Watanzania watumia mamilioni kutafuta watoto Kenya

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,007
Watanzania watumia mamilioni kutafuta watoto Kenya Thursday, 20 January 2011 21:29

joycemtoto.jpg

JOYCE NOREH AKIWA NA MTOTO ALIYEPATIKANA KWA NJIA YA IVF

Na Florence Majani
Mwananchi

WAKATI wengine wanatupa watoto chooni, katika mito au majalalani wengine wakikataa ujauzito huku baadhi wakitoa mimba, wapo wanaohangaika mchana na usiku wakitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutafuta watoto.

Ukosefu wa watoto umekuwa na athari kubwa kwa wanandoa na hata wale walio katika uhusiano wa kawaida, baadhi ya ndoa zimevunjika, wanawake kunyanyasika, kuathirika kisaikolojia na baadhi kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa waganga wa kienyeji au kwa madaktari bingwa wa uzazi.

Moja ya njia ambazo wanandoa wamekuwa wakizitumia kutafuta watoto ni upandikizaji wa mbegu ‘In Vitro Fertilization'(IVF).

Mmoja wa wataalamu wa masuala ya uzazi, Dk Joshua Noreh kutoka Kituo cha Upandikizaji Mbegu Nairobi, (Nairobi IVF Centre) anasema, asilimia 10 ya wanaofika kituoni kwake kutafuta huduma hiyo hutoka Tanzania.
Dk Noreh anasema wastani wa wagonjwa 100 hufika kwa ajili ya ushauri wa mara ya kwanza na nusu yao hurudi kwa matibabu kila mwaka.

Wagonjwa kutoka Tanzania walianza kumiminika katika kliniki hiyo kuanzia mwaka 2006 na kwa kawaida hutumia kiasi kikubwa cha fedha.

Dk Noreh anasema, gharama ya ushauri peke yake ni kiasi cha Sh42,000 za Tanzania.
"Baada ya ushauri, mgonjwa hutozwa kiasi cha Sh420,000 kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo, gharama za matibabu hutegemea ukubwa wa tatizo na kwa kawaida hugharimu kiasi cha kuanzia cha Sh210,000 kwa upandikizaji (insemination) hadi milioni saba za kitanzania kufikia hatua ya kuirutubisha mbegu iliyopandikizwa."

Dk Noreh anasema ukijumlisha gharama za usafiri, malazi, mlo na tiba kwa wagonjwa wanaotoka Tanzania, wengi wao hutumia kati ya Shmilioni nane hadi 10 kwa ajili ya kutafuta watoto.

Anasema Watanzania hutumia mwezi mmoja au zaidi kwa ajili ya huduma hiyo wakifika Kenya kwa sababu ya namna ya tiba ilivyo na mwili wa mwanamke na kuongeza kuwa wengi wao ni wale wenye umri unaozidi miaka 18 na zaidi ya 35.

"Tiba huchukua mwezi mmoja, huanzia siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza hedhi na siku ya yai kurutubishwa lakini mwanamume hutumia siku moja tu pale mbegu zake zinapohitajika."

Anasema sababu ya kuanza tiba siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza mzunguko wake wa mwezi ni kulenga tarehe za uchavushaji, kwani kipindi hicho mbegu za mwanamume hupandikizwa na kusababisha mimba kutungwa.

"Mbegu zilizorutubishwa huachwa kwa siku mbili mpaka tano ndani ya chombo maalumu ili kukuza kiinitete (embryo) kabla ya kuhamishwa katika nyumba ya uzazi ya mwanamke kwa ajili ya kutungisha mimba ya kawaida," anasema Dk Noreh.

Anasema tatizo la ugumba linaongezeka duniani na njia hiyo inatumika kuwasaidia wanawake wasiokuwa na mayai ambao mirija yao ya kuyasafirishia imeziba na wanaume ambao manii yao ni dhaifu na hushindwa kuogelea hadi kufikia yai la mwanamke.

"Tatizo la ugumba kwa sasa ni wastani wa asilimia 10, hiyo ina maana kwamba katika pea za wanandoa 10 mmojawapo hana uwezo wa kushika mimba. Kiwango hiki kwa sasa kinakua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wanawake wa sasa kuchelewa kuolewa wakitoa kipaumbele kumalizia masomo," anasema Dk Noreh.

Dk Noreh anataja sababu za ugumba na kusema hutofautiana katika maeneo mbalimbali ulimwenguni, lakini kubwa ni mayai kushindwa kurutubishwa, mirija ya mwanamke kuziba na udhaifu wa mbegu za kiume ndizo zimekithiri katika nchi zinazoendelea.

"Nyingine ni uvutaji wa sigara, utoaji mimba, magonjwa ya zinaa, wakati mwingine tatizo hili huchochewa na umaskini kwani baadhi hushindwa kumudu gharama za matibabu," anasema Dk Noreh.

Baada ya huduma hiyo inayogharimu kiasi kikubwa cha fedha kila mmoja hutarajia matokeo mazuri, lakini sivyo inavyotokea kwa wote.

"Furaha na matumaini ni jambo la kawaida kwa wale wanaoshika mimba, lakini msongo wa mawazo huwakumba wale ambao mimba zao hutoka au kutoshika kabisa. Lakini sisi huwapa ushauri wa kisaikolojia kwanza kabla ya matibabu ili kuwatayarisha kwa matokeo wasiyoyatarajia. Hata hivyo, zoezi hufanikiwa kwa asilimia 40" anasema.

Anasema wateja hutaarifiwa awali kuwa kuna uwezekano wa kurudia upandikizaji hata zaidi ya mara nne endapo hawakufanikiwa mara ya kwanza lakini gharama hutozwa kwa kila moja.

Hata hivyo, Dk Solomon Wasike wa Kituo cha Upandikizaji cha Afya Royal Clinic anasema kwamba hatua za kumtoa mbegu mwanamume ama kwa kujichua au sindano, huwakera wengi na kuwafanya wasite kurudia utoaji mbegu.

Hata hivyo, Dk Noreh anasema wanaume wengi wa Kitanzania hutoa ushirikiano mkubwa pindi wanapokuja na wenzi wao kupata matibabu.

Mtanzania mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini anasema yeye na mumewe walipoingia ndani ya chumba cha daktari kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini walikuwa na mategemeo lukuki kuwa watapata mtoto lakini mambo hayakwenda hivyo.

"Tumesafiri nchi nyingi, Afrika Kusini, Uingereza na hatimaye tumefanikiwa hapo Nairobi lakini hiyo ni baada ya kutumia Sh milioni nne za Kenya na tumeanza kuhangaika tangu mwaka 2006," anasema.

Anasema ulifika wakati alikata tamaa ya kupata mtoto wa kumzaa kwani alihangaika kwa muda mrefu akitumia kiasi kikubwa cha fedha.

"Huwezi kuamini mpaka sasa bado nalipa baadhi ya mikopo ya pesa nilizokopa nikitafuta mtoto," anasema huku akitabasamu kwani angalau ameona matunda ya uwekezaji wake na sasa ana mtoto wa kike wa miezi 10.

Wanasayansi wanasema wakati mwingine upandikizaji hufeli kutokana na udhaifu wa mayai ya mwanamke, mbegu za kiume na kiini tete; umri wa mwanamke, kiwango cha nyumba ya uzazi; aina ya maisha na mazingira.

Wanasema ushirikiano hafifu kutoka kwa mume pamoja na kutofuata masharti pia vinaweza kusababisha upandikizaji kufeli.

Mtoto wa kwanza kupatikana kwa njia hiyo alizaliwa Julai 1978 huko Uingereza na inasadikiwa kwamba yupo hai na hana tofauti na binadamu wengine.
 
Back
Top Bottom