Watanzania wahimizwa kuzuia maambukizi mapya ya VVU | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Watanzania wahimizwa kuzuia maambukizi mapya ya VVU

Discussion in 'JF Doctor' started by MziziMkavu, May 31, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 31, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  WATANZANIA wametakiwa kuweka juhudi katika kudhibiti na kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi wakati tayari kukiwa na kampeni ya kuzuia maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

  Rais Jakaya Kikwete alitoa changamoto hiyo jana wakati akifungua kongamano na mkutano wa mwaka wa Umoja wa Wabunge wa Tanzani kupambana na Ukimwi (TAPAC) katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

  Alisema zinahitajika juhudi za mtu binafsi hadi taifa zima ili kuhakikisha maambukizi mapya yanazuiwa na kwamba hapo vita dhidi ya Ukimwi itakuwa imedhibitiwa na kufanikiwa vizuri.

  “Tumefanikiwa kupunguza maambukizi ya Ukimwi lakini sasa vita yetu ielekezwe katika kuzuia maambukizi mapya na hapo tutajivunia kuwa tumepiga hatua kubwa…ninachowasihi tuelekeze sasa nguvu zetu katika kuzuia maambukizi mpya lakini haina maana kuwa wale waliokwisha ambukizwa tunaawacha,” alisema.

  Rais Kikwete alisema juhudi mbalimbali zimesaidia kushuka kwa maambukizi kutoka asilimia saba hadi kufikia asilimia 5.6 kwa maana kwamba katika watu wazima 100 watano wameathirika na kuongeza kuwa bado juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha hayatokei maambukizi mapya.

  “Kuna mikoa tatizo hili limepungua sana lakini huko huko bado unakuta baadhi ya sehemu maambukizi bado ni makubwa, kwa hivyo ari na nguvu zaidi inahitajika, kwa maana hiyo inapaswa hilo litambulike ili juhudi zaidi ziongezwe,” alisema.

  Rais Kikwete alisema vita dhidi ya Ukimwi ni ya kudumu na hivyo inapaswa iwepo mikakati mingine ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, afya ya uzazi na unyanyasaji wa kijinsia.

  Alisema serikali imedhamiria kuhakikisha kila kijiji kinapata zahanati na kata inakuwa na kituo cha afya ili kusogeza huduma karibu na wananchi ambapo itasaidia pia kupunguza vifo vya akinamama wajawazito hasa ikizingatiwa Tanzania ni moja ya nchi yenye vifo vingi vya wanawake ambapo kwa mwaka wanawake 578 kati ya wanawake 100,000 hupoteza maisha.

  Rais Kikwete alitoa wito pia kwa wizara husika kuweka mtaala wa kuelimisha watoto mashuleni kuhusu maambukizi ya Ukimwi na namna ya kuchukua tahadhari na alikemea pia tabia ya watu kuwabagua na kuwanyanyapaa waathirika wa Ukimwi na kuongeza kuwa vitendo hivyo vimechangia watu kuogopa kwenda kupima afya zao kwa kuhofia kunyooshewa vidole.

  Mwenyekiti wa TAPAC, Lediana Mng’ong’o alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa umoja huo ilikuwa ni kuhamasisha na kuwaelimisha wabunge ili waweze kuhamasisha wananchi kupambana na maambukizi ya Ukimwi.

  Mng’ong’o alisema kwa kuwa rasilimali za Ukimwi zimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutoka kwa wafadhili ni muhimu serikali kuanzisha Mfuko wa Kupambana na Ukimwi kama ilivyoainishwa katika Sera ya Ukimwi ya mwaka 2001 pamoja na suala la unyanyasaji wa kijinsia na afya ya uzazi lipewe kipaumbele.

  Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) Louise Chamberlain aliwataka wabunge wanapoelekea katika kampeni za uchaguzi kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuongeza juhudi kupambana na maambukizi ya Ukimwi.

  Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Marekani(USAID), Robert Cunnane alisema ingawa serikali katika msimu huu wa bajeti imetoa kipaumbele katika sekta ya kilimo aliitaka isipunguze bajeti yake katika Wizara ya Afya.

  Rais Kikwete pia alitunukiwa Tuzo ya Uongozi uliotukuka katika mapambano dhidi ya Ukimwi kutokana na mchango wake katika vita dhidi ya Ukimwi.
   
Loading...