini leo ni asilimia 65 na idadi hii itaongezeka hadi asilimia 70 mwaka 2015.
  Kwa maeneo ya mjini ni asilimia 81 na itakapofika 2015 karibu asilimia 95 ya Watanzania watakuwa wamefikiwa na huduma hii ya maji safi na salama mijini.

  Kwa hiyo lazima tukiri kuwa Rais Kikwete amepiga hatua kubwa sana katika maeneo mengi, hata Miundiombinu tumejenga barabara nyingi na 2015 mikoa yote itakuwa imeunganishwa kwa lami na wilaya kwa wilaya kutakuwa na barabara za uhakika.
  Lakini kuna suala la vyombo vya habari. Rais Kikwete amekuwa mvumilivu na amepanua sana uhuru wa vyombo vya habari, leo ukitaka kusoma magazeti ya kila siku utalazimika kununua magazeti 14, kuna magazeti ya wiki … kuna redio zaidi ya 95 karibu kila mkoa una redio yake, kuna televisheni nyingi sana.
  Watanzania wanapata habari zaidi na kwa hiyo ameongeza uhuru mkubwa sana katika vyombo vya habari na uvumilivu mkubwa jambo ambalo kwa viongozi wengine wa Afrika si jepesi.
  Rais Kikwete ni mtu mvumilivu, muungwana na anaheshimu maoni na wakati mwingine anaheshimu maoni kuliko hata yake mwenyewe na kwa hiyo naamini atachaguliwa kwa asilimia zaidi 80.
  Raia Mwema: Zipo hoja za Dk. Slaa zinazogusa moja kwa moja wananchi, kuna kupunguza mishahara ya wabunge na Rais. Unazungumziaje haya?
  Kinana: Dk. Slaa amezungumzia mambo matatu ambayo mimi nadhani hayana msingi sana.
  Kwa mfano anasema atakapochaguliwa atapunguza asilimia 15 ya mishahara ya wabunge. Ukichukua wabunge 300 ukachukua asilimia 15 ya mshahara wao na akasema mshahara huu utasaidia kuboresha mazingira na mishahara ya wafanyakazi.
  Tunao wafanyakazi wanaokaribia nusu milioni sasa ukipunguza asilimia 15 ya mshahara wa Sh labda milioni tano ya mbunge ina maana kwamba unaopunguza kwa shilingi 750,000.
  Sh 750,000 mara watu 300 ni unatapa Sh milioni 200 na zaidi ni fedha ndogo sana sijui unawezaje kuboresha mishahara ya wafanyakazi au mazingira yao kwa fedha hizo. Kwa hiyo ni kuchukua vitu vidogo vidogo ambavyo masikio mwa wananchi vinaleta raha lakini havina tija.
  Amesema nakata mshahara wa Rais kwa asilimia 20, mimi nilifikiri anaondoa kabisa mshahara wa Rais labda angeeleweka vizuri zaidi. Rais yeyote duniani, hasa Rais wa Tanzania hana mshahara, Rais anaishi kwa marupurupu zaidi kuliko mshahara.
  Sasa anasema ataondoa asilimia 20 ya mshahara wa Rais, tuchukue kwa mfano Rais analipwa Sh milioni 10 ina maana ataondoa Sh milioni mbili tu kwa mwezi, kwa mwaka ni Sh milioni 24.
  Sasa ukiondoa Sh milioni 24 kwenye mshahara wa Rais inasaidia nini kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Huu ni udanganyifu na hadaa kwa wananchi.
  Lakini jingine ambalo amekuwa akilizungumza na nimekuwa nikilisikia ni kwamba wabunge wanalipwa mshahara mkubwa sana na Spika wa Bunge anajilipa marupurupu makubwa pamoja na kujenga ofisi yake kama Mbunge wa Urambo.
  Jambo moja ambalo Watanzania hawajui na ningependa walijue ni kwamba mara baada ya haya yote yanayofanyika bungeni, mishahara anayosema mikubwa, kujenga ofisi za wabunge na kuanzisha mfuko wa Jimbo haya ni mapendekezo ambayo yameletwa na kukubaliwa na Dk. Slaa mwenyewe.
  Kwa nini? Spika wa Bunge aliunda Tume ya watu saba kuangalia uendeshaji wa Bunge pamoja na maslahi wa wabunge Dk. Slaa alikuwamo.
  Hiyo kamati ilikuwa na watu saba, CCM watano na wawili kutoka Kambi ya Upinzani Bungeni, ambaye ni Dk. Slaa na Hamadi Rashid Mohamed. Wamezunguka nchi mbalimbali duniani kuangalia wabunge wana maslahi gani, wanauwezo kiasi gani, wanahuduma kiasi gani na marupurupu kiasi gani.
  Sasa Dk. Slaa na wenzake ndiyo waliopitisha mapendekezo haya ambayo analalamikia. Alikuwamo kwenye mapendekezo hayo yaliyopitishwa bungeni kwa ushawishi wake.
  Haiwezekani akubali hayo mapendekezo halafu arudi kwa wananchi kuwaambia kwamba hiki kinacholipwa kwa wabunge ni kibaya.
  Na alikuwa anapokea mshahara na hata siku moja sijasikia akikataa mshahara au kuchukua na kupeleka kwenye NGO fulani inayosaidia watu masikini. Sasa huko ni kuhadaa watu.
  Reli: Jingine amesema kwamba akiingia madarakani atajenga reli, treni itoke Mwanza kwenda Dar es Salaam ikitumia saa tatu. Duniani hakuna treni ya aina hiyo.
  Kuna treni inaitwa Bullet Train (yenye umbo la risasi) ya Japan ambayo kwa mwendo huu anaosema Dk. Slaa itachukua karibu saa 10. Kuna treni ya Kifaransa inaitwa TGV, yaani treni inayokwenda kasi sana kuliko nchi yoyote za Ulaya na kwa hesabu nilizopiga (kutoka Dar-Mwanza) inachukua zaidi ya saa sita lakini yeye amesema saa tatu. Huku ni kuhadaa watu, unajua unapokaa majukwaani si vizuri kudanganya watu na ndiyo maana nasema Kikwete atapa kura nyingi.
  Lakini la mwisho ni kwamba Dk. Slaa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, amekuwa akipokea marupurupu hata siku moja sikusikia akilalamikia marupupurupu hayo.
  Amekuwa akilipwa fedha nyingi na posho kama mwenyekiti wa kamati. Amekuwa akipata takrima na usafiri, sijasikia akikataa, aeleze sera zake asizungumzie haya.
  CHADEMA kinaamini katika mrengo wa kulia, chama kinachoamini siasa na sera za kibepari na utakumbuka wakati kinaanzishwa CHADEMA na waasisi wake walikuwa wakipinga sera za siasa za ujamaa, wakitetea sera za ubepari.
  Walikuwa wakipinga serikali kumiliki mashirika ya umma au kampuni si sawa ni vizuri kuyaweka kwenye mikono ya watu binafsi, kutoa huduma za afya na elimu bure serikali isifanye hivyo.
  Hata ukiangalia Katiba yao ndivyo inavyosema inazungumzia juu ya siasa za kuendeleza watu binafsi na si wananchi kwa ujumla. Sasa kauli anazotoa Dk. Slaa hadharani hazifanani na maudhui ya kimsingi yaliyoko kwenye Katiba ya CHADEMA.
  Kauli ya kuaminika na ambayo historia imethibityisha ni kwamba CCM kinajali wananchi wake, kinatoa huduma za msingi kwa watu. Dk. Slaa inawezekana anaamini masuala haya katika mwelekeo wa CCM kusaidia wananchi lakini watu wanaomzunguka si waumini wa siasa za huduma bure kwa wananchi ni watu wanaoamini katika siasa za kibepari.
  Hata ukitazama ushirikiano wa CHADEMA na vyama vilivyoko nje ya nchi, ushirikiano wao unahusisha vyama vya kimwinyi.
  Wako karibu zaidi na vyama vya Republican (Marekani), Conservative (Uingereza) na vyama vya kimwinyi vya Uholanzi, Ujerumani na Australia kwa hiyo wasidanganye wananchi.
  [​IMG]

  Simu:
  0787-643151​
   
Loading...